Maisha yetu yanaathiriwa kwa kiasi kikubwa na jamii inayotuzunguka. Kuna mambo mengi sana yanayofanyika kwenye jamii ambayo yanawaharibu na kuwakatisha tamaa watu wengi sana.

  Ukimchukua mbuzi, kuku, samaki, nyoka na tembo kisha ukawapa shindano la kupanda juu ya mti ni mnyama yupi kati ya hao ataweza zoezi hilo? Na je atakaeshindwa kupanda juu ya mti ndio hana uwezo kabisa?

sio sawa

  Kuna vitu vingi kwenye jamii vinatulinganisha kama vile tuko sawa. Moja ya vitu hivyo ni mfumo wa elimu. Na katika vitu vyote mfumo wa elimu ndio hatari sana kwa sababu ushindani wake unawaharibu watu wengi sana.

  Kwenye mfumo wa elimu(hasa elimu yetu) wanafunzi wote wanapimwa kwa kipimo kimoja cha mitihani ya masomo. Anaepata alama nyingi anaambiwa amefaulu na anaepata alama chache anaambiwa amefeli.

  Hakuna neno baya na linalowaharibu watu wengi kama wanapoambiwa WAMEFELI. Kuambiwa umefeli kunakuondolea ujasiri na kujiona kwamba wewe huwezi, wanaoweza ni wale waliofaulu. Kwa kutumia msamiati huu wa kufeli tumeua vipaji vingi sana.

  Kama kuna yeyote aliyewahi kukuambia umefeli amekudanganya. Hujawahi kufeli, bali aliekuambia umefeli yeye ndio amefeli?

  Kwa nini hujawahi kufeli?

1. Dunia ina watu zaidi ya bilioni saba, na katika watu wote hawa hakuna watu wawili wanaofanana kwa kila kitu. Hata watoto mapacha bado hawafanani kwa kila kitu. Hivyo wewe ni wa pekee katika dunia hii na hakuna unaeweza kulinganishwa nae.(soma; wewe ni wa pekee)

PEKEE

2. Una uwezo mkubwa sana ambao hauwezi kupimwa kwa kutumia masomo ya darasani. Kila mtu anauwezo binafsi ambao akiweza kuutumia anaweza kuyabadili maisha yake. Uwezo huu binafsi haufundishwi shuleni na pia hauwezi kupimwa kwa mtihani.

3. Una vipaji na ubunifu mkubwa sana ambao hakuna mwenye navyo. Kila mtu ana vipaji tofauti, ila mfumo wa elimu unatupima katika mambo machache sana ambayo kwa wengi wetu sio vipaji vyao. Kila mtu ana ubunifu wa kipekee ambao ni vigumu sana kuupima kwa masomo na mitihani ya darasani.(soma; kila mtu ni mbunifu)

  Sahau yote uliyowahi kuambiwa kwamba umefeli, hujawahi kufeli, labda uamue wewe mwenyewe kutotumia uwezo wako binafsi ulio nao ndio utakuwa umefeli.

  Jitambue na ujue uwezo mkubwa ulionao na vipaji vya kipekee ulivyonavyo. Vitumie vitu hivyo kuyajenga upya maisha yako ili uweze kuyafikia malengo yako na kupata mafanikio.

  Hakuna kinachoshindikana kama utaweza kutumia uwezo mkubwa ulionao. Usikubali kurudishwa nyuma na kukatishwa tamaa na jamii ambayo haijui uwezo ulio ndani yako.