Kila mtu anajua kwamba ipo siku atakufa. Pamoja na jitihada zote tunazofanya kufikia malengo mbalimbali kwenye maisha mwisho wa siku wote tunaelekea njia moja kupitia kaburi.

  Una uhakika kwamba utakufa, iwe umefanikiwa au la, uwe tajiri au masikini kifo kitakufika tu. Kwa maana hiyo kifo sio cha kuogopa hapa, ila kuna swali moja la msingi sana ambalo unatakiwa kujiuliza kabla kifo hakijakufika.

  Swali lenyewe ni nini kitatokea baada ya wewe kufa?

  Jumamosi ya tarehe 30/11/2013 kulitokoea msiba wa mwigizaji maarufu wa filamu wa marekani aliyekuwa akiitwa Paul Walker. Nilipata taarifa za msiba huo kupitia mitandao ya kijamii ambapo niliona watu wengi wakitoa salamu za kumuaga paul(wengi waliandika R.I.P PAUL WALKER). Baadae nilifuatilia habari hizo za msiba na kugundua kwamba katika ajali aliyofariki Paul pia kuna mwenzake alifariki. Lakini jamii kubwa inatoa salamu za kuaga kwa paul peke yake!!

paul walkerpaul akiwa na rafiki yake waliofariki pamoja

  Kitu hiko kilinifanya nifikiri sana iweje watu wanajua wamefariki watu wawili kwenye ajali moja ila mmoja anapewa salamu za kuagwa na mwingine hakuna anayehangaika nae kabisa? Je huyu mmoja ni binadamu zaidi ya mwenzake?

 paul walker2 gari waliyopatia ajali.

  

  Hapa ndipo nilipopata picha kwamba kuna kitu kitatokea baada ya kila mtu kufa. Je unakijua kitakachotokea baada ya wewe kufa?

  Katika msiba huo wa Paul utaona yeye ameagwa na watu wengi kushinda mwenzake ambaye walikuwa marafiki kwa sababu yeye paul aliyagusa maisha ya watu wengi. Kupitia kipaji chake cha uigizaji wa filamu aliweza kutumia ubunifu mkubwa na kuwa wa tofauti na waigizaji wengine. Kupitia utofauti huo aliweza kugusa maisha ya watu wengi. Hivyo kifo chake kimewashitua watu wengi kuliko kifo cha rafiki yake ambaye walikuwa pamoja.

  Ni muhimu kujiuliza shughuli zako unazofanya na maisha yako unayoishi je ukifa leo ni nini kitatokea? Je kuna watu wataliona pengo lako ama watu watafurahia kuondoka kwako?

  Shughuli yoyote(halali) unayofanya hata iwe ndogo kiasi gani kama utaifanya kwa moyo, na kutumia ubunifu mkubwa ulio nao ni lazima kuna maisha ya watu utayagusa kwa hali chanya.

  Sio lazima uwe maarufu, ama uwe unafanya jambo kubwa sana. Chochote unachofanya, kama utakipenda na ukatumia uwezo na ubunifu mkubwa uliondani yako kuna watu wengi sana watakaofurahia matunda ya kazi yako. Kuna watu wengi sana ambao maisha yao yatakuwa bora kutokana na kazi yako.

  Jitahidi sana kutumia uwezo mkubwa ulioko ndani yako na pia kujua vipaji na ubunifu mkubwa ulionao kwenye kazi zako. Pia ni muhimu sana kufurahia kazi unayoifanya. Kwa kufanya hivyo utakuwa wa pekee na utagusa maisha ya watu wengi.

  Kama tulivyoona kwenye makala ya sio wote tunaowazika wamekufa, kuna watu ambao tunaishi nao kwenye maisha yetu mpaka leo ili hali tumewazika zaidi hata ya miaka mia iliyopita. (soma; sio wote tunaowazika wamekufa) Jitahidi sana na wewe uwe mmoja wa watu ambao hawatakufa.

  Inawezekana kuishi milele kwenye maisha ya wengine kama utagundua utofauti wako na binadamu wengine na kuweza kutumia utofauti huo kuleta mabadiliko kwenye maisha ya watu wengine.(soma; wewe ni wa pekee na umeletwa duniani kufanya mabadiliko)

  Yaangalie maisha yako unayoishi na kazi zako unazofanya kama unaona watu watafurahi siku utakayoondoka duniani unahitaji kubadilika haraka sana.