Kila mtu anatamani kupata mafanikio kwenye maisha na wengi wetu tuna malengo na mipango mbalimbali kwenye maisha yetu. Ili tuweze kufikia malengo yetu kuna gharama ambazo lazima tulipe, hazikwepeki. Kujua gharama zinazotakiwa kulipwa ili kufikia mafanikio imekuwa ndio tofauti kuu kati wa waliofanikiwa na walioshindwa.

  Wote waliofanikiwa kufikia mlengo yao walijua kuna gharama za kulipa na wakajipanga kuzilipa gharama hizo. Kwa upande wa pili, walioshindwa ama wanaoteseka kuyafikia malengo yao hawajui kuna gharama za kulipa, ama wanajua ila wamepuuzia kuzilipa.

  hudhuria2

  Kama ulikuwa hujui kuna gharama za kulipa ama ulikuwa unapotezea kulipa gharama hizi ni vyema ukakaa chini na kutathmini vizuri safari yako ya mafanikio.

  Kuna gharama nyingi za kulipa ili ufikie malengo uliyojiwekea. Ila kuna gharama moja ambayo ndio inaweza kuwa kuu na ndio ambayo watu wengi inawashinda kulipa. Kutokujua gharama hii au umuhimu wa kuilipa kumefanya watu wengi wahangaike sana kuweza kufikia malengo yao.

  Gharama tunayozungumzia hapa ni kuhudhuria kila siku. Ni lazima kila siku uhudhurie kwenye malengo yako, mipango yako, maisha yako na kazi yako. Ni lazima kila siku uhudhurie. Kama hujaelewa namaanisha nini naposema uhudhurie, hebu tuangalie mifano michache ya mahudhurio.

  Kumbuka kipindi unasoma shule ilikubidi kila siku kuhudhuria ili uweze kufaulu, kila siku yaliitwa majina kujua nani kafika na nani hakufika.. Kama wewe ni mfanyakazi ama umewahi kuwa mfanyakazi utakuwa unaelewa vizuri sana kwamba ili ulipwe mshahara ni lazima kila siku uhudhurie kazini. Ili kusisitiza zaidi umuhimu wa mahudhurio makazini kumewekwa kitabu cha kujiandikisha kama umefika kazini. Hata kama hujisikii kuhudhuria inakubidi tu uhudhurie ili mwisho wa mwezi upokee mshahara. Hii inaonesha ni jinsi gani mahudhurio ndio kitu cha kwanza kwa wewe kufikia malengo yako.

hudhuria3

  Je wewe una utaratibu wa kuhudhuria kwenye malengo na mipango yako kila siku? Kila siku unafanya jambo ambalo litakusogeza kufikia malengo yako? Kila siku ni siku muhimu sana kwako kufanya mambo yanayokupeleka kwenye malengo yako(soma; leo ni siku muhimu kwako). Usiache hata siku moja kuhudhuria kwenye malengo yako.

  Kama ilivyo kwamba huwezi kufaulu bila kuhudhuria darasani, huwezi kulipwa mshahara bila kuhudhuria kazini ndivyo ilivyo kwenye mafanikio. Huwezi kufanikiwa bila kuhudhuria kwenye malengo na mipango yako kila siku.