Kuna mambo mengi sana ya kufanya mpaka kufikia malengo tuliyojiwekea. Na mafanikio hayatokei kwa siku moja tu, bali ni mwendelezo wa mambo madogo madogo yaliyofanywa kwa muda mrefu kwa kurudiwa rudiwa.

  Ili kufikia malengo tuliyojiwekea ni lazima kuwa na mipango madhubuti. Mipango hiyo ndio inayokuongoza na kujua vitu gani ufanye ili kufikia malengo yako.

lazima kufanya

  Sio vyote unavyotakiwa kuvifanya ili ufikie malengo yako utakuwa unafurahia kuvifanya. Kuna baadhi ya vitu utakuwa hupendi kabisa kuvifanya kutokana na wewe kutokuwa na mazoea ya kuvifanya. Pamoja na wewe kutopenda kufanya mambo hayo, ni muhimu sana kwa wewe kuyafanya la sivyo itakuwa ngumu kwako kufikia malengo yako.

  Kwa kuwa hatupendi kufanya mambo hayo, mara nyingi huwa tunapoteza muda mwingi sana kufikiria jinsi ya kuyafanya. Mara nyingine huwa tunatafuta sababu za kukwepa kufanya mambo hayo ili tu muda upite na tusiyafanye. 

  Kwa mfano ni muhimu kwa wewe kujisomea ili kuongeza maarifa yako na kujua mengi zaidi. Lakini inawezekana hupendi kujisomea hivyo kila unapopanga muda wa kujisomea unapata jambo jingine unalohisi ni la muhimu zaidi kufanya. Au unaweza kuona leo umechokachoka hivyo utasoma kesho ukiwa na nguvu za kutosha, na kama tunavyojua kesho ni ngumu sana kufika.

  Inawezekana hujui kama unakwepa kufanya mambo fulani au hujui kwamba unayokwepa kufanya ndio ya muhimu kufikia malengo yako. Weka mipango yako vizuri na kujua ni mambo gani ukiyafanya yanakufikisha kwenye malengo yako. Katika hayo chagua yale ambayo ni ya muhimu zaidi na anza kuyafanya mara moja hata kama hupendi kuyafanya. Jilazimishe kuyafanya mpaka pale itakapokuwa kawaida kwako kuyafanya.

  Ili kupata msukumo wa kutosha wa wewe kufanya usiyopenda kufanya weka mategemeo makubwa kwenye mambo hayo. Ona kwamba kinachokuzuia kuyafikia mafanikio yako ni mambo hayo ambayo unakwepa kuyafanya, na kwa wewe kuweza kuyafanya itakurahisishia sana kupata mafanikio.