Msimu wa sikukuu unamalizika na majukumu yanaanza kurejea kama kawaida. Bado mwaka ni mchanga na bado una matarajio makubwa kwa mwaka huu 2014. Umeshaweka mipango yako ya mwaka huu na una mikakati ya kuitekeleza. Kilichobaki ni wewe kufanya yale uliyopanga kufanya.
Pamoja na kwamba umeshaweka malengo mazuri kwenye maisha yako kwa asilimia kubwa hutoyatimiza. Kama unabisha hili angalia malengo uliyoweka mwaka jana na miaka mingine iliyopita, kuna mambo mengi hukutimiza.
Kuna sababu nyingi zinazokufanya ushindwe kutimiza malengo yako, moja wapo ni jinsi unavyoweka malengo yako. Soma; makosa matano makubwa unayofanya wakati unaweka malengo, ili ujiepushe na makosa unayofanya kila mwaka na kujikuta unashindwa kufikia malengo uliyojiwekea mwenyewe.
![]()
Sababu nyingine kubwa inayotufanya tushindwe kufikia malengo yetu na tuone mwaka kama kisirani ni baadhi ya kauli tunazotumia. Kauli tunazotumia mara kwa mara kwenye maisha yetu hujiumba na kuwa kweli.
Moja ya kauli wengi wetu tunapenda kutumia kuhusu mwaka ni mwaka mbaya, mwaka wa shetani, mwaka wa visirani na kadhalika. Wakati mwaka 2013 unamalizika nilikuwa naona watu wengi wakisema bora mwaka huu uishe maana ulikuwa mwaka mbaya kwangu.
Kama na wewe unafurahia kuisha kwa mwaka 2013 kwa sababu ulikuwa mwaka mbaya kwako nasikitika kukuambia kwamba furaha yako ni ya muda mfupi sana. Furaha yako itakuwa ya muda mfupi kwa sababu mwaka huu 2014 utakuwa mbaya kwako zaidi ya mwaka 2013 ulivyokuwa.
Mwaka kuwa mbaya au mzuri haitegemei namba ya mwaka, matukio ya mwaka wala urefu au ufupi wa mwaka. Mwaka kuwa mbaya au mzuri inategemea na mtazamo wako wewe binafsi. Hivyo kama unaona mwaka jana ulikuwa mwaka mbaya ni kwamba mtizamo wako ni kuona mabaya zaidi ya mazuri na kwakuwa hujabadili mtazamo wako, mwaka huu 2014 utaendelea kuona mabaya zaidi ya unavyoona mazuri. Ndio maana nakuambia kama mwaka jana ulikuwa mbaya kwako, mwaka huu utakuwa mbaya zaidi.
Mtazamo wako na kauli zako ndizo zitaufanya mwaka uwe mbaya au mzuri. Acha kudanganyika na namba za miaka, hata mwaka uwe unaishia na namba tasa, witiri au namba shufwa hakuna tofauti yoyote baina ya miaka. Tofauti inaletwa na mtizamo wako wewe, kama una mtizamo chanya utauona mwaka ni mzuri na kama una mtizamo hasi utauona mwaka ni mbaya na kisirani.
Wengi wanauita mwaka mbaya kama wamekutana na vikwazo vingi ndani ya mwaka huo. Vikwazo ni lazima utakutana navyo na hata ukikutana navyo bado sio mwisho wa dunia(kama hutokufa), maisha lazima yataendelea. Sasa unauitaje mwaka mbaya kama umemaliza ukiwa bado unapumua? Usitumie changamoto na vikwazo vya kwenye maisha kuharibu hata maisha yako ya mbeleni kwa kuharibu mtazamo wako.
Jua kabisa lazima utakutana na changamoto nyingi hata kwenye mwaka huu 2014.(soma; mambo mawili muhimu unayotakiwa kujua kuhusu maisha) Na ili kuvuka vikwazo hivyo ni lazima uwe na mpango kamili wa maisha yako.(soma; mambo yanapokuwa magumu unafanya nini?)
Usiendelee kutumia tena hii kauli ya MWAKA MBAYA au MWAKA WA SHETANI kwenye mwaka huu mpya 2014.
Furahia maisha kwa kufurahia nyakati nzuri na kujifunza kwenye nyakati ngumu. Maisha ni ya kwako na wewe ndiye utakayeyajenga ama kuyabomoa.
Nakutakia kila la kheri kwenye mwaka huu mpya 2014, uwe wa mafanikio kwako na uwe na mtazano chanya kwenye kila jambo unalofanya.
Onyo; Usitumie Kauli hizi Mwaka huu Kama Unataka Mambo yako Yaende Vizuri.