Tarehe 31/12/2012 kupitia ukurasa wangu wa facebook niliweka habari ya kuhamasisha watu kujisomea vitabu. Na nikasema yeyote anaetaka vitabu vya kujisomea anipe email yake kisha nimtumie vitabu. Nilikuwa natuma vitabu vitatu ambavyo ni Rich Dad Poor Dad, Think and Grow Rich na The Richest Man in Babylon. Nilitumiwa email zaidi ya mia mbili na wote niliwatumia vitabu hivyo.

kujisomea

  Miezi mitatu baadae, tarehe 31/03/2013 niliweka habari hiyo hiyo kwenye forum moja kubwa hapa Tanzania. Huko nilikutana na upinzani mkubwa sana ambao sikuwahi kuufikiria. Kuna watu walipinga sana mpango huo na kudai kwamba vinaweza kutumika kwa mazingira ya ulaya tu na kwa Tanzania ni vigumu sana kuweza kuyabadili maisha yako kwa kusoma vitabu hivyo.

  Upinzani huu na hoja hizo vilinifanya nikae chini na kufikiri kama ni kweli hatuwezi kuiga usomaji vitabu wa wenzetu wazungu na hatimaye tukayabadili maisha yetu. Na pia ilinifanya nifikiri ni kwa jinsi gani hatuwezi kuwaiga wazungu kimaendeleo kwa kusoma vitabu hivyo vitatu ambavyo vimewasaidia watu wengi sana duniani.

  Katika kufikiri hivyo nilijikuta nahesabu ni vitu vingapi vya wazungu tumeiga, na majibu yalinishangaza. Asilimia tisini ya maisha yetu ya sasa tumewaiga wazungu. Tunaweza kusema karibu kila kitu tunachofanya sasa tumeiga kutoka kwa wazungu. Kwa mfano uvaaji wa mavazi, filamu tunazopendelea, miziki tunayopendelea, dini tunazosali, magari tunayoendesha, nyumba tunazoishi na mengine mengi ambayo nikiorodhesha hapa hapatowezi kutosha.

  Mtu anaweza kuvaa suti nyeusi na tai kwenye jua na joto kali la dar es salaam(nyuzijoto 30) wakati kwa asili vazi hili lilibuniwa kuvaliwa kwenye nchi zenye baridi. Lakini ukimwambia aige maendeleo ya wazungu anakwambia haiwezekani kwa sababu mazingira yao na ya kwetu ni tofauti. Hebu jiulize kuna mazingira tofauti zaidi ya hayo ya kuvaa suti? Mbona kwa suti(na mengine mengi) inawezekana?

  Je ni kweli tunaweza kuiga kila kitu cha wazungu isipokuwa maendeleo?

  Njia rahisi na halali ya kuiba ujuzi wa mtu ni kusoma vitabu. Usomaji wa vitabu ni muhimu kwa kila mtu na una manufaa makubwa sana.

  Kwa kujisomea vitabu unaongeza maarifa, unabadili mtizamo wako kuhusu maisha na unaongeza uwezo wa kufikiri na kukabiliana na changamoto mbalimbali tunazokutana nazo kila siku.

  Kama bado hujaanza utaratibu wa kujisomea vitabu jiunge na mtandao wa kutumiwa vitabu kwa kuandika email yako. Bonyeza maandishi haya ujiunge na mtandao huo.

  Kama hukupata vitabu vitatu nilivyotoa mwanzo andika email kwenda amakirita@gmail.com, subject iwe NAHITAJI VITABU VITATU.

  Washirikishe wenzako kwa kushare facebook na mitandao mingine ili nao wapate ujumbe huu.