Mteja anapotoa hela kwa ajili ya kununua biashara yako au kulipia huduma yako ina maana kwamba kuna thamani kubwa ya kiuchumi ameiona kwenye bidhaa hiyo ambayo inazidi umuhimu wa hela anayotoa. Hakuna mtu anayependa kupoteza fedha zake hasa pale ambapo zimepatikana kwa shida. Hivyo mpaka mteja achukue hatua ya kukupa fedha zake ni lazima kuwe na thamani kubwa ambayo anaamini ataipata.
Wewe kama mfanya biashara ni vyema ukajua biashara yako inatoa thamani gani ambayo itamshawishi mteja wako kutoa fedha zake mfukoni na kukupa. Kwa kujua thamani hiyo na kuiboresha kila mara ni njia nzuri sana ya wewe kukuza biashara yako.
Kila mtu ana aina yake ya thamani, ila kuna aina tisa za thamani ambazo hutokea kwa watu wengi wakati wanafanya uamuzi wa kununua bidhaa au huduma. Aina hizo ni;
1. Ubora.
Ni kwa kiwango gani bidhaa au huduma yako inaweza kufanya kazi kwa ubora? Wateja wako tayari kulipia bidhaa ambayo ni borea na inafanya kazi vizuri. Kama ubora ni tatizo ni vigumu sana kupata wateja wa kudumu.
2. Kasi.
Ni kwa kasi kubwa kiasi gani bidhaa au huduma yako inaweza kumsaidia mteja? Huu ni wakati ambao kila mtu anataka jambo la haraka, hakuna mtu anayetaka kusubiri mda mrefu ndio aone matokeo. Kama biashara yako inaweza kutatua tatizo la mteja kwa haraka ndivyo thamani yake inavyozidi kuwa kubwa. Kwa mfano; usafiri wa ndege ni gharama kubwa sana kushinda usafiri mwingine kwa sababu ya kasi yake ya kufika unakoelekea.
3. Utegemezi.
Je mteja anaweza akategemea bidhaa au huduma yako kutatua tatizo lako? Watu wako tayari kulipia huduma ambayo wana uhakika wanaweza kuitegemea kwa kiwango kikubwa. Hakuna mtu anapenda alipe fedha leo halafu baada ya siku chache bidhaa au huduma iwe haifanyi kazi kama walivyotegemea.
4. Urahisi wa kutumia.
Ni rahisi kiasi gani kwa mteja kutumia bidhaa au huduma yako? Hakuna mtu aliye tayari kupoteza muda mwingi kwa ajili ya kujifunza jinsi ya kutumia bidhaa au huduma fulani. Hakikisha bidhaa au huduma yako ni rahisi kwa mteja kutumia ili kutatua matatizo yake.
5. Urahisi wa kubadilika.
Ni vitu gani vya ziada ambavyo bidhaa au huduma unayotoa vinaweza kufanya? Kama kitu kinaweza kuwa na matumizi zaidi ya moja ndivyo thamani yake inavyozidi kuwa kubwa na wateja wanakuwa tayari kulipia.
6. Ufahari.
Ni jinsi gani watu watamchukulia mtu ambaye anatumia bidhaa au huduma yako? Kama bidhaa au huduma yako inamfanya mtu aonekane ni wa daraja la juu thamani yake inazidi kuwa kubwa. Kwa mfano simu aina ya Iphone, mtu anayeitumia anaonekana ni wa daraja la juu, hivyo japo matumizi yake sio tofauti sana na simu nyingine, bei yake ni kubwa sana. Mfano mwingine bei ya thahabu huwa inaongezeka kila muda kutokana na fahari mtu anayoipata kwa kuvaa vito vya thamani.
7. Mvuto.
Ni kwa kiasi gani bidhaa au huduma yako ina mvuto kwa mteja? Kuna kitu fulani kwenye bidhaa au huduma yako kinaweza kuwa kinawavutia sana wateja. Jinsi ambavyo biashara ina mvuto kwa wateja ndivyo ambavyo thamani yake inakuwa kubwa.
8. Hisia.
Bidhaa au huduma yako inamfanya mtu ajisikieje? Kama bidhaa au huduma yako inamfanya mtu awe na hisia nzuri juu yake mwenyewe thamani yake inakuwa kubwa zaidi.
9. Gharama.
Ni gharama kiasi gani mteja analipia ili kupata bidhaa au huduma yako? Baada ya kuangalia baadhi ya thamani hizo hapo juu, mwishowe mteja anakuja kuangalia bei ya huduma au bidhaa husika. Kama ina thamani kubwa kwake atakuwa tayari kulipia gharama za bei na kuipata. Kama haina thamani kubwa kwake ni vigumu sana kwa yeye kutoa fedha yake aliypipata kwa shida. Hivyo kama unaona bidhaa au huduma yako haina thamani kubwa ya kumfanya mtu akimbilie kuilipia tumia njia hii ya mwishoa ambayo ni kuweka bei ndogo. Jinsi bei inavyokuwa ndogo ndivyo wateja wanavyoweza kununua wakiamini kwamba hata kama hawatapata thamani kidogo waliyolipia watakuwa hawajapoteza sana.
Tumia aina hizo tisha za thamani ya kiuchumi wakati unaandaa bidhaa au huduma zako. Angalia jinsi unavyoweza kuongeza baadhi ya thamani hizo ili kuweza kukuza biashara yako.
Nakutakia kila la kheri.