Kuna wakati unaona mambo mazuri yanatokea kwa watu wengine ila kwako wewe hayatokei. Wakati kama huo unaona labda mambo hayo hayatokei kwako kwa sababu wewe huna bahati. Unaona mambo hayo mazuri yanatokea kwa watu wengine kwa sababu wao wana bahati nzuri.
Wakati mwingine unaona mambo mabaya yanatokea kwako tu. Na wakati kama huo unaona kama wewe una bahati mbaya.
Kwa kuwaona watu wanaokuzunguka wanapata nafasi nzuri za kubadili maisha yao ila wewe unakosa nafasi hizo unakubali kwamba wewe huna bahati ila wao wana bahati nzuri. Unaweza kuwa unafanya kazi, na mfanyakazi mwenzako ambao hamtofautiani sana ukashangaa anapata nafasi nzuri kwenye kazi yenu. Unaweza kuwa unafanya biashara ukaona wafanya biashara wenzako ambao hamtofautiani sana wanapata mafanikio makubwa ila wewe unabaki ulivyo. Kila ukijaribu kufikiria kwa nini mambo mazuri yanatokea kwa wengine ila kwako hayatokei unakubali kwamba wewe huna bahati au una bahati mbaya na wenzako wana bahati nzuri.
Je ni kweli huna bahati?
Kama mambo mazuri hayatokei kwako, ndio ni kweli huna bahati. Na kama unaona yanatokea kwa wengine basi wao wana bahati. Habari njema kwako ni kwamba hata wewe unaweza kuwa na bahati kama utaamua bahati iwe upande wako. Mpaka sasa huna bahati kwa sababu hujajua nini maana ya bahati na ni jinsi gani unaweza kuielekeza bahati upande wako.
Bahati ni nini?
Bahati ni maanadalizi yaliyokutana na fursa. Bahati sio jambo ambalo linatokea tu kimiujiza, ila kuna kazi inayofanyika kutengeneza bahati. Kuna baadhi ya mambo huwa yanatokea kimiujiza ila ni machache sana. Bahati inatengenezwa, hata wewe unaweza kuitengeneza upande wako na ukaanza kupata mambo mazuri kwenye maisha yako.
Ili kutengeneza bahati kwenye maisha yako fanya mambo haya mawili.
1. Fanya maandalizi ya kutosha. Kama tulivyoona kwamba bahati ni maandalizi yaliyokutana na fursa, cha muhimu na msingi kwenye maisha yako na kazi zako ni kufanya maandalizi. Jiandae kupokea vitu unavyotaka kwenye maisha yako, jiandae kufanya vitu unavyotaka kufanya kwenye shughuli zako. Utakutana na bahati pale ambapo wewe unaweza kufanya jambo ambalo hakuna mtu mwingine anayeweza kulifanya. Kwa mfano kama umeajiriwa ila wewe ukawa unajifunza komputa kwa muda wako wa ziada, wakati wenzako wanapiga soga. Siku ofisi ikinunua kompyuta na akakosekana mtu wa kuitumia wewe ndiye utakayepata nafasi ya kutumia kompyuta hiyo. Kwa mtu ambae hakukuona wakati unateseka kujifunza kitu hicho kipya ataishia kusema wewe una bahati ndio maana umepewa nafasi hiyo. Kumbe ukweli ni kwamba wewe ulikuwa na maandalizi kabla. Fanya maandalizi ya ziada kwenye kazi zako, biashara na hata maisha ya kawaida. Hakikisha kuna kitu fulani unaweza kufanya ambacho watu wengine hawawezi.
2. Tafuta fursa zinazoendana na maandalizi yako. Tumesema bahati ni maandalizi yaliyokutana na fursa. Kama una maanadalizi ila ukaishia hapo ni vigumu sana kukutana na fursa. Tafuta fursa zinazoendana na maandalizi yako na uanze kuonesha uwezo na ujuzi wako wa ziada. Kwenye mfano wa kujifunza kompyuta niliotumia hapo juu, kama nafasi hiyo ya kutumia kompyuta imepatikana ila wewe hukujionesha kwamba unaweza kufanya hivyo ni vigumu sana kwako kukutana na fursa. Hakuna mtu atakayekuangalia usoni na kujua wewe una kitu cha ziada, wewe ndiye unayetakiwa kuwaonesha watu kwamba una kitu cha ziada. Ni jambo la muhimu sana kuangalia fursa zinazopatikana kulingana na maandalizi yako kisha kuonesha uwezo na ujuzi wako wa ziada.
Acha kujifikiria kwamba wewe huna bahati. Unaweza kutengeneza bahati kwenye maisha yako kwa kujua kitu fulani ambacho hakuna mwingine anayejua. Au kuweza kufanya kitu fulani ambacho hakuna mwingine anayeweza kufanya. Tafuta ama jua kitu hicho na anza kukifanyia kazi. Bahati iko kwenye mikono yako mwenyewe amua kuanza kuitumia.
Angalizo; Bahati nayozungumzia hapa huwezi kuitumia kwenye michezo ya kubahatisha na kamari.