Makala hii imeandikwa na Meshack Maganga, unaweza kuwasiliana nae kupitia mawasiliano yake yaliyopo mwisho wa makala.

 

Mwaka uliopita niliandika makala kuhusu wasomi kujifunza kujiajiri nilikusudia kuwasilisha ujumbe mmoja ya kwamba, “Wasomi na watanzania kwa ujumla wetu tunatakiwa kubadilisha mitazamo yetu ili kujipatia mipenyo ya kiuchumi na kifedha (financial freedom.

Kimsingi ni kwamba zipo imani zinazosapoti watu kuwa na fedha za kutosha na zipo imani na mitazamo inayozuia watu kuwa na fedha ama inawafanya waishi maisha ya kupungukiwa nyakati zote! Imani na mitazamo hii kimsingi huzalishwa kutokana na malezi, utamaduni na mazingira. Mtazamo wa mtu kuhusu fedha tunaita, “Money blue print” .

Nafahamu kuwa wengi kama sio wote tunakubaliana kuwa fedha zina umuhimu mkubwa sana katika maisha ya mtu, na kwamba ukosefu wa fedha ndio msingi wa maovu(Ingawa wapo watu wanatumia fedha kufanya uovu wao) tunachotofautiana ni imani kuhusu fedha. Mitazamo kuhusu fedha ndio inayoamua kiwango cha fedha alichonacho kila mmoja. Hii ina maana kuwa kila mtu anamiliki kiwango cha pesa sawa sawa na imani ama mtazamo wake kuhusu fedha.

vitunguu

Miaka michache iliyopita wakulima walikuwa ni watu wanaotazamwa kama watu wenye shida, walio jitokeza kuwekeza kwenye kilimo walionekana wameshindwa shule ( waliokimbia umande). Na hii ilisababishwa na imani ama mapokeo ya tuliyolishwa na wazazi wetu na walimu wetu kutoka kwenye kipindi cha zama za viwanda (Industria Age). Lakini kwa sasa dunia imebadilika sana, kilimo kimewafikisha watu kwenye ndoto zao, Nimesoma kwenye jarida la Forbes kwamba tajiri wa kwanza Afrika amewekeza kwenye kilimo, wajarisiamali wakubwa hapa Tanzania wamewekeza kwenye kilimo, na wale wanaojiona wameenda shule ‘middle class’ wanaendelea kushangaa na kuendelea kuongea sentensi hasi na kulalamikia viwango vidogo vya mishahara.

  Miaka ya hivi karibuni kwenye Mikoa ya Arusha, Manyara, Iringa, Mbeya,Tanga, Singida na Kilimanjaro zao la vitunguu limejizolea umaarufu mkubwa kwa kuendelea kuajiri maelfu ya Watanzania. Kuna ambao wamefikia ndoto zao kupitia kilomo cha vitunguu, wamejenga nyumba, wamefungua makampuni yao, wanasomesha watoto nk. Vitunguu hivi hivi kuna rafiki zangu wamenunua magari ya ndoto zao, wamejipa likizo nchi za nje.

Nitaongelea hasa eneo la Mahenge sehemu ninayolima mimi. Hali ya hewa na maji ni vipengele muhimu sana vya kuzingatia katika uzalishaji wa zao la vitunguu.Vitunguu vinastawi vizuri katika hali ya ukavu kwa kutumia umwagiliaji.(Local Irrigation) Maji mengi hasa wakati wa masika husababisha magonjwa mengi hasa ukungu, vitunguu haviwezi kukomaa vizuri, hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mazao.

Aina ya mbegu tunayolima sisi pale Mahenge ni pamoja na Mang’ola (traditional) red, Red creole na Bombay Red. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mazao mengi kuanzia magunia 70- 90 kwa hekta ikiwa kilimo bora kitazingatiwa na iwapo mkulima atakuwa anaongozwa na malengo yake na hamasa ya ndani (self drive). Mkulima anaweza kuchagua mbegu kwa kuzingatia, soko, msimu wa kupanda nk. Wasambazaji wa mbegu ni pamoja na maduka ya TFA, na maduka ya bembejeo za kilimo katika maduka mbalimbali. Ingawa wapo baadhi ya watu hasa maeneo ya Ilula –Iringa ambao huandaa wenyewe mbegu kwa kutumia maua ya vingunguu.

  Uandaaji wa kitalu hutegemea sehemu husika, lakini kwa kifupi Sehemu ya kitalu iwe wazi, mbali na kivuli na kiwe karibu na chanzo cha maji na huchukua takribani wiki tano mpaka sita kabla ya kupelekwa kwenye shamba husika. Zipo changamoto mbalimbali ambazo hujitokeza kwenye maandalizi ya kitalu mpaka shambani, changamoto hizo ni pamoja na wadudu, ugonjwa wa ukungu, Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa wekundu ambao wanashambulia majani, na wadudu waitwao Sota ambao hukata miche. Ili kudhibiti tatizo, shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, mkulima – mjasirimali ana shauriwa kuchukua hatua za kuzuia kabla uharibifu mkubwa haujatokea ambao husabaisha wakulima wapya kukata tama na kurudi kule kule kwenye kuilamikia serikali kwamba haiwajali.

