Leo ni siku muhimu sana kwenye maisha yako, leo ndio siku pekee unayoweza kuiathiri, leo ndio siku ya mafanikio yako.
Mafanikio yoyote hayatokei kwa mara moja tu, mafanikio ni mjumuiko wa vitu vidogo vidogo ambavyo kwa pamoja ndio mafanikio. Ili kufikia mafanikio ni lazima kila siku kufanya vitu vinavyokupeleka kwenye mafanikio. Mafanikio yanatokana na mjumuisho wa vitu unavyofanya kila siku.
Leo ni siku muhimu kwako kuyafikia mafanikio yako kwa sababu utakachofanya leo ni cha muhimu sana kwenye maisha yako. Unaweza kuamua kuyabadili maisha yako leo kuwa bora ama kuwa hovyo. Maamuzi na mambo yote unayoyafanya leo yana athari kubwa kwenye maisha yako.
Leo pekee ndio siku unayoweza kuiathiri, jana imeshapita na kesho bado hujaiona. Usipoteze muda mwingi kusumbukia siku ya jana, tayari imepita na hakuna unaloweza kulibadili, cha msingi ni kujifunza kutokana na siku hiyo iliyopita. Kama kuna jema ulilofanya liendeleze, kama kuna ovu ulilofanya liepuke. Pia usipoteze muda wako mwingi kuhofu kesho itakuwaje kwa sababu hata ukihofu kwa kiasi gani bado huwezi kuiathiri ama kuibadili siku ya kesho. Jambo la msingi kuhusu kesho ni kuipanga vizuri na kutegemea kufanya makubwa, na sio kuihofia.
Leo ndio leo, mambo yote yako leo, chochote unachokitaka utakipata kwa juhudi utakazofanya leo. Hakikisha leo umefanya jambo kubwa la kukusogeza kwenye mafanikio. Anza leo kufanya kile ambacho umekuwa unapanga kufanya kila siku ila bado hujaanza kukifanya.
Usikubali siku ya leo ipite hivi hivi bila kuwa na athari kwenye maisha yako. Ifanye leo kuwa siku ya kihistoria kwenye maisha yako kwa kufanya maamuzi sahihi yatakayokufikisha kule unakotaka kuelekea.