Jifunze Kusema Hapana, Itakusaidia Sana Kwenye Maisha Yako

  Mpaka sasa una malengo na mipango mikubwa ya kubadili maisha yako. Na ili kufikia malengo hayo unajua(kama ulikuwa hujui basi jua) kwamba ni lazima ufanye mabadiliko makubwa kwenye maisha yako. Ni lazima ubadili baadhi ya tabia zako na pia ni lazima uwe na mipango mizuri unayoitekeleza kila siku.

        HAPANA ED

  Pamoja na kujua yote hayo bado unapata shida ya kutekeleza mipango yako. Kila siku unaipangilia vizuri siku yako ila mwisho wa siku unajikuta unashindwa kutekeleza mipango yako. Unaweka mipango mizuri ya kufikia baada ya muda fulani na unaweka mchanganuo mzuri wa nini unatakiwa kufanya kila siku ila baada ya siku chache unajikuta haupo kwenye mstari uliotarajia kuwepo.

  Unapofikia wakati kama huu unajikuta unachanganyikiwa na hujui ufanye nini. Umeambiwa uweke malengo ukaweka, umeambiwa weka mipango ya kutekeleza kila siku umeweka, umeambiwa tena kila siku fanya jambo la kukufikisha kwenye malengo yako, hapa ndipo shida inapoanzia. Unajaribu kufanya jambo la kukufikisha kwenye malengo yako kila siku ila unashindwa. Mwishowe unaamini kwamba yote uliyoambiwa kuhusu kuweka malengo na mipango ni uongo ama hayawezi kufanyika kwako.

  Kabla hujaamini sana hicho unachofikiri soma hapa kwa makini na kisha ujiangalie tena. Zipo sababu nyingi sana zinazokufanya ushindwe kufikia malengo uliyojiwekea ama kufanya mipango uliyojiwekea. Moja ya sababu hizo ni kusema NDIO zaidi ya unavyosema HAPANA.

  Hebu fikiri ni mara ngapi na kwa watu wangapi umekuwa unasema NDIO?

Mtu anakuja na wazo lake ambalo halipo kwenye mipango yako na haliwezi kukusaidia ila unasema NDIO ili kumridhisha.

Mtu anakuambia mawazo yako makubwa hayawezi kutekelezeka kwa sababu fulani anazoziamini yeye na wewe unasema NDIO.

Umeweka mipango yako labda saa sita mpaka saa nane mchana utakuwa unafanya kitu fulani ili kufikia malengo yako, anatokea rafiki yako(ama anakupigia simu) anakuambie mwende mkatembee unamwambia NDIO.

Umeamua kubadili tabia ambayo inakuzuia wewe kufikia malengo yako, ila wale uliokuwa unashirikiana nao kwenye tabia hiyo(kama ulevi) wanapokushawishi kwamba usiache ama uendelee kuwa nao unasema NDIO mwishowe unabaki na tabia yako.

  Umekuwa ukisema NDIO, NDIO, NDIO mpaka huna udhubutu wa kusema HAPANA. Mara nyingine NDIO unazosema ni za unafiki tu, hukubaliani nazo ila unasema ili kumfurahisha unayemwambia au usionekane wewe ni mbaya au mkwamishaji.

  Kwa utaratibu huo wa kusema NDIO mara nyingi na kwa watu wengi ni vigumu sana kufikia malengo na mipango yako. Kwa sababu kwenye kila unachofanya kuna mtu(tena wa karibu) atakuja na wazo jipya. Unaposema NDIO kwenye wazo hilo jipya unaanza kutekeleza mipango ya mtu mwingine na kusahau ya kwako. Kwenye kila jambo kubwa unalofanya kuna watu wako wa karibu watakaokuambia huwezi ama utashindwa. Ukiwaambia NDIO unaacha mipango yako na unabaki ukitangatanga tu usijue ni lipi la kufanya.

  Anza sasa kujifunza kusema HAPANA.

Sema HAPANA kwa wazo lolote jipya unalopewa ambalo haliendani ama litakwamisha malengo yako.

Sema HAPANA kwa mtu yeyote anayekushawishi kurudi kwenye tabia uliyoamua kuiacha.

Sema hapana kwa mtu yeyote anayekuondoa kwenye mipango yako ili mkafanye mambo ambayo hayana msaada mkubwa kwako.

Sema hapana kwa mtu yeyote anayekukatisha tamaa na kukuambia kwamba huwezi kufikia malengo yako makubwa.

Sema hapana kubwa kwa jambo ama mtu yeyote ambae atakuwa kikwazo kwako kufikia malengo yako. Naposema mtu yeyote namaanisha mtu yeyote kweli na usilete unafiki kwa kufikiri watu fulani wanahitaji sana NDIO yako.

  Utakapoanza kusema HAPANA wengi watakulaumu na kukuona wewe ni mbaya. Ila kama utawapa sababu ya msingi watakuelewa na hata wasipokuelewa sasa watakuelewa baadae. Utakapoanza kusema HAPANA watu wataanza kujenga nidhamu kwako na kuna baadhi ya mambo wataacha kukuambia kwa sababu wanajua huendani nayo.

  Punguza unafiki kwenye maisha yako, fikiri kuhusu malengo na mipango yako zaidi na sema HAPANA kwa jambo lolote ambalo halina msaada kwenye malengo na maisha yako.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s