Mpenzi msomaji wa blog hii ya AMKA MTANZANIA napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwako kwa kuendelea kusoma na kufurahia makala mbalimbali katika blog hii.
Lengo kuu la blog hii ni kuhamasisha watanzania kuweza kutambua na kutumia uwezo wa kipekee walionao katika kuyajenga maisha yao na kufikia malengo waliyojiwekea. Pia kupitia blog hii tunashirikishana fursa mbalimbali zinazopatikana Tanzania na jinsi tunavyoweza kuzitumia kupata mafanikio.
Nimekuwa nikipata email kutoka kwenu wasomaji mkieleza jinsi makala zilizopo kwenye blog hii zinavyowasaidia. Pia kupitia blog hii nimeweza kujuana na kukutana na watu wengi ambao mpaka sasa tumekuwa tunashirikiana kwa mambo mengi.
Ni faraja kubwa pale unapofanya jambo halafu ukapata mrejesho kutoka kwa watu. Inakupa nguvu ya kusonga mbele na kuvuka vikwazo mbalimbali kwa kujua kuna watu wanafuatilia kinachoendelea.
Hakuna kazi ngumu kama kuandika.
Makala zote zinazowekwa kwenye blog hii zimeandikwa kutokana na matatizo mbalimbali tunayoyapitia watanzania. Hakuna makala hata moja ambayo imenakiliwa ama kutafsiriwa kutoka kwenye chanzo kingine kile. Ni furaha kuiona makala ikienda hewani na kusomwa na watu ila ni kazi ngumu sana kuandaa makala mpaka kufikia kuwekwa mtandaoni. Ni kazi unayohitaji utafiti, kufikiri na kusoma vitu mbalimbali.
Mara nyingi nimekuwa nikipata makala kutokana na mawasiliano ninayokuwa nayo na baadhi ya wasomaji wanaonitumia barua pepe.
Kutokana na idadi ya wasomaji wa blog hii kuongezeka kila siku, kazi ya kuandika ndiyo inazidi kuwa ngumu zaidi. Lakini ugumu huu ndio ninaufurahia kwa maana ndio unafanya nifikiri zaidi na kupata majibu bora zaidi.
Ombi kuu kwako msomaji wa blog hii.
Nina maombi matatu kwako msomaji wa blog hii ya AMKA MTANZANIA
1. Washirikishe marafiki zako wa kwenye mitandao ya kijamii makala mbalimbali unazozisoma kwenye blog hii. Kila mwisho wa makala kuna vitufe vya facebook, twitter na google+. Tafadhali bonyeza vitufe hivyo kuwajulisha marafiki zako mambo mazuri yanayopatikana kwenye blog hii
2. Kama una wazo lolote ambalo unafikiri linaweza kuwasaidia watanzania wenzetu tafadhali usisite kuwasiliana nami ili tuweze kuwashirikisha wenzetu. Kama unaweza kuandika makala fanya hivyo kisha tutaiweka kwenye blog. Kama huwezi kuandika wasiliana nami na unipe wazo hilo na kisha nitaandaa makala nzuri na wewe utahusika kama mchangiaji mkuu. Pia tuendelee kuwasiliana kwa jambo lolote linalohusiana na yanayoandikwa kwenye blog hii.
3. Tafadhali sana unaponakili makala ama sehemu ya makala kwenye blog hii na kuiweka sehemu nyingine kwenye mtandao, weka link kuonesha kwamba umeitoa wapi. Kwa kuweka link unakuwa umenitendea haki kwa kazi ngumu niliyoifanya ya kuandika makala hiyo. Mwanzo kulikuwa na wimbi kubwa sana la watu kukopi makala na kuweka kwenye blog zao. Ilinibidi nifunge mtu asiweze kukopi hovyo ila kwa sasa nitafungulia na yeyote anaetaka kunakili anakili tu, ila uwe tu mtu wa shukrani kwa kuweka link ya blog.
Tuendelee kushirikiana na kusaidiana ili kuweza kuamka na kuwaamsha watanzania wenzetu na tuweze kutumia uwezo wetu binafsi kuyajenga maisha yetu na kufikia malengo yetu.
Nashukuru sana kwa ushirikiano wako.
Makirita Amani, mwendeshaji mkuu wa AMKA MTANZANIA.
Mawasiliano
Email; amakirita @gmail.com
Simu; 0717396253