Maisha yetu binadamu yanatofautiana kwa kiwango kikubwa sana. Kuna watu wanaishi maisha ya kawaida ila wanafuraha sana na kuna watu wanaishi maisha ya kifahari ila hawana furaha. Kuna watu wanaonekana kushindwa kwenye mambo mengi ila maisha yao yanaenda na kuna watu wanajitahidi wasishindwe kwenye jambo lolote wanalofanya na bado maisha yao ni magumu sana.
Ndivyo sarakasi za maisha zilivyo, kila mtu anahangaika na yake kwa njia anayojua mwenyewe. Japo kuna wengine wanaiga maisha ya wengine ila kwenye furaha au huzuni inawakuta wao.
Kuna kosa moja sana tunalifanya kwenye maisha ambalo linatugharimu furaha na utulivu wa maisha. Kosa hilo limefanya baadhi ya watu wapate msongo wa mawazo na wengine wanaishia kukata tamaa kabisa na maisha. Kutokana na kufanya kosa hilo umekuwa ukijitesa sana kwenye maisha, leo utaondoa mateso hayo baada ya kusoma hapa.
Kosa kubwa unalofanya kwenye maisha yako ni kufikiri kwamba maisha yatakwenda vile ulivyopanga kwa asilimia mia moja. Hicho ni kitu ambacho hakiwezi kutokea duniani. Hata uhangaike vipi kuna jambo fulani halitokwenda sawa. Hata ujiumize na kujitesa kiasi gani kuna vitu hutoweza kuvikamilisha. Sasa kwa nini unajitesa na wakati kuna vitu viko nje ya uwezo wako?
Unaweza kuwa na malengo na mipango mizuri ila kwenye utekelezaji likajitokeza jambo ambalo linakuzuia kukamilisha mipango yako kwa wakati. Unaweza kufanya mambo yako vizuri akatokea mtu mwingine akaharibu. Ndivyo maisha yalivyo, kama wewe utaumia kwa kila jambo linalotokea maisha yako yatakuwa magumu sana na hutokuwa na furaha.
Wacha mambo yaende, furahia maisha. Ukikwama jambo moja kuna jingine utakamilisha, furahia lile ulilokamilisha na jifunze kwa lile ulilokwama. Tumia uwezo, juhudi na maarifa kufanya upande wako, ikitokea upande mwingine umekwamisha usijiumize endelea mbele.
Kama kuna makosa makubwa umefanya na kusababisha ushindwe kufikia ulikopanga kufika jifunze kutokana na makosa hayo kisha achana nayo. Songa mbele, usitumie muda mwingi kuangalia nyuma ni nini kilitokea, ukishajifunza nenda mbele achana na ya nyuma.
Hakuna haja ya kujitesa kwa sababu ya vitu fulani ulivyoshindwa kukamilisha au ulivyokwamishwa. Bado una mambo mengi sana ya kufurahia na kushukuru kwa hapo ulipo.
“Acha kujitesa, maisha hayawezi kuwa asilimia mia moja ya vile unavyotaka yawe”