Unapozungumzia swala la hela ni lazima kila binadamu atahusika kwa namna moja au nyingine. Fedha ni moja ya vitu vinavyoamsha hisia za binadamu wote bila ya kujali umri, rangi, kabila wala dini. Fedha imepewa nafasi kubwa sana kwenye maisha ya kila siku ya binadamu.

  Pamoja na kwamba fedha imepewa nafasi kubwa sana kwenye maisha ya binadamu, bado ndio kitu kinachomtesa sana binadamu. Watu wengi sana wanapitia matatizo mengi kutokana na fedha. Mtu anaweza kupata matatizo kwa kukosa fedha na pia mtu anaweza kupata matatizo makubwa kwa kuwa na fedha nyingi.

PESA2

  Kutokana na matatizo hayo fedha imepewa majina mengi, mazuri na mabaya. Na mara nyingi watu wamekuwa wanasema fedha ndio inaleta matatizo. Ila kiukweli fedha haina tatizo na mtu bali tabia zetu sisi binadamu kwenye mambo ya fedha ndio zinasababisha matatizo yote.(soma; tatizo sio fedha, tatizo ni wewe.)

  Umekuwa ukisumbuka na fedha kila siku, unaona kipato hakikutoshi na hata kikiongezeka bado huoni mabadiliko. Unatamani sana uweke akiba ila unaona kipato chako hakitoshelezi wewe kujiwekea akiba hivyo kila mara unajikuta matumizi yako yanazidi mapato. Kama unapitia hayo ni kwa sababu kuna siri moja kuhusu malipo ambayo bado hujaijua. Leo utaijua siri hiyo na kama ukiamua kuitumia utabadili mfumo wako wa matumizi na utunzaji wa fedha.

  Kipato chochote unachopata unamlipa kila mtu kasoro mtu mmoja muhimu sana. Unamlipa anayeuza chakula, unamlipa anayeuza maji, unamlipa anayeuza umeme, unamlipa anayeuza mafuta na wengine wengi.

  Wote hao unawalipa kwa uaminifu mkubwa ili kupata huduma zao. Ila mtu ambae ni muhimu na ambae angetakiwa kuwa wa kwanza kulipwa unamsahau. Mtu huyo ni wewe. Ndio, mtu wa kwanza kulipwa ni wewe, yaani ni lazima uanze kujilipa.

  Unajiuliza utajilipaje wakati hivyo unavyolipia ndio vya muhimu?

  Katika kitabu cha MTU TAJIRI WA BABELI(the richest man in Babylon) imeshauriwa kwamba katika kipato chochote unachopata toa asilimia kumi ujilipe wewe kwanza. Asilimia hiyo kumi haitakiwi kuwekwa kwenye matumizi yoyote bali umejilipa wewe na inabidi kuitunza. Baada ya muda kiwango ulichohifadhi unaweza kuwekeza na kupata faida zaidi.

  Unaweza kufikiri kwamba kwa kuwa kwa sasa una kipato kidogo basi huwezi kutoa hiyo asilimia kumi na kuweka pembeni. Lakini ukiangalia kwa kina ukiondoa asilimia kumi kwenye kiwango chochote cha hela hakuna upungufu mkubwa sana. Kwa mfano kwenye laki moja, asilimia kumi ni elfu kumi, na kama ukiiweka pembeni unabaki na elfu tisini. Kama utashindwa kutimiza mahitaji yako kwa elfu tisini hata kwa laki moja bado hutoweza kutimiza. Na kama utaona kuishi kwa hiyo asilimia tisini hakuwezekani basi ni vyema kufanya jitihada za kuongeza kipato chako.

  Katika kipato chochote unachopata iwe ni mshahara au faida ya biashara hakikisha unaweka asilimia kumi pembeni. Fedha hiyo haitakiwi kuwa kwenye bajeti ya matumizi. Ni vyema ukajijengea utaratifu huu wa kuweka akiba kabla ya matumizi. Wengi wetu tumezoea kuweka akiba baada ya matumizi, na mara nyingi baada ya matumizi fedha yote inakuwa imeisha hivyo tunakosa cha kuweka akiba.

  Anza sasa kujilipa kwa sababu wewe ni wa muhimu kwako zaidi ya hao wengine wote ambao unakimbilia kuwalipa kwanza. Unaweza kuweka akiba asilimia yoyote unayoona inafaa kwako ila isiwe chini ya asilimia kumi.

  Kitabu cha MTU TAJIRI WA BABELI(the richest man in Babylon) kimejaa mafunzo mengi mazuri kuhusu matumizi ya fedha na jinsi ya kupata utajiri. Kama bado hujakisoma kitabu hiki kisome mara moja. Nilishakituma kitabu hiki kwa wanachama wa mtandao huu. Kama hujakipata nitakituma tena, jiunge na mtandao huu kwa kubonyeza maandishi haya na uweke email yako kisha utapata kitabu hicho na vingine vingi.