Mara nyingi tunaposhindwa kufikia malengo tuliyojiwekea huwa tunatafuta sababu. Na mara nyingi huwa tunaishia kutafuta wa kumlaumu.
Katika kutafuta sababu za kushindwa kufikia malengo fulani wengi wetu hupata sababu kwamba kuna vitu wamekosa ndio maana wameshindwa kufika walikotaka kufika. Na mara nyingi sababu tunazoona tumekosa ni baada ya kujilinganisha na wenzetu waliofanikiwa. Hivyo unapomwangalia aliefanikiwa na wewe umeshindwa jibu rahisi linakujia kwamba yeye ana hiki ama kie ambacho wewe huna.
Unaweza kusema labda huna elimu ya kutosha ama huna fedha za kutosha na sababu nyingine lukuki, ila hakuna hata sababu moja ya kweli.
Kama umeweza kusoma hapa basi una kila unachohitaji ili uweze kufikia mafanikio yako. Kuna watu wengi wamepata mafaniko makubwa na hawana tofauti kubwa na wewe. Na kuna wengine wamekosa hata hivyo ulivyonavyo na bado wameweza kufikia mafanikio makubwa.
Kikubwa unachhitaji ili kufikia malengo yako ni kufanya maamuzi thabiti. Njia pekee ya kukufikisha kule unakotaka ni kuamua kutobaki hapo ulipo. Hivyo weka malengo na mipango(ambayo tayari unayo) na kisha amua kufikia malengo hayo. Tumia kila kinachokuzunguka kufika kule unakotaka kwenda. Tumia uwezo na vipaji vyako vya pekee kufikia malengo yako.
Usipoteze muda mwingi kuangalia ni nini umekosa bali tumia muda huo kupanga njia bora za kutumia ulivyonavyo ili kufikia malengo yako.