Ukweli ni kwamba wengi wa waliofanikiwa na walioleta mabadiliko duniani hawakufanya kazi. Kama na wewe unataka kupata mafanikio ama kufikia malengo yako na kuibadili dunia usifanye kazi. Kama usipofanya kazi utafanya nini? Sote tunajua kwamba kazi ndio msingi wa maendeleo na ni vigumu kufanikiwa bila kufanya kazi. Ndio, ni kweli kabisa, ila kuna kitu ambacho huenda hukielewi kuhusu kazi.
Waliofanikiwa na kubadili maisha yao na ya wenzao hawafanyi ama hawakufanya kazi, bali walifanya wanavyopenda kufanya. Walifurahia kufanya wanachofanya na mwishowe wakafanikiwa sana.
Pale unapofanya unachopenda kufanya kazi inakuwa sio kazi tena bali sehemu ya maisha yako. Wanaokuzunguka wataona unafanya kazi ila wewe binafsi hutoona ni kazi bali sehemu ya maisha. Je unaipenda na unafurahia kazi unayoifanya kwa sasa?
Kama hupendi unachokifanya ni vigumu sana kufanikiwa kupitia hicho unachofanya. Kama hupendi kazi unayoifanya kila siku kwako itakuwa ni malalamiko na kukwepa baadhi ya majukumu. Kwa kutopenda kazi unayoifanya ufanisi unakuwa mdogo sana, na hata ubunifu hauwezi kuwepo kabisa. Kama hupendi unachofanya unakuwa unahesbu sana muda wa kazi kuisha na mwisho wa wiki ndio furaha kubwa kwako. Kama unaona unafurahia sana masaa ya kazi yanapoisha na furaha yako inakuwa kubwa zaidi ijumaa inapofika, kuna uwezekano mkubwa sana wa kutopata mafanikio makubwa kwa unachofanya.
Kama unapenda unachofanya kila siku unakuwa na hamu ya kujifunza jambo jipya kuhusiana na unachofanya. Kila siku utakuwa mbunifu ili kurahisisha kazi unayoifanya. Na kupitia ubunifu ndio njia ya kufanikiwa na kuleta mabadiliko kwako na kwa wanaokuzunguka. Kama unapenda unachofanya unakuwa na msukumo ndani yako wa kutaka kufanya zaidi ya unachotegemewa kufanya, kujifunza zaidi na kutaka kubobea zaidi. Kama unapenda unachofanya unakuwa tayari kutumia muda wako wa ziada baada ya kazi kufanya mambo yanayohusiana na kazi yako.
Nini cha kufanya kama hupendi kazi unayoifanya?
Kama hupendi kazi unayoifanya kuna njia mbili za kukusidia ili uweze kupata mafanikio.
Njia ya kwanza ni kujilazimisha kuipenda kazi unayofanya. Kama huna njia nyingine zaidi ya kazi unayofanya huna budi kujilazimisha kuipenda. Na kujilazimisha haimaanishi ujichape viboko, bali kujipa sbabu kubwa ya wewe kupenda unachofanya. Angalia fursa unazoweza kuzipata kupitia unachfanya, angalia mafanikio makubwa unayoweza kupata kwa kufanya kazi hiyo kwa bidii. Na pia angalia waliofanikiwa kwa kufanya unachofanya na ufanye kama wao na kwa ubunifu zaidi ili na wewe ufanikiwe.
Njia ya pili ni kuacha kupoteza muda. Kama upo kwenye kazi ambayo huipendi na hakuna dalili zozote za wewe kuweza kujilazimisha kuipenda unapoteza muda. Badala ya kuendelea kupoteza muda wako, acha mara moja na uanze kufanya kile unachopenda kufanya. Usijidanganye unafanya tu hivyo kwa muda ila baadae utaondoka na kwenda kufanya kazi nyingine, utazeekea kwenye kazi hiyo hiyo. Kama huamini jaribu kumuuliza mtu aliefanya kazi unayoifanya kwa zaidi ya miaka ishirini na muulize alivyoanza alikuwa na mawazo gani na sasa ana mawazo gani.
Mafanikio yanakuja kwa kupenda unachofanya, iwe umeajiriwa, umejiajiri ama unfanya biashara. Watu wote waliofanikiwa sana walipenda sana kazi zao na hivyo kuwa sehemu ya maisha yao. Ipende kazi yako na haitakuwa kazi tena bali maisha ya kawaida. Kazi ikishakuwa sehemu ya maisha yako ufanisi na ubunifu unakuwa wa hali ya juu sana na hapo ndipo mafanikio yanapoanzia.