Tayari umeshaweka malengo yako ya mwaka 2014 na kuendelea na tayari umeshaweka mipango mbalimbali ya kukusaidia kufikia malengo uliyojiwekea.
  Tayari pia umesoma
jinsi ya kuweka malengo utakayoyafikia na makosa matano unayofanya wakati unaweka malengo yako, na hivyo umeshajipanga vizuri ili usije kurudia makosa uliyokuwa unafanya miaka mingi ya nyuma na ukashindwa kufikia malengo yako.
jenga tabia
  Sasa kuna jambo moja kubwa ambalo ni lazima ulifanye ili uweze kufikia malengo uliyojiwekea. Jambo hilo ni rahisi sana ila utekelezaji wake ni mgumu kwa sababu inahitaji kujitoa hasa. Kabla ya kujua jambo hilo hebu tuangalie mifano michache ya mambo uliyoshindwa kutimiza.
  Hebu fikiri ni mara ngapi umekuwa na moyo wa kutaka kufanya au kuacha jambo fulani, unajipanga vya kutosha ila baada ya muda mfupi unajikuta umeshindwa kuendelea?
  Mara nyingi tunashindwa kufikia mipango yetu kwa sababu hatujui kwamba kupanga na hata kufanya kwa moyo na shauku kubwa tu hakutoshi kutufanya tufikie mipango yetu.
  Kuna jambo moja la muhimu na lazima kufanya ili kuweza kufanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yako kwa kuweza kufikia
malengo na mipango uliyojiwekea. Jambo hilo ni KUJENGA TABIA.
  Ni muhimu na lazima kujenga tabia zitakazokufikisha kwenye malengo yako uliyojiwekea maishani. Nakuambia KUJENGA TABIA na sio KUBADILI TABIA. Kila kitu kwenye maisha kina gharama, na ili kufanikiwa kuna gharama lazima ulipe. Ili uweze kulipa gharama hizo ni lazima ujenge tabia itakayokuwezesha kufanya hivyo.(soma; hii ndio gharama ya mafanikio unayotakiwa kulipa)
  Huwezi kufikia malengo na mipango yako kama utaendelea na maisha hayo hayo uliyokuwa unaishi kila siku na yakakufikisha hapo ulipo. Ni lazima ubadili sehemu kubwa sana ya maisha yako kama unataka ufikie mafanikio makubwa na kama umejiwekea malengo makubwa. Na ili uweze kubadili maisha yako ni lazima UJENGE TABIA tofauti na ulizo nazo sasa ambazo zimeshindwa kukupatia mafanikio unayotazamia.
  Tabia moja kuu unayotakiwa kujenga(zipo tabia nyingi) ni kuhudhuria kila siku. Ni lazima ujenge tabia ya kila siku kufanya kitu ambacho kitakusogeza karibu na mafanikio unayotazamia. Naposema kila siku namaanisha siku 365 kwa mwaka, bila kujali siku ya wiki au siku za mapumziko ya mwisho wa wiki au sikukuu. Usikubali siku iishe bila ya kufanya kitu kilichopo kwenye malengo yako, hata kama utafanya kitu kidogo sana ni bora kuliko kutofanya kabisa.
  Hata kama hujisikii vizuri ama umevurugwa ni lazima ukae chini na kufanya jambo moja ambalo lina msaada kwenye malengo na mipango yako. Labda kama una hali mbaya sana ya ugonjwa au umekumbwa na matatizo makubwa ambayo yanakuzuia kufanya jambo lolote, hata kufikiri tu.
  Tabia nyingine unazotakiwa kujenga ni;
1. Kufanya mambo kwa kurudiarudia ili kujenga uzoefu na ujuzi.
2. Kuacha kukwepa kufanya jambo ambalo ni lazima ulifanye ili kufikia malengo yako.
3. Kuwa na nidhamu ya hali ya juu kwenye matumizi yako ya fedha na ya muda.
4. Kuacha kutafuta sababu za kutokufanya mambo ambayo ni muhimu ili kufikia malengo yako.
5. Kujipongeza pale unapofikia malengo uliyojiwekea kwa siku au wiki.
  Kujenga tabia ni muhimu sana ili kufanikiwa maishani. Na tabia unayotakiwa kujenga ni tofauti sana na maisha ya watu wengine kwenye jamii. Sio kitu rahisi kujenga tabia ila kidogo kidogo unaweza kujenga tabia unayoitaka ili uweze kufikia malengo yako.