Mafanikio ni msamiati ambao hauwezi kuwa na jibu moja kwa watu wote. Neno mafanikio linaweza kuwa na majibu mengi sawasawa na idadi ya binadamu tulioko duniani. Hii inatokana na kwamba mafanikio hayawezi kuwa na kipimo kimoja kwa watu wote duniani.
               
pima mafanikio
  Pamoja na hayo kwamba mafanikio ni tofauti kulingana na utofauti wa watu bado kuna watu wanateseka sana kwa kutokujua hili. Kuna watu wameshindwa kufurahia maisha na kila siku wanajikuta wana msongo wa mawazo kutokana na kutojua kwamba mafanikio ni kitu ambacho hakiwezi kuwa sawa kwa wote.
  Kuna watu wamejikuta wanalazimika kupima mafanikio yao kutokana na viwango vilivyowekwa na jamii. Hivyo malengo yao makubwa kwenye maisha yanakuwa kupata vile ambavyo watu waliofanikiwa kwenye jamii wanaonekana kuwa navyo. Inaweza kuwa kipimo kizuri sana ila tatizo liko hapa; Kama unafikiri mafanikio kulingana na jamii yako ni kuwa na gari na nyumba unaweza kujipanga sana ukapata hilo gari na nyumba, baada ya kuvipata hivyo utakuta kuna wengine wana nyumba kumi na magari matano, unajiona wewe bado. Unahangaika tena kupata vitu hivyo, wakati uko kwenye mipango ya kufikia hivyo unagundua kuna wengine wana ndege zao binafsi, wengine wanamiliki vitu vikubwa zaidi. Kwa kuangalia hivi unazidi kuchanganyikiwa na kujiona wewe kwenye maisha unacheza tu, ama unaigiza.
  Utajikuta unapata shida sana kwenye maisha kwa kufuata viwango vya mafanikio vilivyowekwa na jamii. Sikuambii usiangalie mafanikio ya wengine na uwe na wivu wa maendeleo. Nachokuambia hapa ni wewe kuwa na viwango vyako mwenyewe vya mafanikio ambavyo vitakufanya uishi maisha mazuri na ambayo utayafurahia.
  Wewe ni wa pekee, hakuna binadamu anayefanana na wewe duniani. Wewe una uwezo mkubwa na wa kipekee na pia una vipaji na ubunifu mkubwa ambao hauwezi kulinganishwa na binadamu mwingine. Sasa iweje ujilinganishe mafanikio yako na ya watu wengine?
  Wewe unajijua vizuri nguvu zako na mapungufu yako, na pia unavijua vipaji na ubunifu wako. Sasa weka malengo ya mafanikio kwa viwango vyako wewe mwenyewe kwa unavyojijua. Usijitese kwa kutaka kuwa kama kila mtu anayeonekana kufanikiwa kwenye jamii, utapata shida sana.
  Furahia maisha kwa kuwa na
malengo na mipango inayoendana na viwango vyako mwenyewe vya mafanikio. Pia usijiwekee viwango vidogo sana ambavyo vitakufanya ujione umefanikiwa kumbe bado hujatumia uwezo mkubwa ulioko ndani yako.
  Viwango unavyojiwekea hakikisha vinakupa changamoto ya kufikiri zaidi na kutenda zaidi. Hakikisha viwango hivyo vinakusukuma vya kutosha kuamka kitandani asubuhi kwenda kufanya yale yatakayokufikisha kwenye malengo yako.
  Unaweza kufanya mambo makubwa kama utaweza kutambua uwezo mkubwa ulionao. Unaweza kufanya makubwa kwa vipaji na ubunifu wa kipekee ulioko nao. Tumia vitu hivi kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yako na ya wanaokuzunguka. Usikubali kufuata kundi na ukaishi maisha ya kuteseka kila siku.
  Kama bado unasumbuka kuweka malengo yanayoweza kubadili maisha yako soma makala hii (jinsi ya kuweka malengo utakayoyafikia) na pia bonyeza hapa na ujaze fomu ya kuhudhuria semina ambayo itayabadili maisha yako.
  Kila la kheri na bado tuko pamoja.