Sasa hivi tatizo sio kusoma bali tatizo kubwa ni kupata ajira. Na tatizo hili linakuzwa na mfumo wetu wa elimu ambao unaandaa waajiriwa.(soma; mfumo mbovu wa elimu na tatizo la ajira tanzania)

  Kutokana na tatizo la msingi kuwa upatikanaji wa ajira uchaguzi wa kozi za kusoma umekuwa mgumu sana. Kwa sababu kozi karibu zote zimeshakuwa na wahitimu wengi hivyo nafasi za ajira zinazidi kuwa finyu.

  Swali la kozi gani mtu asome ili asisumbuke kupata ajira ni swali linaloulizwa sana sasa hivi. Pia ni swali gumu sana kujibu kutokana na hali halisi ya wingi wa vyuo na wahitimu na ufinyu wa nafasi za ajira.

 chuo2

  Kama bado hujafikia kuchagua kozi ya kusoma, au kama ndio uko chuoni unasoma ama umemaliza kusoma ila bado ajira hujapata soma hapa na unaweza kupata baadhi ya vitu vitakavyokusaidia kutokana na swali hilo.

  Kwanza tuanze na ukweli mchungu, miaka mitano ijayo kila kada itakuwa na tatizo la ajira kama hakuna juhudi za makusudi zitakazofanyika karibuni kuzuia hilo.

  Kwa sasa inaonekana kozi za sayansi hasa uinjinia, udaktari na ualimu hazina tatizo kubwa la ajira. Na upungufu mkubwa tulionao wa wataalamu hawa unawafanya watu waamini kwamba nafasi hizi haziwezi kujaa haraka. Inaweza kuwa kweli, ila kuna vitu viwili vya msingi vya kuangalia hapa, kwanza vyuo vinaongezeka na udahili unaongezeka kila mwaka na pili uwezo wa serikali na taasisi nyingine kuajiri unapungua kila mwaka. Hivyo ndani ya miaka mitano ijayo, wahitimu watakuwa wengi na nafasi za ajira zitakuwa finyu mno.

  Kwa maana hiyo basi hakuna kozi yenye uafadhali hasa unapoangalia mbali. Je unaweza kumshauri vipi mtu anayekwenda kusoma?

  Kwa upande wangu kuna mambo matano nayoweza kusema kutokana na swala hili;

  Ushauri wa kwanza ninaoweza kuutoa ni mtu kujua kwamba mfumo wa elimu ni mbovu. Ndio unasoma kwenye mfumo mbovu ambao unakuandaa kuajiriwa na wakati huo huo nafasi za kuajiriwa ni chache. Hivyo wakati bado uko chuoni elewa mtaani hakuna kazi na uanze kujipanga mapema.

  Pili jua kabisa kwamba kuna tatizo la ajira na tatizo hili lipo kwenye kada zote. Kujua hivyo kutakufanya ufikirie kozi ya kusoma bila ya kuegemea upande wowote. Na pia kutakufanya usidharau kile unachosoma na kuona vingine ndio vya maana.

  Tatu soma kile unachopenda kusoma, ama kwa lugha nyingine kile unachofurahia kusoma. Kwa sababu kwa kusoma kitu unachokipenda unakuwa na ubunifu mkubwa na unaweza kutumia unavyojifunza kujiajiri mwenyewe. Ila kama unasoma kitu usichokipenda unakuwa kama unasukumwa hivyo hata kutumia ubunifu wako inakuwa vigumu. Kwa mfano kuna watu wamesoma kozi za TEHAMA(ICT) na kutokana na kupenda kozi hizo wamekuwa watundu na mwishowe wamefungua kampuni zao za kutoa huduma hizo za TEHAMA.

  Nne jua kabisa watu wengi sasa hivi hawaajiriwi kutokana na kozi walizosoma bali kwa kuangalia uwezo wao. Tofauti na mfumo wa kusaili wanaoomba ajira wa zamani siku hizi kuna kampuni zinafanya kazi hiyo maalumu ya kusaili. Moja ya vitu vikubwa wanavyoangalia kwenye usaili ni uwezo wa mtu kupambana na changamoto za kila siku. Hivyo wakati unasoma ama kama umeshamaliza ongeza uwezo wako na onesha uwezo wako popote unapopewa nafasi ya kufanya hivyo.

  Tano, jua kwamba kitakachokutoa maisha haya sio ulichosomea wala unachofanyia kazi bali uwezo wako na juhudi zako binafsi. Popote unapoweka juhudi na kutumia vipaji na uwezo wa pekee ulionao lazima utafanikiwa.

  Tatizo la ajira ni kubwa hivyo badala ya kuliogopa tatizo hilo ni vyema ukajipanga jinsi ya kukabiliana nalo. Kujua njia mbali mbali za kukabiliana na tatizo hilo soma; kabla hujaanza kuzunguka na bahasha soma hapa.