Kuna siku unaweza kutoka asubuhi bila kusafisha kinywa na mwili wako? Ni vigumu sana mtu kuweza kuamka na kuenda tu kwenye shughuli zake bila ya kufanya usafi wa mwili wake. Kusafisha mwili ni kitu kikubwa ambacho kila mtu anakifanya anapoamka na kabla ya kutoka nyumbani.
Ni vizuri sana kufanya usafi wa mwili kila siku asubuhi, ila kuna kosa wengi wetu tunafanya kila asubuhi. Je umewahi kufanya ama una utaratibu wa kufanya usafi wa akili ama fikra zako kila siku asubuhi? Ama unafikiri haiwezekani kufanya usafi wa akili au unadhani hakuna umuhimu huo?
Ni muhimu sana kufanya usafi wa akili yako kila siku asubuhi unapoamka na kabla ya kufanya chochote. Unapolala unapumzisha akili, unapoamka akili inakuwa tayari kupokea kile unachokipata asubuhi.
Kama huna utaratibu wa kusafisha akili yako kila asubuhi utajikuta akili yako inapokea chochote kinachokujia. Kama utaanza kwa kufikiria matatizo ina maana siku nzima hutofikiria lolote la maana zaidi ya matatizo. Kama utaanza kwa kupata habari za umbea ama udaku itakuwia ngumu kuweza kufikiria malengo na mipango yako.
Unaposafisha akili yako asubuhi unaiweka tayari kwa ajili ya kuwa na mawazo chanya yenye kukufikisha kwenye malengo yako. Inakusaidia kuweza kuvivuka vikwazo mbalimbali unavyokutana navyo kila siku. Inakusidia kuweza kuendelea mbele hata pale unapoambiwa hapana haiwezekani.
Unasafishaje akili yako kila siku asubuhi?
Kuna njia mbalimbali unazoweza kuzitumia kusafisha akili yako kila siku asubuhi, baadhi ya njia hizo ni;
Kupitia malengo na mipango yako kila siku asubuhi. Kama unautaratibu wa kupitia malengo yako uliyoandika(kama hujandika soma hapa) kila siku asubuhi, unaianza siku yako ukijua umefikia wapi na ni nini kinahitajika kufanyika ili kufikia malengo yako.
Pia unaweza kuwa na utaratibu wa kujisomea kitabu ama chochote kinachohusiana na shughuli unazofanya ili kuongeza ufanisi wako na kujua mambo mengi zaidi.(soma; zoezi zuri la kufanya kila siku)
Njia nyingine nzuri ya kuianza siku yako kwa kusafisha akili yako ni kusikiliza vitabu vilivyosmwa(audio books). Hii ni njia rahisi ya kujifunza vitu vingi kwa muda unaokuwa unafanya mambo mengine. Kwa mfano unaweza kusikiliza vitabu hivyo ukiwa unjiandaa ama ukiwa njiani kuelekea kwenye shughuli zako. Vipo vitabu vilivyosmwa kwenye kila kada na kama unataka kupata vitabu hivyo bonyeza PATA AUDIO BOOKS
Pia unweza kuianza siku yako vizuri kwa kupitia blog hii ya AMKA MTANZANIA na kusoma makala mbalimbali zitakazo kusaidia katika harakati za kufikia malengo yako.
Kwa vyovyote vile hakikisha unaianza siku yako akili yako ikiwa safi na tayari kwa ajili ya kuendeleza harakati za kufikia malengo yako. Usikubali kuamka tu na kupokea chochote kinachokuja kwenye akili yako.