Kila siku tunakutana na watu wengi sana ambao wamekata tamaa na maisha yao. Na wengine wengi wapo tu kusukuma maisha yaende. Sababu kuu ya watu kufikia hapa ni kukosa furaha maishani. Mpaka mtu anafikia hatua ya kujiua ama kuwa mlevi wa kupindukia sababu kuu ni kutoyafurahia maisha. Asilimia kubwa ya watu hawayafurahii maisha, kila siku wanakutana na matatizo tu na maisha yao hayana tena maana kwao. Waweza nawe ukawa mmoja wa watu waliokata tamaa na maisha yao, ila kwa kusoma hapa leo utakwenda kuyabadili maisha yako na utayafurahia sana.
Niliandika makala hapa ya kuelezea jinsi ambavyo furaha ya maisha yako unayo wewe mwenyewe(soma; hii ni haki yako ya kuzaliwa). Pamoja na kwamba furaha unajiletea mwenyewe, bado huwezi tu kujilazimisha kuwa na furaha. Lazima kuna vitu viwe katika maisha yako ili kweli uweze kuona maisha yako yana maana fulani. Na kuna kitu kimoja kikubwa ambacho ukishakuwa nacho maisha yako yatakuwa ya furaha kila siku.
Sababu kuu mpaka sasa huyafurahii maisha yako ni kutobobea kwenye jambo lolote ama kazi yoyote unayofanya. Kazi ni sehemu kubwa sana ya maisha yetu, na chanzo kikuu cha matatizo na msongo wa mawazo watu wanaopata vinaanzia kwenye kazi. Kama hakuna kitu chochote unachoweza kufanya kwa ubunifu mkubwa, na kutoa matokeo mazuri sana, maisha yako hayawezi kuwa ya furaha.
Unapobobea ama kuwa mtaalamu na mbunifu mkubwa kwenye kazi yoyote unayofanya ni lazima utayafurahia maisha kwa sababu kuu mbili.
Kwanza watu wanaokuzunguka watauona utofauti wako na watakusifu kwa jinsi unavyoweza kufanya makubwa, hii itakufanya uone jinsi ulivyo wa muhimu kwenye maisha yao. Kutokana na sifa unazopata zinakupa deni la kutotaka kuwaangusha na kwa njia hiyo utafanya zaidi. Kwa kufanya zaidi unazidi kutoa vitu vizuri na kuzidi kusifiwa. Kwa njia hii unakuwa na furaha sana unapofanya kazi kwani unajua matokeo yatakuwa mazuri na tofauti na yatawafurahisha wengi.
Pili, kwa wewe kubobea na kufanya kwa ubunifu zaidi kutafanya utoe matokeo mazuri sana na hivyo kuongeza thamani ya kazi zako. Kwa kuongeza thamani moja kwa moja unajikuta unalipwa zaidi na hii itakuletea furaha kubwa ya kazi na maisha kwa ujumla.(soma; kama unataka kulipwa zaidi)
Unawezaje kubobea kwa unachofanya ili na wewe ufurahie maisha yako?
Ninaposema kubobea haimaanishi uende shule ukasome labda uchukue shahada ya uzamili na uzamivu, hapana. Kwa kubobea namaanisha utumie uwezo, vipaji na ubunifu wako katika kazi unazofanya. Kila mtu ana uwezo, vipaji na ubunifu wa hali ya juu na tofauti kabisa na watu wengine. Kwa kuweza kuvijua vitu hivi ndani yako na kuvitumia kwenye kazi zako utatoa majibu mazuri sana ambayo yatamfurahisha kila mtu.(soma; kamwe usijishushe na kujiona wa chini)
Tumia uwezo, vipaji na ubunifu ulionao katika jambo lolote unalofanya na utatoa majibu mazuri sana yatakayowafurahisha wanaokuzunguka. Kwa kazi zako kuwafurahisha wengine, kunakupa umuhimu na kunakufanya ufurahie kufanya kazi na uyafurahie maisha. Kumbuka wote waliofanikiwa hawakufanya kazi bali walifanya yale wanayofurahia kufanya(soma; kama unataka kufanikiwa usifanye kazi)
Japo maisha ni magumu lakini tunakila sababu ya kuyafurahia, na ukiamua kuyafurahia maisha yako hakuna anayeweza kukuzuia. Anza sasa kwa kuongeza thamani kwenye kazi zako na baada ya muda utaanza kuona matunda ya wewe kutumia vipaji, uwezo na ubunifu wa kipekee ulionao(kumbuka kila mtu anavyo, hivyo usijione labda wewe huna).