Una malengo na mipango mbalimbali kwenye maisha yako, je umeyaandika malengo hayo? Najua hujaandika, na sio wewe tu bali wengi wetu inatuwia vigumu sana kuandika malengo yetu(kama huna ama huelewi malengo yako soma;maisha ni zaidi ya kuwa na hela nyingi).
Wengi wetu hatufikii malengo na mipango yetu kwa sababu mbalimbali. Moja ya sababu hizo na ambayo ni sababu kuu ya kutofikia malengo ni kutoyaandika malengo yetu.
Unaweza kuona haina umuhimu mkubwa wa kuandika ila ni muhimu zaidi ya unavyofikiri. Wengi ambao hawaandiki malengo wanakuwa wameyaweka tu kwenye mawazo yao.
Kuandika malengo yako ni muhimu kwa sababu kutakusaidia yafuatayo;
Yanakuwa na maana kubwa. Kitu chochote tunachoandika kinakuwa na mana sana kwenye maisha yetu. Kama utaweka kwenye mawazo tu ni rahisi kusahau ama kutotilia maanani. Ila unapokaa chini na kuandika ni kama umeingia mkataba ambao itakubidi kuutekeleza.
Inakufanya ufikiri zaidi. Unapoandika malengo unafikiria zaidi njia za kuweza kuyafikia, totauti na pale unapokuwa nayo kichwani tu. Unapondika unakuwa umejihusisha zaidi na unachokiandika hivyo kuweza kuchambua na kujua vizuri ni nini unaandika.
Inakusaidia kuona na kufurahia mafanikio. Kama umeandika malengo na ukayafikia ni rahisi kujua umeyafikia kwa sababu uliandika ni nini hasa unachotaka. Ila kwa kufikiria tu ni vigumu kujua kama umeshafikia malengo ama umebakiza kiasi gani kufikia malengo yako.
Inakusaidia kutumia muda wako vizuri. Kama umepanga kufikia malengo fulani ndani ya muda fulani na ukaandika kila utakachofanya ndani ya muda huo inakusaidia sana kutumia muda wako vizuri. Kama hujaandika popote ni vigumu kujua kama uko kwenye mstari au nje ya mstari.
Kuwa na kijitabu ambacho unaweza kuandika malengo yako, unaweza kuwa na ‘diary’ ama ‘notebook’ ambavyo ni rahisi sana kupatikana na ni rahisi kutunza.
Kama hujawahi kuandika ama huoni kama kuna umuhimu wa kuandika anza sasa kuandika na utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.
Ni vigumu sana kuanza kuandika kama hujazoea kufanya hivyo ila andika kile kinachotoka ndani yako. Usiogope kama ukiandika na huna uhakika wa kufikia hayo, wewe andika malengo yako na mipango ya kuitekeleza kisha anza kutekeleza mipango hiyo.
Kitu chochote ambacho hakijaandikwa ni vigumu sana kutekelezeka ndio maana hata mashuleni, maofisini na kwenye miradi yoyote kila kitu kinakwenda kwa maandishi. Ripoti zinaandikwa, majukumu yanaandikwa, ratiba zinaandikwa na vingine vingi. Anza na wewe kuandika kila unachopanga kufanya na itakuwia rahisi kukipata.