Siku moja nilipata ujumbe kutoka kwa msomaji mzuri wa blog hii AMKA MTANZANIA. Ujumbe wenyewe unasomeka hivi

“namaanisha unawezaje kumsaidia mtu kupata kitabu anachokitaka for free,unanufaikaje na huduma hiyo mkuu.na kama kweli unafanya hivyo,hata mimi nauhitaji huo msaada mkuu!”

  Kwa kifupi msomaji huyu alitaka kujua nanufaika vipi kwa kuwatumia watu vitabu vya kujisomea bure.

  Nilimjibu kwa kifupi ila nimeona leo niandae makala kwa sababu kuna siri kubwa niliyojifunza na ambayo watu wengi hawaijui na kutokuijua kunapelekea maisha yao kuwa magumu sana.

  Kama unafanya unachofanya(kazi, biashara, ama huduma yoyote) ili upate hela, hutozipata na maisha yako yatakuwa magumu sana.

pesa

  Katika makala hii nitatumia mifano minne, na makala hii itakuwa ndefu kidogo hivyo jipe muda wa kuisoma mpaka mwisho ili upate mtizamo tofauti juu ya fedha.

  Watu wote walioleta mabadiliko duniani na hata waliofanikiwa sana hawakuweka fedha kama lengo lao kuu. Lengo lao kubwa lilikuwa kuleta mabadiliko ama kusaidia watu wanaowazunguka.

  Hebu tuangalie mifano michache ya watu walioleta mabadiliko na jinsi ambavyo hawakuweka fedha kama lengo lao kuu.

 1. WRIGHT BROTHERS na urushaji wa ndege ya kwanza.

   Katika harakati za kurusha ndege ya kwanza angani kulikuwa na makundi mawili yaliyopania kufanya hivyo. Kwa upande mmoja kulikuwa na WRIGHT BROTHERS na upande wa pili SAMUEL LANGLEY. Samuel langely alikuwa na kila kitu kilichohotajika kwa ajili ya kupaisha ndege. Alikuwa na hela za kutosha, aliajiri mainjinia na tayari alikuwa na soko la kuuza ndege kama angefanikiwa kuirusha. Alitaka kurusha ndege ili kupata pesa nyingi kwa kuwa tayari alikuwa na soko.

  Kwa upande wa pili WRIGHT BROTHERS hawakuwa na chochote kilichoonekana kinahitajika ili kurusha ndege. Hawakuwa na elimu kubwa(walikuwa mafundi baiskeli), hawakuwa na fedha, ila walikuwa na shauku kubwa ya kutaka kubadilisha hali ya usafiri kwa kuweza kurusha ndege.

  Pamoja na kwamba WRIGHT BROTHERS walichekwa sana ila wao ndio waliokuwa wa kwanza kurusha ndege.

 

2. ALEXANDER BELL na uvumbuzi wa simu.

  Alexander bell ndiye binadamu wa kwanza kugundua njia ya kusafirisha sauti kwenye nyaya na hatimaye kuweza kutengeneza simu. Mama yake na mke wake Alexender walikuwa viziwi. Alexander alitumia muda mwingi kutafuta njia ya kuweza kuwasaidia viziwi kuwasiliana na watu wengine. Ni katika harakati hizo ndipo alipogundua njia ya kusafirisha sauti kwenye nyaya. Japokuwa kulikuwa na bwana mwingine aliyekuwa anafanya ugunduzi wa simu lakini nia ya Alexander ya kusaidia na kubadili maisha ya watu ilimfanya kugundua simu mapema zaidi.

 

3. MARK ZUCKERBERG na uanzilishi wa Facebook.

  Mwanzilishi wa facebook, MARK ZUCKERBERG mara nyingi amenukuliwa akisema hakujua kama facebook ingekuja kuwa biashara kubwa yenye thamani ya mabilioni ya dola. Anasema yeye alianzisha facebook kubadili jinsi watu wanavyowasiliana. Alitaka kurahisisha mawasiliano kwa kutumia teknolojia ya kompyuta na mtandao aliyokuwa amejifunza. Nia yake hiyo imefanya facebook iendelee kuwa biashara kubwa duniani.

 

  Kupitia mifano hiyo michache unaweza kuona ni jinsi gani wagunduzi wakubwa hawakuweka fedha kama lengo lao kuu.

  Unapoweka fedha kama lengo kuu la wewe kufanya unachofanya ni vigumu sana kuweza kutumia uwezo wako mkubwa ulioko nao. Inakuwa vigumu sana kwako kutumia ubunifu na vipaji vikubwa vilivyoko ndani yako. Kwa kuwa lengo lako kuu ni kupata fedha hivyo utafanya yale yanayokuingizia fedha tu.

ubunifu2

  Na kama tunavyojua kuwa fedha huwa haitoshi, kwa kuweka fedha kuwa lengo kuu kwako kila siku utayaona maisha ni magumu sana kwako. Kwa sababu hazitakutosha na kila siku utakuwa unafikiria hela tuu.

  Ukiangalia watu wengi wanaofanya kazi za kuajiriwa, fedha huwa tatizo sana kwao. Wengi mishahara huwa haikutani na kila siku hulalamika maisha ni magumu na mishahara haitoshi. Yote haya chanzo kikuu ni kwa kuwa wanachokiona kwenye ajira zao ni hela tu. Wanachofikiria ni mwisho wa mwezi wachukue chao. Wengi hawaangalii kutoa huduma ama kuleta mabadiliko kwenye maisha yao na ya wanaowazunguka. Hii inafanya maisha yao kuwa magumu sana.

  Kama una mtizamo huu wa kuangalia fedha sana zaidi ya huduma unayotoa ni vyema ukaubadilisha kama unataka uyafurahie maisha. Fikiria kutoa huduma bora, fikiria kuleta mabadiliko na fikiria kuyagusa maisha ya watu na kuyabadili. Kwa kufanya hivyo utaanza kuyafurahia maisha na fedha zitakuja zenyewe bila ya wewe kuumiza kichwa.

 

  Mfano wa nne nitakaoutumia kwenye makala hii ni mimi MAKIRITA AMANI na blog hii ya AMKA MTANZANIA.

  Nimewahi kuwa na blog kadhaa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita. Lengo kuu la kuanzisha blog hizo ilikuwa kupata fedha. Nilijua kuwa na blog yenye watembeleaji wengi ni rahisi kupata matangazo na baadae kupata fedha. Nilihangaika sana kutafuta habari za kuweka ili kuwavutia watu lakini kwa mwaka mzima sikupata hata shilingi kumi. Baada ya kujifunza siri hiyo kubwa niliyoeleza hapo juu nilibadili mtazamo na kuamua kufanya kitu kitakachonibadili mimi na yeyote atakaesoma blog hii. Ndani ya miezi sita ya blog AMKA MTANZANIA nimejuana na watu wengi na nimeanza kupata fedha japo kidogo kupitia blog hii. Lengo kuu la blog hii sio kupata fedha bali kubadili maisha ya watu, na kwa kufanya hivyo fedha zimekuwa zikijitokeza zenyewe bila hata ya kutumia nguvu nyingi.

 

  Badili mtizamo wako juu ya unachofanya na fedha. Ukiweka fedha mbele kila siku utasumbuka kuzipata. Na hata kama utazipata bado hutakuwa na furaha kama pale unapofanya jambo la kuwasaidia wengine na wewe kuwa unafurahia kufanya jambo hilo.