Katika wakati wowote kwenye maisha yako muda ni tatizo. Kwa wakati wowote na popote ulipo una mambo mengi ya kufanya na muda hautoshi. Hata unapojaribu kupanga ratiba na kuwa na mipango bado muda ulioko nao haukutoshi na mambo unayohitaji kufanya yanaonekana ni mengi sana.

                 huwezi kufanya kila kitu

  Kama usipokuwa na mipangilio mizuri unaweza kujikuta unapata msongo wa mawazo kutokana na mambo unayotakiwa yanavyozidi kuwa mengi na jinsi ambavyo muda haukutoshi kukamilisha yote.

  Wakati mwingine jinsi unavyozidi kujaribu kufanya mambo yako ndivyo unavyozidi kukosa furaha kwa sababu ya majibu unayoyatoa kutokuwa mazuri. Unajikuta una siku iliyoko “bize” ila mwisho wa siku ukiangalia ulichofanya hukioni.

  Kama unapitia nyakati kama hizo kwenye shughuli zako ni kwa sababu hujajua jinsi ya kupangilia mambo yako. Ukweli ni kwamba huwezi kufanya kila kitu ambacho unataka kufanya. Huna ujuzi wa kutosha na wala huna muda wa kutosha kufanya kila unalofikiri inabidi ufanye. Ila kuna jambo moja au mambo machache unaweza kufanya na ukapata mafanikio makubwa sana.

  Jukumu lako kubwa ni kujua jambo hilo au mambo hayo na kuhamishia nguvu zako katika mambo hayo machache ili upate mafanikio unayotazamia.

  Katika mambo yote ama shughuli zote unazofanya kuna chache ambazo ukizifanya unafurahi sana na pia unatoa majibu mazuri sana ambayo kila mtu anayafurahia. Kuna jukumu fulani ikilifanya hata wanaokuzunguka wanafurahia sana jinsi ulivyofanya na wewe mwenyewe unafurahia sana majibu unayopata. Jukumu hilo ndilo lililobeba mafanikio yako. Kama ukiweza kulitambua na kulifanya kwa ubunifu mkubwa basi majibu yatakuwa mazuri zaidi na utapata mafanikio makubwa.

  Wewe ni wa pekee na una uwezo mkubwa sana, vipaji na ubunifu wa kipekee. Kuna vitu vya kipekee unaweza kufanya ambavyo hakuna mtu mwingine anayeweza kufanya. Na katika vitu hivyo kuna ambavyo majibu yake yana manufaa makubwa kwenye kazi zako ama biashara zako. Vijue vitu hivyo na wekeza kila siku katika kuviendeleza ili kupata mafanikio makubwa.

  Inawezekana uko vizuri sana kwenye uongozi, ama una ushawishi mkubwa au unaweza kuandika vizuri sana. Pia inawezekana ukipangilia mambo kila mtu anafurahi ama ukifanya kazi ya sanaa watu wanaipenda sana. Inawezekana ukifanya biashara fulani wateja wanafurahi na unapata faida kubwa. Kama umeajiriwa kuna vitu fulani ukifanya kwenye kazi zako wafanyakazi wenzako na hata bosi wako anafurahia sana majibu unayotoa. Kwa vyovyote vile kuna kitu ukifanya majibu yanakuwa tofauti na vitu vingine. Hivi ndivyo vitu vitakavyokuletea mafanikio kama ukiviendeleza.

  Mwanga wa jua unajoto la kawaida la kumulika vitu. Ila mwanga huu ukikusanywa sehemu moja kwa kutumia lensi unaweza kuchoma kitu na kikawaka moto. Na kama mwanga huu utakusanywa kwa utaalamu mkubwa zaidi na ukawa mionzi(laser beam) unaweza kukata chuma. Unafikiri ni kitu gani kimeufanya mwanga wa jua unaoufurahia kila siku kuwa na nguvu ya kukata chuma?

  Kwa kujaribu kumulika dunia nzima mwanga wa jua unagawa sana nguvu yake na hivyo kuishia kuwa mwanga tu. Kwa mwanga huu huu kukusanywa sehemu moja na kuelekezwa kwenye sehemu moja tu unaweza kukata chuma. Hivyo ndivyo ilivyo kwa ufanisi wako na nguvu zako. Ukijaribu kufanya kila kitu utafanya ila majibu yatakuwa ya kawaida sana ambayo hayatamshtua mtu yeyote. Ila ukielekeza nguvu zako na ufanisi wako kwenye vitu vichache utapata majibu mazuri ambayo yatamshangaza kila mtu ukianza na wewe.

  Punguza hitaji la kutaka kufanya kila kitu, panga vitu vichache ambavyo unapendelea kuvifanya na ambavyo vitakupatia mafanikio unayotazamia kisha weka nguvu zako zote na ufanisi wako wote kwenye kufanya vitu hivyo. Utajikuta una muda mwingi zaidi, unafurahia unachofanya zaidi na hutokuwa na msongo wa mawazo.