Leo ni siku ya ijumaa kuu, na jumatatu ni siku ya pili ya pasaka. Siku hizi mbili ni za mapumziko hivyo ukiunganisha na jumamosi na jumapili unapata siku nne za mapumziko zilizofuatana.
Asilimia kubwa ya watu wanapumzika katika siku hizi nne. Je wewe unafanya nini kwenye siku hizi nne? Utakuwa unaendelea na kazi zako au utakuwa mapumzikoni?
Watu wengi wameshapanga jinsi ya kuzitumia siku hizi nne. Kuna ambao wamepanga kusafiri kidogo kuona ndugu na jamaa. Kuna wengine wamepanga kufanya starehe za kutosha katika kipindi hiki. Kuna wengine watakwenda kusali na kuweka ukaribu wao na muumba wao. Na kuna wengine hawajui hata watafanya nini kwenye siku hizi nne.
Hawa ambao hawajui watafanya nini wanaweza kulala tu au kufanya au kwenda kokote watakaposhawishiwa na watu wao wa karibu.
Bila ya kujali mipango yako ndani ya siku hizi nne nakuomba ufanye jambo moja ambalo hujawahi kulifanya. Kwa kufanya jambo hilo unaweza ukayabadilisha maisha yako kwa kiasi kikubwa sana. Nakuomba ndani ya siku hizi nne usome kitabu kimoja tu na uanze kuyatumia yale unayoyasoma kwenye kitabu hicho ili kuboresha maisha yako. Ninaposema siku nne simaanishi utatumia siku zote nne, bali tenga masaa mawili kila siku, saa moja asubuhi na saa nyingine moja jioni.![]()
Nimekuwa nikiwatumia wasomaji vitabu mara kwa mara ila nina uhakika ni wachache sana ambao wamekuwa wakimaliza kusoma vitabu hivi. Ndio maana nimekuomba utumie siku hizi nne kusoma kitabu kimoja ambacho nitakutumia.
Leo nakutumia kitabu kinachoitwa The Power of Self Confidence kilichoandikwa na Brian Tracy. Kama jina linavyojieleza utajifunza umuhimu na nguvu ya kujiamini mwenyewe. Ni ukweli usiopingika kwamba mafanikio yanaanzia na kujiamini wewe mwenyewe. Kama hujiamini ni vigumu sana kupambana na kuchukua fursa mbalimbali zinazokuzunguka.
Katika kitabu hiki Brian Tracy ameelezea vitu muhimu unavyotakiwa kufanya ili kujijengea kujiamini na kuondokana na hofu. Kitabu hiki kina kurasa 91, ila ukiondoa za utangulizi na za mwisho unabaki na kurasa 60 zenye mafunzo haya. Kwa hiyo kama utakisoma ndani ya siku nne ina maana kwa siku moja unatakiwa kusoma kurasa 15. Kama ukitenga masaa mawili tu kwa siku yanakutosha kusoma kurasa hizo 15 na ukazielewa vizuri.
Kupata kitabu hichi bonyeza maandishi haya ya jina la kitabu na utaanza kukidownload. The Power Of Self Confidence by Brian Tracy.
Kisome kitabu hiki na kama utakimaliza, jumatatu jioni au jumanne niandikie email(amakirita@gmail.com) kuniambia kwamba umekimaliza kisha nitakupa zawadi nzuri sana.
Nakutakia kila la kheri katika harakati zako.
Kumbuka TUKO PAMOJA.
Tumia Siku Hizi Nne Kubadili Maisha Yako; Jinsi ya Kujijengea kujiamini na ujasiri.