Hakuna siku moja utakayoamka asubuhi na kusema leo ndio nimefikia mafanikio yangu. Mafanikio hayatokei kwa siku moja bali kwa siku nyingi zenye mafanikio kidogo kidogo. Kuweza kupanga na kutimiza malengo unayojiwekea kwa siku ni njia rahisi ya kufikia malengo yako maishani na kufanikiwa. Hivyo jinsi unavyoishi siku yako ndivyo unavyoyatengeneza ama kuyabomoa mafanikio yako.

kujihamasisha  

  Ili uweze kufikia malengo yako na kufanikiwa kwenye maisha ni muhimu sana kuishi kila siku kwa mafanikio. Ni muhimu sana kuipanga kila siku na kutekeleza mipango hiyo ya siku. Ni muhimu kuwa na furaha kila siku ili maisha yako yawe ya furaha.

  Inawezekana huwa unapanga siku yako vizuri sana lakini kutekeleza mipango yako kunakuwa kugumu sana. Kuna kitu kimoja cha muhimu sana kufanya kila sikuu na kila mara ili uweze kuishi siku yako kwa mafanikio na furaha na hatimaye kuweza kufikia malengo yako maishani.

  Kitu hicho unachotakiwa kufanya kila siku ni KUJIHAMASISHA(self motivation). Ni muhimu sana kujihamasisha kila siku. Tena ni muhimu zaidi kujihamasisha wakati wa asubuhi kabla hujaianza siku.(soma; hili ndilo kosa unalofanya kila siku asubuhi)

 

 Kwa nini ni muhimu sana kujihamasisha?

  Kujihamasisha ni muhimu sana ili kuianza na kuimaliza siku ukiwa na mtizamo chanya juu yako na malengo yako. Dunia ina ukatishaji tamaa mkubwa sana. Unaweza kuwa na malengo yako mazuri lakini kila unapojaribu kuyatekeleza kila anayekuzunguka anakukatisha tamaa au hakuna anayekupa moyo kwamba unaweza kufanya ulichopanga kufanya. Kila mtu anaweza kukubeza na mwishowe ukawaona wako sahihi na ukaamua kuachana na mipango yako. Hali kama hii imeshawatokea wengi hata wewe kuna vitu vingi umewahi kupanga kufanya ila kutokana na ukatishaji tamaa wa jamii inayokuzunguka ulishindwa kufikia malengo.

  Kwa kujihamasisha kila siku ni rahisi kuweza kushinda ukatishaji tamaa unaofanywa na jamii inayokuzunguka. Kwa kujihamasisha unafanya ukiwa na ari ya juu na matumaini makubwa ya kupata majibu mazuri.

  Unawezaje kujihamasisha kila siku?

  Kuna njia nyingi sana za kuweza kujihamasisha kila siku. Hapa nitazungumzia njia nne ambazo ukiweza kuzifanya kila siku asubuhi siku yako itakuwa ya mafanikio na furaha kubwa.

1. Kujipa muda wa kuyafikiria maisha yako. Mara nyingi huwa tunajidhulumu wenyewe. Uko tayari kumpa kila anayekuzunguka muda ila hujawahi kujipa muda wewe mwenyewe. Kila siku asubuhi chukua muda mchache kufikiria kuhusu wewe tu. Weka kila mtu na kila tatizo pembeni, fikiria maisha yako na malengo yako tu. Kisha pitia mipango yako ya muda mrefu na muda mfupi kisha ianze siku kwa kutekeleza mipango ya siku.

2. Kujisomea vitabu vinavyohamasisha. Kuna vitabu vingi sana vinavyohamasisha na kutia nguvu kuhusiana na mafanikio katika maisha. Ni muhimu sana kutenga japo nusu saa kila asubuhi na kusoma sehemu kidogo ya kitabu kinachohamasisha. Nimekuwa nikiwatumia watu vitabu vya kuhamasisha bure.Na wakati huu nitatuma kitabu cha Njia 100 za kujihamasisha. Kitabu hiki kitatumwa kwa wanachama wa mtandao huu, kama unataka kukipata na bado hujawa mwanachama bonyeza maandishi haya na ujiunge kwa kuweka email yako.

3. Kusikiliza vitabu vilivyosomwa(audio books). Ni muhimu sana kusikiliza vitabu vya kuhamasisha vilivyosomwa hasa pale unapokuwa upo kwenye jambo linalokulazimisha kupoteza muda. Kwa mfano upo kwenye safari ndefu ama upo kwenye foleni. Kwa kusikiliza vitabu hivi unajikuta unajifunza mengi sana na kuhamasika badala ya kupoteza tu muda. Kama huna vitabu vilivyosomwa unaweza kuvipata kwa kubonyeza maandishi haya(kupata audio books)

vitabu

4. Njia ya nne ambayo napenda sana kuitumia mimi kujihamasisha kila siku asubuhi ni kutembelea mitandao mbalimbali inayotoa mazungumzo yanayohamasisha. Mtandao kama YOUTUBE una video nyingi sana za kuhamasisha kwa chochote unachofanya. Mtandao mwingine mkubwa na mzuri sana wa kujihamasisha ni TED TALKS(tembelea www.ted.com). Mtandao huo una video nyingi sana zilizotolewa kitaalamu na zenye uhamasishaji mkubwa. Ukiweza kuangalia video moja tu kwa siku(kama utaweza kuchagua nzuri, maana zipo nyingi) utaweza kuianza siku yako ukiwa na mtizamo chanya na kuimaliza kwa furaha. Nakusihi sana utembelee mtandao huo, download baadhi ya video kisha anza kuangalia na kuzisikiliza.

ted

  Jinsi unavyoziishi siku zako ndivyo unavyoelekea kwenye mafanikio. Tujitahidi sana kuziishi siku zetu vizuri ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea. Njia mojawapo ya kuziishi siku zetu vizuri ni kujihamasisha.

  Kujihamasisha hakufanyiki tu mara moja kisha ukawa umekamilika, hiki ni kitu cha kufanya kila siku, kama ilivyo kuoga au kula. Ukatishaji tamaa upo kila siku na kila mahali, hivyo usipokuwa na kitu cha kukusukuma ni rahisi sana kukata tamaa.