Mtandao huu wa AMKA MTANZANIA tarehe 31/03/2014 unatimiza mwaka mmoja tokea uanzishwe tarehe 31/03/2013. Ndani ya mwaka huu mmoja Mtandao huu umepitia mengi sana. Mtandao ulianza na wasomaji wachache sana ambao walikuwa hawazidi 50 kwa siku. Lakini kutokana na kutokata tamaa mtandao umekuwa unakua kidogo kidogo kila siku mpaka sasa umefikia zaidi ya wasomaji 1000 kwa siku.

tz

Kwa nini AMKA MTANZANIA?

Katika makala zote nilizoandika kwenye mtandao huu hakuna hata moja ambayo nimewahi kuandika kwa nini niliuita mtandao huu AMKA MTANZANIA. Japo watu wengi niliowahi kukutana nao wamekuwa wakiniuliza kwa nini nilitumia jina hilo.

Ukweli ni kwamba Watanzania tumelala, na kulala kwetu kunawafaidisha watu wachache huku wengi tukiendelea kuumia. Watanzania tunaendelea kufanya mambo ambayo yameshapitwa na wakati duniani na hivyo tunateseka sana ila mafanikio hatupati. Haya ni baadhi ya mambo ambayo watanzania wengi tunafanya na yanagharimu maisha yetu.

1. Watanzania wengi tumekata tamaa na maisha yetu. Hatuoni kama tunao uwezo wa kubadili maisha yetu kuwa bora zaidi ya yalivyo sasa.

2. Watanzania tunafanya kazi na biashara zetu kwa mazoea. Watu wengi watakwenda kwenye shughuli zao kesho kwa sababu tu leo na jana walikwenda.

3. Watanzania tunafikiri kuna mtu wa kuja kututoa hapa tulipo. Tumedanganywa na kuwaamini sana wanasiasa tukifikiri kwamba kama mtu fulani au chama fulani kitachaguliwa basi maisha yatakuwa bora sana, kitu ambacho hakiwezi kutokea.

4. Tunafanya mambo mengi kwa kuiga. Asilimia kubwa ya watanzania tunafanya mambo kwa sababu tu wanaotuzunguka wanafanya.

5. Hatufurahii kazi au biashara tunazofanya ndio maana inakuwa vigumu kufanikiwa.

6. Hatupendi kujifunza mambo mapya ambayo yatatuendeleza katika kazi zetu na biashara zetu.

7. Tunapenda kulalamika sana hivyo tunashindwa kuchukua hatua juu ya maisha yetu.

8. Tunatafuta njia za mkato za kufikia mafanikio, hivyo tunaishia kuwa wezi, mafisadi na hata matapeli.

9. Hatuna malengo na mipango mikubwa kwenye maisha yetu.

10. Tunapoteza muda wetu mwingi kufanya mambo ambayo hayana msaada kwenye maisha yetu.

Yapo mambo mengi yanayoturudisha nyuma watanzania ila hayo kumi ndio ambayo yanafanywa angalau na kila mtanzania. Hapo ulipo sasa hivi unafanya mambo zaidi ya matano kati ya hayo niliyotaja hapo juu. Kwa kufanya mambo hayo huwezi kufikia mafanikio ambayo unayatazamia.

Hata mimi mwenyewe nilkuwa nafanya mambo hayo yote ila baadae nikagundua siwezi kubadili maisha yangu kwa kuwa na fikra hizo. Hivyo nilianza kubadili moja baada ya nyingine na kuona mabadiliko makubwa kwenye maisha yangu. Japo sijaweza kuacha yote hayo ila kwa asilimia tisini nimeweza kuacha kufanya mambo hayo.

Baada ya kuona mabadiliko makubwa kwenye maisha yangu kwa kubadili mambo hayo niliona ni vyema kuwashirikisha watanzania wenzangu njia ninazopitia na mabadiliko ninayofanya na kuwashauri nao wayafanye. Hapa ndipo ilipozaliwa AMKA MTANZANIA kwa lengo moja la kuwaondoa watanzania kwenye mawazo hayo ambayo ni sawa na usingizi.

100_7563 ED

  Watu wengi mmekuwa mkiniandikia kushukuru jinsi makala mbalimbali zilivyoweza kuyabadili maisha yenu. Nafarijika sana na mrejesho huu ninaoupata kutoka kwenu na unanipa moyo wa kuendelea kuwaandikia ili kuendelea kuboresha maisha yetu sote.

  Kwa sentensi moja naweza kusema kwamba wewe pekee ndiye unayeweza kuboresha maisha yako na kufikia mafanikio makubwa, hakuna mtu yeyote duniani anayeweza kuja kukutoa hapo ulipo bila ya wewe kuwa tayari kuondoka hapo.

  Naomba tuendelee kuwa pamoja kwenye safari hii ya kuboresha maisha yetu. Kumbuka mimi na wewe tupo safari moja ya kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu, hatujafika pale ila nakuhakikishia lazima tutafika kama tutaendelea kuwa pamoja. Ninao ushahidi wa kutosha wa jinsi gani mambo ninayokuandikia yameweza kuboresha maisha yangu na kufikia malengo ambayo yalikuwa ndoto za mchana kwa watu wengine.

  Tafadhali tushirikishe kwenye maoni hapo chini ni jinsi gani mtandao huu umekuwa na manufaa kwenye maisha yako. Kama huna lolote la kutushirikisha tafadhali andika IDUMU AMKA MTANZANIA kuonesha kwamba ungependa mtandao huu uendelee kuwepo. Tafadhali sana usiache kusema chochote.

  Asante sana kwa kuendelea kuwa nami, twende pamoja ili tuweze kuboresha maisha yetu.

  Tuko pamoja.

Makirita Amani,

amakirita@gmail.com

0717396253