Mfalme wa nchi moja aliwaita watu wenye busara nakuwaambia nendeni mkatengeneze falsafa ya maendeleo ambayo kila mwananchi ataitumia kufikia mafanikio. Watu wale walikaa na kutengeneza vitabu kumi na mbili vinavyoelezea falsafa ya maendeleo na mafanikio. Walipovileta kwa mfalme, akawaambia nina hakika humo kwenye vitabu kuna falsafa nzuri lakini vitabu hivyo ni vikubwa na vingi sana hivyo watu hawataweza kumaliza kuvisoma. Akawaambia nendeni mkaifanye iwe rahisi ili kila mtu aweze kuisoma. Wakaenda kukaa wakatengeneza kitabu kimoja, bado mfalme akasema kitabu ni kikubwa mno. Wakaenda kutengeneza sura moja, mfalme akasema bado ni kubwa, wakatengeneza aya bado mfalme akasema ni kubwa kusoma. Mwishowe wakaenda kutengeneza sentensi moja, mfalme alipoisoma sentensi ile alitikisa kichwa kwa kuitika na kufurahi na kuwaambia hii ndio falsafa na busara ya vizazi vyote. Na kila mwananchi aisome na kuielewa na kuitumia kwenye maisha yake ya kila siku. Sentensi hiyo ilikuwa inasomeka HAKUNA KITU CHA BURE.

bure

  Ni kweli kabisa sehemu yeyote na katika maisha yoyote hakuna kitu cha bure. Kila kitu kina gharama unayolipa, iwe ya fedha, muda au hata utu wako. Lazima utoe kitu ili upate kitu. Hata kama ukiwa na kuni huwezi kupata moto bila ya wewe kuanzisha moto. Huwezi kuandaa shamba kisha ukategemea mazao kama hujapanda mbegu nzuri.

  Na katika maendeleo na mafanikio, huwezi kufikia mafanikio ya kweli bila ya kufanya kazi. KAZI NDIO MSINGI WA MAENDELEO. Maendeleo yoyote yanaanzia kwenye kazi. Mafanikio makubwa yanatokana na ufanyaji kwazi kwa bidii na maarifa. Hakuna kinachoweza kuondoa kazi katika swala la maendeleo na mafanikio.

  Wakati kazi ndio msingi wa maendeleo na mafanikio, jamii inatumia nguvu nyingi kukushawishi utumie njia nyingine kupata mafanikio.

Jamii inakushawishi ucheze kamari ili upate fedha nyingi kwa haraka.

Jamii inakushawishi ucheze bahati na sibu mbalimbali ili uweze kupata fedha nyingi kwa haraka.

Jamii inafurahia kuwaona watu wenye fedha nyingi huku kazi wanazofanya hazieleweki.

Jamii inakulazimisha utoe ama kupokea rushwa ili upate mafanikio.

Jamii inafurahia na kutegemea misaada kama njia ya kuwapatia maendeleo.

  Katika yote hayo ambayo jamii inakushawishi kufanya hakuna hata moja ambalo litakuletea mafanikio ya kweli na kuridhisha nafsi yako. Tumeona watu wengi wanaoshinda bahati na sibu mbalimbali, fedha wanazopata zinaishia wapi?

Tumeona watu wengi waliopata fedha nyingi kwa njia za wizi, ufisadi, rushwa na hata utapeli, lakini fedha na maisha yao vimeishia wapi?

  Kazi pekee ndio njia halali itakayokupatia mafanikio halali na yatakayoridhisha nafsi yako. Kama utafanya kazi halali kwa moyo, bidii na maarifa makubwa lazima utafanikiwa. Haijalishi ni kazi gani unafanya, kazi yoyote ina fursa nyingi za mafanikio kama utaamua kufanikiwa.(soma; hizi ndizo fursa unazozipita kila siku)

  Japokuwa jamii inakushawishi sana usifanye kazi na utafute njia mbadala ya mafanikio, jua kwamba hakuna njia mbadala zaidi ya kazi. Kama utaifata jamii kwa hili hakika unajiondoa kwenye njia ya mafanikio. Na ili ufanikiwe kwenye kazi yoyote unayofanya ni muhimu sana ubadili mtizamo wako juu ya kazi.(soma; kama unataka kufanikiwa usifanye kazi).

  Nakutakia kila la kheri katika kazi zako halali unazofanya na nikuhakikishie kama utafanya kwa moyo, bidii na ubunifu ni lazima utafanikiwa.