Ili uweze kubadili maisha yako ni lazima uanze kwa kubadilika wewe kwanza. Huwezi kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako na kubadili maisha yako kwa kiasi kikubwa kama utaendelea kufanya mambo unayofanya kila siku.

      “Ili upate kitu ambacho hujawahi kupata ni lazima uwe mtu ambaye hujawahi kuwa”

  Na ili uweze kupata mabadiliko makubwa kwenye maisha yako kuna wakati mgumu sana utakaopitia mwanzoni. Unapoanza kufanya jambo lolote jipya kuna upinzani mkubwa sana unaokutana nao kutoka ndani yako na kutoka kwenye mazingira yanayokuzunguka. Kama hujajipanga vizuri au kama huna sababu kubwa inayokufanya ufanye jambo hilo jipya ni rahisi sana kuacha jambo hilo jipya unalofanya.

        usijidanganye

  Na ili kujiridhisha kwamba hukuweza kufikia mabadiliko uliyotaka kuna sababu nyingi za kijinga ambazo huwa unatumia. Umekuwa ukitumia sababu hizo mara kwa mara ili kukimbia mwanzo mgumu wa kufanya mabadiliko kwenye maisha yako. Na pia sababu hizo zinakupa faraja kwamba kushindwa kufikia mabadiliko uliyotaka sio kosa lako bali ni nje ya uwezo wako.

  Nasema sababu hizo ni za kijinga kwa sababu hakuna hata moja ambayo ni ya kweli. Pamoja na kwamba sio za kweli zimekuwa zikitumiwa sana hasa na watu ambao wameshindwa kwenye maisha.

  Hapa nitazungumzia sababu tano za kijinga unazopenda kutumia sana kufunika kushindwa kwako.

1. Muda umeshanitupa mkono, laiti ningelikuwa kijana.

  Hii ni sababu ya kijinga inayotumiwa na watu ambao umri wao umekwenda kidogo. Unakuta mtu ana miaka 50 na anagundua kuna makosa alifanya kwenye maisha yake. Badala ya kuangalia njia za kubadili au kuanza upya anatoa sababu kwamba muda umeshakwenda hivyo hakuna jambo kubwa anaweza kufanya. Katika wakati wowote kwenye maisha yako kama uko hai unaweza kuyabadili maisha yako vile unavyotaka. Usitumie umri kama kikwazo.

2. Sina elimu ya kutosha.

  Kuna wakati watu hufikiri kwamba kinachowazuia kufanya mambo makubwa kwenye maisha yao ni ukosefu wa elimu. Inaweza kuwa kweli huna elimu ya kutosha ila je unafanya nini kurekebisha hilo? Kwa ulimwengu wa sasa unaweza kupata elimu yoyote unayohitaji kwa gharama ndogo sana. Kinachotakiwa ni wewe tu kuhitaji elimu hiyo na kuanza kuitafuta. Usitumie ukosefu wa elimu kama kigezo cha wewe kushindwa bali tafuta elimu unayohitaji ili ufanikiwe.

3. Nimetoka kwenye familia masikini

  Nadhani hii ndio sababu inayotumiwa na watu wengi walioshindwa hasa wanapoangalia wenzao ambao wamefanikiwa na familia zao zina mafanikio makubwa. Mara nyingi unajikuta ukishawishika kwamba kama ungetoka kwenye familia yenye uwezo basi huenda na wewe ungekuwa na mafanikio makubwa. Inaweza kuwa kweli ila tayari haujatoka kwenye familia yenye uwezo, sasa unafanya nini kutoka hapo ulipo? Tunafahamu watu wengi waliofanikiwa sana kwenye maisha hawakutoka kwenye familia zenye uwezo mkubwa. Wao walifanya nini wakafanikiwa? Jua na wewe uanze kufanya ili upate mafanikio makubwa.

4. Sina bahati

  Ni mara ngapi umewahi kufikiri huna bahati na kuona wenzako wanaofanikiwa sana kama ndio wenye bahati sana? Ni mara ngapi umeona watu wanapata fursa na wanabadili maisha yao ila wewe unakosa kwa sababu huna bahati? Huu ni uongo mkubwa sana ambao umekuwa unajidanganya kwa muda mrefu. Kila mtu ana bahati na bahati yako unaitengeneza mwenyewe. Bahati ni fursa iliyokutana na maandalizi. Hivyo jiandae vya kutosha kisa tafuta fursa na utengeneze bahati yako mwenyewe.

5. Nitaanza kesho

  Kama kuna uongo ambao umemaliza ndoto za watu wengi sana duniani basi ni huu wa kwamba nitaanza kesho. Ubaya ni kwamba kesho huwa haifiki. Hivyo kama una mipango mikubwa ya kubadili maisha yako ila unasema utaanza kesho au utaanza baada ya kitu fulani kufanyika basi jua hutofanya kabisa mipango yako. Kama kuna kitu ambacho unataka kufanya ili kubadili maisha yako anza sasa na anza mara moja.

  Sababu hizi na nyingine nyingi zimekuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Acha kujipa sababu, hakuna sababu yoyote inayokuzuia wewe kufikia mafanikio unayotazamia kwenye maisha yako.

  Kama utaendelea kutumia sababu zisizo za msingi utaendelea kuyaona mafanikio kwa wengine na utajiona kama wewe una kisirani. Kama utaamua kufanya vyovyote vile ili ufanikiwe basi utafanikiwa.

  Kama unafikiri unaweza au unafikiri huwezi uko sahihi kabisa. Badili mtazamo wako kubadili maisha yako.