Nani ambae hapendi kufanikiwa? Nani ambae hapendi kupata kile anachokitaka kwa wakati anaotaka? Nani ambae hapendi kuwa tajiri? Kwa binadamu aliekamilika lazima atapenda kufanikiwa kwenye jambo fulani analofanya. Kama kila mtu anataka kufanikiwa kwa nini wengi hawajafanikiwa? Kwa nini ni wachache sana ndio wanafikia malengo waliyojiwekea?
Jibu ni kwamba sio rahisi. Sio rahisi kufanikiwa, sio rahisi kufikia malengo makubwa uliyoweka, ingekuwa rahisi kusingekuwa na haja ya kuyaandika na kusoma haya. Ni kazi ngumu, inayochukua muda mrefu na inayohitaji uvumilivu.
Nakuambia sio rahisi, sio kwa sababu nakutisha, hapana ila kwa kujua sio kazi rahisi inakusaidia kupunguza ugumu. Kwa kujua sio rahisi kufikia mafanikio yako inakuandaa wewe kuweza kukabiliana na changamoto utakazokutana nazo njiani.
Sio rahisi kupanga mipango na kuifuata kila siku bila ya kuchoka hata kama huoni majibu. Sio rahisi kuambiwa hapana ukaendelea, kuambiwa huwezi ukataka kuwaonesha inawezekana. Sio rahisi kuacha furaha ya karibu na kusubiri furaha kuu utayoipata kwa kutimiza malengo yako.
Sio rahisi hata kidogo ndio maana wengi wanashindwa kufika walikopanga kufika, ila sio wewe, wewe utafika kwa kuwa unajua sio rahisi kufika hivyo utajipanga sawasawa.
Tusikate tamaa, tuendelee na mapambano ili tuweze kufika kule tunakotaka kufika. Japokuwa sio rahisi inawezekana, hakuna kinachoshindikana