Mara nyingi watu wamekuwa wakiwasiliana na mimi baada ya kusoma makala mbalimbali nzuri kwenye blog hii. Kutokana na makala hizo wengi huamua kufanya maamuzi ya kubadili maisha yao na kufuata ushauri unaotolewa kwenye makala hizo.

  Baada ya muda ukiwafatilia watu hao unakuta wamerudia maisha yao ya zamani. Yale yote waliyoahidi kufanya ili kubadili maisha yao yanakuwa yamewashinda na wanaamua kurudia maisha yao.

  Hata wewe ni mmoja wa watu hao, sio lazima uwe umesoma blog hii na ukaamua kubadilika ila katika wakati fulani kwenye maisha yako umewahi kufanya maamuzi kwamba kuanzia sasa unayabadili maisha yako. Unakuwa umekutana na vikwazo ama unakuwa umeshauriwa na kujiridhisha na nafsi yako kwamba sasa ni wakati wa kubadilika.

tofauti

  Baada ya kufanya maamuzi hayo siku chache za mwanzo huwa nzuri sana. Unakuwa na furaha sana kwa kuwa maisha yako yanakwenda kubadilika na kuwa bora zaidi.

  Nini kinatokea wiki ama mwezi baada ya hapo?

  Mara nyingi baada ya muda kupita unajikuta taratibu unarudia maisha yako ya zamani. Na unaanza kujiridhisha kwamba maamuzi uliyofanya yasingewezekana kwako hivyo unarudi ulikotoka na maisha yanaendelea yalivyokuwa.

  Kila mtu ameshapitia hali hii katika kipindi fulani kwenye maisha yake. Na wengi tunaishia kurudia maisha yetu ya awali kwa sababu kuna vitu fulani ambavyo tunakuwa hatujavijua kabla hatujafanya hayo maamuzi.

  Unapoamua kufanya maamuzi ya kubadili maisha yako, iwe ni kubadili tabia, mtazamo, au kazi, kuna vitu viwili vya msingi unavyotakiwa kuvijua. Kwa kuvijua vitu hivi inakuwa rahisi kwako kuvuka nyakati ngumu ambazo ni lazima ukutane nazo.

1. Sio kitu rahisi. Mabadiliko sio kitu rahisi na wala haijawahi kuwa rahisi. Mabadiliko yoyote ni magumu na yanahitaji maamuzi magumu. Sio kitu rahisi kuacha tabia ama mfumo wa maisha uliozoea zaidi ya miaka ishirini na kuanza mfumo mpya. Ni kitu ambacho kinahitaji kujitoa kweli na kuwa tayari kupitia nyakati ngumu. Kwa kujua kwamba mabadiliko sio rahisi itakurahisishia kuzivuka nyakati ngumu.(soma; ingekuwa rahisi kila mtu angefanya)

2. Kuna vita kubwa kati yako na jamii inayokuzunguka pale unapofanya mabadiliko ya mfumo wako wa maisha. Hili ndilo tatizo kubwa sana unalokutana nalo kila unapoamua kufanya mabadiliko. Kabla hujaamua kufanya mabadiliko kwenye maisha yako kuna mfumo wa maisha uliokuwa unaishi ambao wengi wa wanaokuzunguka wanaishi. Hivyo mnakuwa pamoja kwa sababu wote mnafanya vitu vinavyoendana. Unapoamua kufanya mabadiliko kuna vitu vingi ulivyokuwa unafanya ambavyo inabidi uviache, hapo ndipo tatizo linapoanzia.(soma;wanaokuzunguka wana mchango mkubwa wa hapo ulipo)

  Kutokana na mabadiliko yako utaanza kujiona hauendi sawa na jamii inavyokwenda, walio karibu yako watakukatisha tamaa na kama hujajipanga vizuri huwezi kuvuka kikwazo hiki.

  Kwa mfano umeamua kujisomea vitabu ili kubadili jinsi unavyofikiri na kubadili maisha yako na muda pekee unaoweza kujisomea labda ni jioni baada ya shughuli zako. Na muda huo huo ni muda ambao mmezoea kukutana na marafiki zako kwa ajili ya maongezi, matembezi ama kukutana baa na kupata vinywaji. Wewe unaamua kuvunja ratiba hizo na kutumia muda huo kuboresha maisha yako, unafikiri ni kitu rahisi? Kwanza marafiki zako watakuona wewe ni mtu wa ajabu, yaani badala ya kupumzika nao unaenda kusoma vitabu? Halafu ukishavisoma inakuwaje? Wako ambao watakuambia maisha ni mafupi acha kujitesa.

  Mfano mwingine unaweza kuwa umeamua kuamka asubuhi na mapema kwa ajili ya kuianza vizuri siku yako kwa kujisomea kidogo na pia kuipangilia siku yako. Ila kila unapoamka wengine wote wamelala, ni rahisi sana kurudi kulala kama utawaangalia wao.

  Kwa maamuzi yoyote ya mabadiliko unayofanya lazima utakwenda kinyume na mfumo wa maisha uliozoeleka kwenye jamii unayoishi. Kama hujafanya maamuzi thabiti ya kusimamia maamuzi yako ni rahisi sana kurudi kwenye maisha yako ya awali.

  Jamii inapenda sana watu wanaofanya yale ambayo kila mtu anayafanya. Na pia jamii inawatenga wale ambao hawafanyi yale ambayo kila mtu anayafanya.

  Unapofanya maamuzi jua kabisa sio kitu rahisi na pia una vita kali na jamii inayokuzunguka

  Ungana na watanzania wenzako wanaojisomea vitabu kwa kujiunga na mtandao huu. Bonyeza maandishi haya na uweke email yako ili uweze kutumiwa vitabu mbalimbali na uweze kubadili maisha yako.