Sote tunajua ni jinsi gani uchaguzi ulivyo na adhari kubwa kwenye maisha yetu. Iwe unajihusisha na siasa au la uchaguzi una nafasi kubwa sana kwenye maisha yako.

  Ninaposema uchaguzi mkuu muhimu huenda umeshafikiria mwaka 2015. Ni kweli uchaguzi huo ni muhimu sana kwetu na kwa nchi yetu ila sio muhimu zaidi ya uchaguzi nitakaokuambia hapa. Kuna uchaguzi muhimu sana kwenye maisha yako ambao kuna uwezekano mkubwa bado hujaufanya. Na kama bado hujafanya uchaguzi huu muhimu hata ukasubiri kwa kiasi gani 2015, itakuja itapita na maisha yako bado yataendelea kuwa yalivyo.

uchaguzi

  Unapofanya uchaguzi wa serikali unachagua ni nani atakayeyaadhiri maisha yako kwa kipindi chote atakachokuwa madarakani. Ndio maana tunasisitiziwa kuwa makini sana wakati wa uchaguzi maana kosa dogo linaweza kukupatia kiongozi mbovu sana na mambo yakazidi kuwa magumu.

  Tatizo kubwa wakati wa chaguzi hizi kuna wengi wanaongea na kuahidi mengi na wengine wanahonga ili wapate nafasi wanazotaka. Wanapozipata sote tunajua ni nini kinatokea, hakuna kubwa linalobadilika na wakati mwingine mambo yanakuwa mabaya zaidi. Kwa kuangushwa huku tunahamishia matumaini yetu kwenye uchaguzi unaofuata kwamba “tutawakomesha kwenye uchaguzi ujao”

  Kuangushwa huku na malalamiko tunayokuwa nayo kunatokana na kutofanya uchaguzi muhimu kwenye maisha yako.

  Uchaguzi upi ni muhimu kwa maisha yako?

  Leo au siku yoyote ya karibuni tenga muda na ufanye uchaguzi mkuu kwenye maisha yako. Katika uchaguzi huo mkuu mpigie kura mtu ambae atakuwa kiongozi mkuu wa maisha yako, mtu ambae hatima ya maisha yako unaiweka kwenye mikono yake. Mtu huyo ndio mwenye uwezo wa kuyajenga ama kuyabomoa maisha yako. Mtu huyo anaweza kukuangusha ila una kila sababu ya kumlaumu kama atafanya hivyo. Mtu huyo ni WEWE.

  Wewe ndio kiongozi mkuu wa maisha yako, wewe ndiye unayeweza kuyabadili maisha yako na wewe ndio dereva wa safari ya maisha yako. Unajua ni wapi unapotaka kwenda na ni njia gani itakufikisha unakokwenda. Kama utashindwa kufika basi wewe ndio wa kwanza kulaumiwa.(soma; usimlaumu yeyote anza kujilaumu wewe)

  Usiweke hatima ya maisha yako kwa mtu mwingine yeyote. Hakuna yeyote anayeweza kukutoa hapo ulipo kama wewe mwenyewe hujajitambua na kujua ni kipi unachotaka na utakipataje. Wewe unao uwezo mkubwa sana wa kuyajenga ama kuyabomoa maisha yako. Na wewe ni wa pekee hapa duniani, una vipaji na uwezo tofauti kabisa na binadamu wengine(soma; wewe ni wa pekee).

  Fanya uchaguzi wa kujichagua wewe kuwa kiongozi na muendeshaji mkuu wa maisha yako. Kama umepania uchaguzi wa 2015 na ikafika na ukafanya uchaguzi huo bado maisha yako hayatobadilika kwa kiasi kikubwa kama hujafanya uchaguzi wa kujichagua wewe. Ukishajichagua wewe mwenyewe ni rahisi kwako kuweza kumchagua kiongozi anayefaa. Kama unashindwa kujichagua mwenyewe, kwa kujitambua, ni rahisi sana kulaghaiwa na kuchagua watu wabovu.