Kila inapofika siku ya ijumaa kuna dalili moja huwa naiona sana kwenye mitandao ya kijamii hasa facebook. Watu wengi huweka maandiko ya kufurahia kufika mwisho wa wiki. Kuna kifupisho huwa kinatumika sana kwenye mitandao siku za ijumaa. Kifupisho hicho ni TGIF(Thanks God Its Friday), kwa maana kwamba wanamshukuru Mungu ijumaa imefika.

tgif

  Sio kwenye mitandao tu, hata katika maisha ya kawaida watu wengi sana wanaifurahia siku ya ijumaa. Ijumaa inasemekana ndio siku ambayo watu wengi sana wanakuwa na furaha kwa sababu ni karibu na siku za mapumziko.

  Siku za mwisho wa wiki ndizo siku zinazokuwa na starehe nyingi. Siku za mwisho wa wiki ndipo watu wanafanya matumizi makubwa ya fedha bila ya mpangilio.

  Kama na wewe ni mmoja wa watu ambao wanafurahia sana siku ya ijumaa nasikitika kukuambia kwamba HUNA MAISHA. Kama katika siku saba za wiki unaishi ukisubiria siku mbili tu ndio ufurahie basi ni vyema ukayatafakari maisha yako upya.

  Huna maisha kwa sababu tabia hii haitoisha bila ya wewe kuchukua hatua. Unakuwa na furaha sana inapofika ijumaa na unakuwa na huzuni sana kila jumapili jioni na jumatatu asubuhi. Na katikati ya wiki ndio unakuwa hujielewi kabisa.

  Hebu jiulize ni maisha ya aina gani ambapo una siku mbili za kufurahia na siku tano za kujisukuma? Ni maisha ya aina gani ambapo unaishi ukihesabu siku ngapi zimebaki kufika mwisho wa wiki?

  Kama unasubiri mwisho wa wiki kwa shauku kubwa ni vyema ukayaangalia upya maisha yako. Sisemi kwamba usipumzike au usifurahie maisha siku za mwisho wa wiki. Nachotaka hapa ni wewe ufurahie maisha kila siku ya wiki na sio mwisho wa wiki pekee.

  Unaweza kufurahia kila siku unayoishi na kuwa na mafanikio makubwa kila siku. Soma makala hii kujua jinsi ya unavyoweza kuyafurahia maisha yako kila siku.(hii ndio sababu kuu ya wewe kutofurahia maisha)

  Zitumie siku za mwisho wa wiki kuyapanga maisha yako na kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako. Soma makala hii kujua mambo matano unayotakiwa kufanya kila mwisho wa wiki(mambo matano muhimu ya kufanya kila mwisho wa wiki)

  Nakutakia kila la heri katika harakati zako za maisha. Tumia vizuri siku za mapumziko ya mwisho wa wiki kuyabadili maisha yako.