Kwa maendeleo makubwa ya kiteknolojia dunia iliyofikia mtandao umekuwa rahisi sana kupatikana kwa watu wengi. Tofauti na ilivyokuwa zamani, sasa mtu anaweza kutumia mtandao kwa kutumia simu ya mkononi.

  Maendeleo haya makubwa yamepeekea kuwepo kwa mitandao ya kijamii. Mitandao hii imerahisisha sana mawasiliano kwani kwa sasa unaweza kuwasiliana na mtu yeyote popote alipo duniani kwa gharama nafuu na kwa haraka kama vile mpo ana kwa ana.

  Mitandao ya kijamii pia imerahisisha sana biashara ndani na nje ya mataifa.

  Kwa sasa inasemekana kuna mitandao ya kijamii zaidi ya mia mbili (200) duniani. Mitandao ya kijamii maarufu sana duniani ni Facebook, Twitter, LinkedIn, Pinterest, Instagram, Google plus+, My space na Orkut

mitandao3social ntw4

  Mitandao ya kijamii yenye watumiaji wengi kutoka Tanzania ni Facebook, Twitter, LinkedIn, na Google plus+

  Pamoja na uzuri na faida nyingi za mitandao hii ya kijamii kuna watu wanateseka sana na mitandao hii. Unaweza kuwa mmoja wa wanaoteswa na mitandao hii ila ni vigumu kujua kama unateswa. Unaweza kuona ni kitu cha kawaida tu ila ni mateso makubwa.

  Kuna watu wanakaa kwenye hii mitandao zaidi ya masaa matano kwa siku. Kuna wengine hayawezi kupita masaa mawili bila ya kuingia, wengine saa moja tu wanajihisi kuumwa kama wasipoingia kwenye mitandao hii. Na imekuwa rahisi sana kuingia kwenye mitandao hii kwa sababu hata visimu vya mchina vinaingia facebook na twitter bila shida yoyote.

mitandao5

  Kama huwezi kujipangia muda wa kuingia na kutoka kwenye mitandao hii basi wewe ni mmoja wa wanaoteswa na mitandao hii. Kama kila unapoingia inakuwia vigumu kutoka, hapo umeshakuwa mtumwa.

  Tatizo kubwa la utumwa wa mitandao ya kijamii ni wa kisaikolojia hivyo napokwambia wewe ni mtumwa inakuwia vigumu sana kunielewa.

mitandao11

  Binadamu tuna tabia ya kutopenda kupitwa na jambo, hivyo unapoingia kwenye mitandao hii hasa facebook au twitter, kila unapoperuzi unakutana na habari nzuri zaidi ama mabishano unayopendelea. Kidogo kidogo unazama na kuendelea kuperuzi mwishowe unasahau hata kutoka.

mitandao6

  Tabia nyingine ya binadamu ni kupenda kujua kinachoendelea kwenye maisha ya wengine. Watu wanapenda sana kujua fulani kafanya nini kwenye maisha yake, hasa huyo fulani anapokuwa ni mtu maarufu. Kwa kutaka kupata habari zaidi kuhusu watu unajikuta unapotumia muda mwingi kuangalia profile na status za watu.

  Kuna hisia fulani mtu unazipata pale unapokuwa hujaingia kwenye mitandao hii kwa muda, unahisi kama unapitwa na mambo fulani, unahisi kuna habari mpya umezikosa na kadhalika, hii inakupelekea kutamani kuingia kuchungulia nini kinaendelea kwenye mtandao. Kwa bahati mbaya pale tu unapchungulia unamezwa na hizo tabia za kutaka kujua zaidi na unajikuta inakuwia ngumu kutoka.

mitandao9mitandao10

  Kama unatumia zaidi ya masaa mawili(muda usio wa kazi) kwa siku kwenye mitandao ya kijamii na hakuna biashara yoyote unayoifanya kupitia mitandao hiyo basi wewe umeshakuwa mtumwa wa mitandao ya kijamii. Kama hakuna hata shilingi mia unayoingiza kupitia facebook basi unapoteza muda wako kwa mambo ambayo hayana uhusiano kabisa kwa wewe kufikia malengo yako. Kama unaijua thamani ya muda wako(kama hujui soma; unajua thamani ya muda wako) basi hakikisha muda wa kazi unaoutumia facebook unakuingizia fedha kulingana na viwango vyako.

mitandao7

  Kama umeshakuwa mtumwa wa mitandao ya kijamii unaweza kujikomboa kama ukiamua kufanya hivyo. Ili kujikomboa na utumwa huo ni bora ukabadili tabia zako kwenye mitandao ya kijamii. Ni vigumu sana kubadili tabia hizo kwa haraka, ila unaweza kubadili muda unaoutumia kwenye mitandao kwa kufanya kitu kingine kitakachokuwa na faida kwako.(soma; jinsi ya kubadili tabia)

  Tuitumie mitandao hii kwa manufaa ya kupata habari na kuwasiliana na ndugu jamaa na marafiki. Ila tusikubali mitandao hii kututawala. Lazima uwe na uwezo wa kuamua ni muda gani wa kuingia na ni muda gani wa kutoka. Kama hutengenezi fedha kwenye mitandao hii hakuna unachweza kupoteza kwa kutoingia hata kwa siku tano. Kama huamini jaribu kutokuingia na kutokuweka mawazo yako ni nini kinaendelea kwenye mitandao hiyo kwa siku moja. Utapata ahueni kubwa sana na utajikuta unakamilisha mipango yako mingi.