Maisha ya kila binadamu ni tofauti sana na ya watu wengine. Kuna watu wanaishi kwa furaha sana na kuna watu wanaishi kwa huzuni na manung’uniko sana. Kuna watu wanaonekana kuwa na mafanikio sana na kuna watu wanaonekana kushindwa kupata mafanikio licha ya juhudi kubwa wanazofanya maishani.

  Kama wewe upo upande mbaya wa maisha ambapo kila unalofanya hufikii mafanikio, kila siku unakwazika na kuvunjika moyo kutokana na mambo yanayotokea basi upo gerezani. Kuna gereza kuu la maisha yako ambapo maisha yako yamefungwa. Huwezi kujua maisha yako yamefungwa gerezani kama hujajua gereza hilo.

          GEREZA

  Gereza kubwa kwenye maisha yako ni akili yako, mawazo yako na mtazamo wako kwenye maisha. Kwa ujumla tunaweza kusema mtazamo wako kuhusu maisha ndio unaochangia kwa kiasi kikubwa sana aina ya maisha unayoishi. Kama una mtazamo hasi kuhusu maisha basi jambo lolote litakalotokea utaliona ni hasi na kuangalia zaidi ubaya wake kuliko uzuri. Kama una mtazamo chanya kuhusu maisha basi jambo lolote litakalo tokea utachukulia kama sehemu ya kujifunza na utaangalia zaidi uzuri kuliko ubaya wa jambo husika.

  Ni rahisi hivyo lakini bado wengi wetu tuko kwenye gereza hili kubwa. Tumezifunga fikra zetu na hatutaki kufikiria zaidi ya tunavyoamini au tunavyoaminishwa. Huwezi kuwa huru kama huna uhuru wa fikra.

  Kile unachofikiri kwa muda mrefu ndicho kinachotokea kwenye maisha yako. Kama unafikiri mikosi, visirani na kushindwa kila mara basi katika jambo lolote utakalofanya hayo ndio majibu utakayopata. Kama unafikiri kufanikiwa na kujifunza kila mara basi katika jambo lolote utakalofanya lazima utafanikiwa. Na hata usipofanikiwa bado hutoumia kwa sababu utachukua kama sehemu ya kujifunza hivyo wakati mwingine itakuwa rahisi zaidi kufanikiwa.

SEMINA

 

Kuna kauli watu wengi wanapenda kuitumia inasema “mchawi wa mtu ni mtu mwenyewe”, yaani mchawi wako ni wewe mwenyewe. Usihangaike kutafuta anayekuloga na kusababisha mambo yako yaende hovyo. Wewe mwenyewe ndiye unayekwamisha mambo yako kwa sababu ya mawazo uliyojaza kwenye akili yako.

  Unaweza kutoka kwenye gereza lako leo hii kwa kubadili mtazamo wako juu yako, juu ya maisha na juu ya watu wengine. Ukiwa na mtazamo chanya kila kitu kitakwenda vizuri na utayafurahia maisha. Ukiwa na mtazamo hasi kila kitu kitakwenda hovyo na utakuwa na msongo wa mawazo kila siku.

  Acha kuteseka kwa kujifungia kwenye hilo gereza lako. Ondoka sasa kwenye gereza hilo na uanze kuyafurahia maisha.

“Badili mtazamo wako, badili maisha yako”.