Acha Kufanya Kosa Hili Kubwa Linalogharimu Maisha Yako.

Ni mara ngapi umewahi kuangalia watu ambao mmekua pamoja au mmesoma pamoja na kuona wao wamefanikiwa sana kwenye maisha kuliko wewe?

  Unakutana na rafiki yako ambae mlipotezana miaka mitano au hata kumi iliyopita. Katika kuzungumza kuhusu maisha anakwambia yeye ana kazi au biashara inayolipa sana, ana nyumba mbili, magari matatu na mashamba. Ukijifikiria wewe huna kazi au biashara ya kueleweka, bado unaishi kwenye nyumba ya kupanga na usafiri wako ni daladala. Unajisikiaje baada ya kupata picha hii ya mwenzako?

  Mbaya zaidi unakuta mtu huyo mlikuwa mnafaulu sawa darasani na hata wakati mwingine ulikuwa unafaulu zaidi yake. Unapata hasira na kujiona wewe umeshapoteza maisha! Hiki ndicho kinachotokea kwa watu wengi.

usijilinganishe

  Kosa kubwa unalofanya kwenye maisha yako kila siku ni kujilinganisha na wengine, kosa hili ni baya sana na linakugharimu sana kwenye maisha yako. Unaweza kusema kujilinganisha na wengine kunakupa wivu wa maendeleo au kunakufanya ukazane zaidi, huo sio ukweli hata kidogo. Kujilinganisha na wengine na hasa pale wanapokuwa wamefanikiwa kushinda wewe ndio unazidi kujirudisha nyuma. Unajisikia vibaya sana kuona mtu uliecheza nae utotoni ana mafanikio mara mia ya uliyonayo wewe. Hapa ndipo unapoanza kuona labda wewe una kisirani na yeye ana bahati au alibebwa.

Kila mtu ni wa pekee

Dunia ina watu zaidi ya bilioni saba, lakini kati ya watu hao hakuna watu wawili wanaofanana kwa kila kitu, hata mapacha hawana ufanano wa asilimia 100. Wewe ni wa pekee, una uwezo mkubwa na vipaji vya kipekee. Hakuna mtu yeyote duniani anayeweza kufanya vitu fulani kama unavyoweza kufanya wewe. (soma; wewe ni wa pekee)

  Pamoja na kwamba kila mtu ni wa pekee, tumetengenezwa kuamini kwamba wote tuko sawa na mwishowe tunaamini inabidi tufanikiwe kwa usawa.

  Unakwenda shule ya chekechea na wenzako, baadae mnakwenda shule ya msingi, baadae wachache mnaendelea na sekondari mpaka hata vyuo mbalimbali. Katika wakati wote huu unafikiri wote mko sawa, mna malengo sawa ya kufaulu na kuwa na maisha mazuri. Ila baada ya kila mtu kutawanyika ndipo mambo yanapoanza kuwa mazuri.

Kila mtu anasafiri kwenye njia yake binafsi.

Tatizo la kujilinganisha linaanza pale unapofikiri mlikuwa kwenye niia moja ya safari kwa sababu mlianza pamoja. Hapa ndipo unapochelewa na kuachwa nyuma. Kila mtu anasafiri kwenye njia yake binafsi. Kuna ambao watafanya kazi na kufanikiwa sana, kuna ambao watafanya biashara na kufanikiwa mno. Pia kuna wengine watafanya kazi za utumishi na kuwa na maisha mazuri sana. Unapojaribu kujilinganisha na watu hawa ambao wako kwenye njia tofauti hujitendei haki wewe mwenyewe.

  Kama hujafanikiwa kama wenzako walivyofanikiwa huenda hujajua ni kitu gani unachofanya kwenye maisha yako. Huenda hujajua ni kitu gani cha kipekee unachoweza kufanya na ukafanikiwa sana. Na kwa asilimia kubwa huenda unaiga maisha ya watu wengine.

Jilinganishe na wewe mwenyewe.

  Badala ya kujilinganisha na wenzako ambao wanaonekana wamefanikiwa kuliko wewe na kuanza kujisikia vibaya hebu anza kujilinganisha na wewe mwenyewe. Jiulize hicho unachofanya kwenye maisha yako je unakifurahia? Kumbuka ni vigumu sana kufanikiwa kama unafanya kitu ambacho hukipendi(soma; kama unataka kufanikiwa usifanye kazi )

  Jiulize ni vipaji gani ulivyonavyo, jua ya kwamba una uwezo mkubwa na ubunifu wa hali ya juu. Vijue na kutumia vitu hivi ili kuboresha maisha yako. Kama mpaka sasa hujajua vipaji vyako soma; jinsi ya kugundua vipaji vilivyopo ndani yako.

  Shindana na wewe mwenyewe, hakikisha kila siku mpya unakuwa bora zaidi ya siku iliyopita. Unapomaliza siku ya leo hakikisha umefanya vitu unavyofanya kwa ubora zaidi ya ulivyofanya jana. Kwa njia hii utajikuta ufanisi wako unaongezeka kila siku na mwishowe unapata mafanikio makubwa. Kama unafanya vitu kwa mazoea tayari upo nje ya njia ya kuelekea kwenye mafanikio. Kama sababu pekee inayokufanya uende kwenye shughuli zako leo ni kwa sababu jana ulienda upo kwenye hatari kubwa.

  Hakikisha kila siku una kitu cha kuongeza kwenye ujuzi na ufanisi wako wa kazi. Hakikisha kila siku kuna kitu kipya unajifunza ambacho kitakusaidia kwenye maisha yako.

Asikudanganye mtu yeyote kwamba wewe umeshapotezwa kwenye maisha. Huenda hujajua ni nini kinafanya kazi kwenye maisha yako. Karibu twende pamoja kwenye safari hii ya kubadili maisha na uwe na maisha bora kulingana na uwezo wako mkubwa. Kwa mengi zaidi jiunge na kisima cha maarifa. Kama bado hujajiunga na kisima hiki bonyeza maandishi haya kupata maelezo ya kisima.

Kila la kheri katika harakati zako za maisha, tuko pamoja.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: