Kila siku maisha yanaonekana kuwa magumu zaidi ya siku zilizopita. Fedha zinakuwa ngumu kupatikana, uhalifu unaongezeka, amani inatoweka na hata uelewano ndani ya familia unakuwa mgumu. Kila kitu kinaonekana kuwa kigumu na changamoto ni nyingi kila kunapokucha. Hata kuendesha mahusiano ya kimapenzi ama ya ndoa kumekuwa kugumu sana siku za hivi karibuni. Ndio maana mahusiano na ndoa nyingi zinavunjika sana sasa. Ufisadi nao umeshika kasi sana na kila mtu anaona kuiba ndio njia rahisi ya kupunguza machungu yake.

  Tumekuwa tukitafuta sababu mbalimbali za nini kinachofanya maisha kufika hapa. Tumekuwa tukiangalia mambo makubwa sana na kusahau kitu kidogo ambacho kila mtu angekifahamu na kukifanya maisha yangekuwa mazuri na rahisi kwa kila mtu.

  Maisha yangekuwa mazuri na rahisi sana kama wote tungejua tuko kwenye upande mmoja. Kama wote tungejua tuko kwenye upande mmoja ingepunguza sana migogoro baina ya watu na mamatizo mengi yaliyopo. Mara nyingi watu tunakuwa upande mmoja, ila tunatofautiana mitazamo ama njia za utekelezaji.

umoja

   Kama wanafamilia wangejua kwamba wako kwenye upande mmoja wa kuboresha maisha ya kila mtu, basi migogoro mingi isingekuwepo.

  Kama wananchi na viongozi wangejua wako kwenye upande mmoja wa kuendeleza taifa basi wizi na ufisadi usingekuwepo.

  Kama waajiri na waajiriwa wangejua wako kwenye upande mmoja wa kutaka kuimarisha mazingira ya kazi na uzalishaji basi matatizo mengi ya kwenye kazi yasingekuwepo.

  Kama wapenzi ama wanandoa wangejua wako kwenye upande mmoja wa kuimarisha mahusiano yao na maisha yao basi migogoro mingi inayosababisha mahusiano kuvunjika isingekuwepo.

  Pale tunaposhindwa kujua kwamba tupo kwenye upande mmoja ndipo ubinafsi unapoanzia na kila mtu kumwona mwenzake kama anafaidi sana. Na ubinafsi unapanza kila mtu huanza kuchukua hatua anazodhani zinamfaidisha yeye kumbe zinamuumiza yeye na aliye upande wa pili.

  Wote tuko kwenye upande mmoja kwa lolote tunalofanya, hivyo tuungane ili tuweze kufaidi sote kwa pamoja na tukafurahia maisha yetu. Kutofautina kimtizamo haimaanishi kuna uadui bali ni wakati mzuri wa kutafuta njia itakayowanufaisha wote.