Ni mara ngapi umekuwa unafikiri ama unafanya jambo fulani halafu unapata mawazo mazuri sana? Hayo mawazo umewahi kuatekeleza? Kama huatekelezi yanaishia wapi?
Mara nyingi huwa tunapata mawazo mazuri sana ambayo kama tukiyatekeleza tunaweza kuyabadili maisha yetu kwa kiasi kikubwa. Mawazo haya tunayapata kwa njia zifuatazo,
- Kusoma ama kusikiliza vitabu mbalimbali.
- Kufuatilia habari na maisha ya kawaida
- Ushauri na uzoefu kutoka kwenye maisha ya kawaida.
- Kufikiria au unapokuwa umetulia.
- Wakati tunafuraha ama tumefanikiwa kukamilisha jambo
lililokuwa linatushinda.
Ni wachache sana na mara chache sana watu huweza kutekeleza mawazo ya aina hiyo. Na usichokijua ni kwamba wale wanaotekeleza mawazo ya aina hii ndio wanaoleta mabadiliko kwao na kwa dunia kiujumla.
Sababu pekee mpaka sasa hujafanya mabadiliko makubwa ni kwa kuwa hutekelezi mawazo hayo mazuri. Na sababu pekee ya kutotekeleza mawazo hayo ni kupotea kwa mawazo hayo.
Mawazo haya mazuri yanapotea kwa sababu hujui kama yanapotea hivyo inakuwia vigumu kuyatekeleza.
Sababu kuu ya mawazo hayo kupotea ni kutoyaandika mawazo hayo. Kitu chochote ambacho hakijaandikwa ni vigumu sana kutekelezeka.
Kuna faida kubwa sana ya kuandika kila wazo linalokujia kichwani kwako. Kwa kufanya hivi unakuwa na mawazo mengi na ukiyachanganya pamoja unaweza kutoka na wazo moja zuri sana ambalo linaweza kuyabadili maisha yako na yawanaokuzunguka.
Kama tulivyoona kwenye kuandika malengo(soma; ni muhimu kuandika malengo yako) kitu chochote kinachowekwa kwenye maandishi ni rahisi kutekelezwa kwa sababu kuandika kunatufanya tufikiri zaidi na kuweka mkataba fulani ambao inatubidi kuufikia.
Kuwa na mawazo mazuri na kukaa nayo kichwani ni rahisi sana kupotea hasa pale unapopata mawazo mengine mapya. Hii imeshakutokea mara nyingi sana na inamtokea kila mtu.
Anza utaratibu wa kuandika mawazo yako kila yanapokujia na kuyapitia mara kwa mara. Kwa kufanya hivyo itakuwia rahisi sana kuyafikiria zaidi na kuyaboresha mawazo yako.
Hakikisha kila ulipo unakuwa na kijitabu kidogo cha kuandika mawazo yanayokujia, inaweza kuwa notebook au diary.
Na diary ni nzuri sana kwa sababu ina tarehe hivyo ni rahisi kujua kila wazo na siku yake. Kama huna diary nunua japo ndogo(ambayo inauzwa kwa bei ndogo sana) n uanze kuitumia kuandika mawazo yako.
Pia unaweza kuwa na vikadi vidogo vidogo ambavyo unaandika mawazo yako na baadae kuvipanga na kupata wazo kamili.
Kama unatumia ‘smart phone’ kuna application nyingi unazoweza kutumia kutunza mawazo yako kwa kuandika ama kurekodi. Tafuta moja ya application hizo na uanze kutunza mawazo yako.
Usikubali mawazo yako yapotee tu kama mvuke ama moshi angani. Kaa nayo, yafikirie zaidi na baadae yakuletee mabadiliko kwenye maisha yako na ya wanaokuzunguka. Njia pekee ya kutunza mawazo yako ni kuyaandika.