Safari hii ya maisha na harakati mbalimbali tunazofanya kila siku ili kuboresha maisha yetu haina bingwa. Kila mtu kwa wakati tofauti kwenye maisha anakutana na vikwazo mbalimbali. Kwa vikwazo hivyo wapo wanaovivuka na kuendelea na maisha yao na wapo ambao vikwazo vinawashinda na kuharibu maisha yao.(soma; mambo mawili muhimu unayotakiwa kujua kuhusu maisha)
Inawezekana wewe ni mmoja wa watu ambao umekutana na vikwazo vingi kwenye maisha na kufikia kuona maisha yako hayana thamani tena. Huenda matatizo mbalimbali unayokutana nayo kwenye maisha yamegeuza maisha yako na kuwa mabaya na umeshakata tamaa na maisha yako.
Huenda umeshafikia hatua ya kuona ni bora kuachana na haya maisha kwa sababu hakuna jema unalopata kwenye maisha.
Unaweza kuwa sahihi kwenye hayo yote ila kuna jambo moja nataka nikueleze leo. Jambo hilo ni MAKABURI YAMEJAA WATU WENGI AMBAO WANGEPENDA KUWA NA MATATIZO ULIYONAYO.
Unaweza kufikiria kauli hiyo kwa urahisi sana ila ukiyaangalia maisha yako kwa upande mwingine utaelewa na kuanza kuyafurahia maisha yako.
Mara nyingi tumekuwa tukiangalia sana vitu gani hatupati kwenye maisha na kusahau kuangalia ni vitu gani vya muhimu tumepewa kwenye maisha.
Haijalishi matatizo unayopitia kwa sasa, kuwa tu na uhai ni kitu kikubwa sana unachotakiwa kushukuru. Kuna watu wengi sana ambao wanapigania maisha yao dakika hii unayosoma hapa. Watu wanatumia gharama kubwa na kusafiri mpaka nchi za mbali ili tu kunusuru uhai wao. Wewe unao uhai huo na hakuna gharama kubwa unayotakiwa kulipa kwa sasa ili kuuzuia usitoke, je huoni hiki ni kitu kikubwa sana kwenye maisha yako?
Unaweza kuwa na matatizo makubwa sana kwenye maisha ila kama unafanya mambo mema kuna watu wengi wanaokupenda. Kuna watu wanakupenda na wanaona mchango wako kwenye maisha yao. Japo huna mafanikio makubwa bado kuna watu wanakupenda sana kwa jinsi ulivyo, je huoni hiki ni kitu kikubwa kwenye maisha yako?
Una macho, mikono, miguu, masikio na viungo vyote vya mwili. Una uwezo mkubwa kwenye akili yako, una vipaji na ubunifu wa kipekee, je hivi ni vitu visivyo na thamani kwenye maisha yako?(soma; huu ndio utajiri mkubwa unaomiliki wewe)
Kabla hujakata tamaa na maisha yako hebu jipe muda na ufikiri thamani kubwa iliyo ndani ya maisha yako.
Hebu fikiria watu wanaotumia gharama kubwa kujaribu kuokoa uhai wao.
Hebu fikiria watu ambao wamekosa baadhi ya viungo ulivyonayo wewe na bado wanaishi.
Baada ya kufikiri yote hayo, chukua hatua dhidi ya maisha yako. Jua ya kwamba wewe ndio kiongozi mkuu wa maisha yako na ndiye utakayebadili maisha yako.(soma; mambo yanapokuwa magumu unafanya nini?)
Anza sasa kwa kushukuru kwa vitu vingi ambavyo unavyo kwenye maisha yako. Yapange maisha yako na kuwa dereva wa maisha yako.
Ama kweli nimepata mwalimu katika maisha.kwa kutokufanikiwa kiuchumi nilikuwa nawaza kuwa mungu ameniacha,hanipendi au amenisahau.lakini kwa funzo la makala hii mimi ambaye nina viungo kamili,akili timamu na afya njema bila gharama,nimebarikiwa sana.
LikeLike