Hakuna binadamu aliekamilika, kila bindamu ana mapungufu yake na kila mmoja ana madhaifu yake. Pamoja na kutokamilika huko bado hakutupi sababu ya kufanya mambo ya hovyo, tunategemea binadamu mwenye akili timamu afanye mambo yanayokubaika katika jamii.
Unapofanya jambo lolote ambalo liko kinyume na jamii hata kama limetokana na mapungufu yako, utaangaliwa wewe kama wewe na sio mapungufu yako. Utahukumiwa wewe na hakuna popote unakoweza kujitetea kwamba mapungufu ama udhaifu wako ndio umesababisha wewe ufanye ulichofanya.
Kutokana na jamii kutokujali mapungufu yako ni vyema kujitahidi kuwa bora kila siku. Kila siku badili kitu fulani kwenye maisha yako kitakachopunguza udhaifu na mapungufu yako. Kila siku unayoianza panga kuwa mtu bora zaidi ya jana na boresha kila eneo la maisha yako.
Unapata faida gani kwa kuaboresha maisha yako?
Kuna faida nyingi unazozipata kwa kuboresha maisha yako kila siku, baadhi ya faida hizo ni;
Kuweza kufikia malengo yako kwa muda uliweka. Kama ukiweza kuaboresha maisha yako ukaondokana ama ukapunguza udhaifu wako inakuwa rahisi sana kwa wewe kuweza kufikia malengo yako.
Kubadili na kunufaisha jamii inayokuzunguka. Kwa wewe kuwa bora kuna msaada mkubwa sana kwa jamii yako. Wanajamii wataiga mazuri unayofanya na pia uhalifu utapungua kwenye jamii yako.
Kwa wewe kuwa bora kutakufanya uyafurahie maisha na uwe na sababu ya kwa nini unaishi. Ukiweza kuyadhibiti mapungufu yako, na ukaweza kuisaidia jamii yako ni sababu tosha ya wewe kufurahia maisha yako. Ni vigumu sana kuyafurahia maisha kama kila mtu anakusema kwa tabia zako mbaya.
Japo hatuwezi kuwa wakamilifu kwa asilimia 100, tuna uwezo wa kudhibiti sehemu kubwa ya matendo yetu. Kila siku jitahidi kuyaboresha maisha yako. Kama kuna tabia zinafanya maisha yako yawe ya hovyo zibadili mara moja(soma; jinsi ya kubadili tabia).
Huwezi kufikia malengo yako kwa kuwa na maisha ya hovyo. Ni lazima maisha yako yawe ya maana ndio uweze kukaa na kupanga mipango ya kufikia maengo uiyojiwekewa. Ongeza thamani ya maisha yako kwa kuyaboresha kila siku.