  Baada ya maandalizi ya kitalu na mbengu kupelekwa shambani, hatua inayofatia ni ufatiliaji wa malakwamala kwa kupulizia dawa na palizi. Iwapo mkulima yupo mbali na eneo husika, kwa mfano yupo Mwanza, Dar, Moshi ama popote Duniani, mkulima atalazimika kuajiri vijana ambao watamfanyia kazi kwa malipo mpaka vitunguu vitakapo komaa. Miche ya vitunguu, huota taratibu sana, hivyo miezi ya mwanzoni, miche husongwa sana na magugu. Palizi mbili mpaka tatu zinashauriwa na zinatosha kuweka shamba safi.

  Kabla ya kuanza kuvuna vitunguu mkulima anashauriwa kukagua shamba ili kuhakikisha kuwa vitunguu vimekomaa. Na iwapo upo mbali na shamba lako hakikisha unatembelea shamba lako malakwamala. Dalili ya vitunguu kukomaa ni, majani kunyauka na kuanza kukauka asilimia 80 -100% na majani kukauka. Mpaka sasa hapa Tanzania, vitunguu huvunwa kwa mikono. Mimea inangolewa au kuchimbuliwa kwa kutumia jembe dogo.

  Baada ya kuvuna vitunguu vinaweza kuachwa shambani vikiwa vimefunikwa na majani kukinga jua kwa muda wa siku mbili au tatu kutegemeana na hali ya hewa. Lengo nikuimarisha ngozi(Nyama) ya vitunguu nk. Pia kupunguza unyevu kwenye majani na mashina na kuruhusu sehemu ya chini ya shingo kufunga. Ikiwa usalama ni mdogo, vitunguu vinachambuliwa na kukatwa majani na mizizi na kuanikwa sehemu nyingine. Ukaushaji hutumia wiki mbili kutegemea hali ya eneo.

  Kwa sasa soko la vitunguu lipo juu sana,Watu wa kada mabalimabali wanahusika na ununuzi na uuzaji wa vitunguu wakiwa ni pamoja na: wakulima, wachuuzi, wafanya biashara ndogondogo, wauza jumla, wauza rejareja, wasafirishaji na madalali. Kutoka shambani mpaka sokoni.

  Kama nilivyotangulia kusema hapo juu, hekari moja inaweza kutoa magunia 80-100 kwa sasa maeneo ya Njombe, Iringa, na Kwingineko gunia moja la vitunguu huuzwa kati ya shilingi 130,000/= mpaka laki 150,000/= lakini mkoani Njombe kwa bei ya sasa gunia moja ni shilingi 200,000/= kwa gunia. Ingawa kuna baadhi ya misimu soko hushuka sana mpaka kufikia shilingi laki moja kwa gunia ama elfu 70.(Kumbuka kwamba kutafuta pesa ni sawa na mchezo wa mpira wa miguu kadiri unavyo ucheza ndiyo unavyo kuwa hodari-uchaguzi ni wako) Ukiwa na gunia labda 70 ukaziuza unaweza pata hadi shilingi milioni milioni 9, kwa ekari moja baada ya kuondoa gharama yote. Sasa ukiwa na ekari 5, 6,ama 3 utakuwa na shilingi ngapi? Wakati huo unasubiri mshahara wako. Kaka yangu mimi kwa msimu uliopita alipata magunia 1000, ni utajiri gani huu?

  Kila mtu anayo nafasi sawa (equal channce) ya kuwa na fedha za kutosha kumpa uhuru wa kiuchumi. Pili hakuna raha wala sifa ya kuendelea kuwa masikini, kama unafikiri nisifa ama unajidanganya kuwa masikini watapunguziwa adhabu siku ya mwisho unapoteza muda wako kwa sababu masikini ni mzigo kwa dunia. Masikini na umasikini wake hata awe ni mtakatifu na mwema kiasi gani ni kwamba anaitesa dunia (kwa sababu anahitaji kusaidiwa). Tajiri (ama niseme mwenye fedha za kutosha) hata kama ni mchoyo ama bahiri bado ni msaada kwa dunia (kwa sababu anajisaidia).

  Ninatamani kila mmoja apokee changamoto ya kutamani kuwa na uhuru wa kifedha na kiuchumi kwa kuanza na vitu tunavyo viona ni vidogo kwenye macho yetu ama kuachana na kasumba tuliyopewa shuleni kwamba ukimaliza kusoma lazima usake ajira. Ajira zenyewe hakuna na zilizopo bado ni chache. Na hili linawezekana ikiwa mitazamo na imani za wengi kuhusu fedha zitabadilika na kuwa zinazosapoti badala ya kuvuruga nafasi ya mtu kupata fedha.Kila mtanzania anastahili ushindi wa kifedha. Wengi wetu tumekuwa watu wa kuhangaikia malengo ya wenzetu, kuna watanzania wenzetu wapo tayari kuzungumzia Malengo za timu za ulaya siku nzima, wiki, mwezi na jinsi ya kuhakikisha wanapata ushindi nk, mtu huyohuyo hana ajira, ama ajira aliyonayo mshahara hautoshi.

  Kwa watanzania watakao penda kufanya kilimo hiki ama kile cha miti wanaweza kunitafuta nikawapa maelezo ya kutosha.Nchi hii ina matatizo mawili ya msingi kwenye kipengele cha Ujasiriamali, kuna wanaozifahamu fursa lakini hataki kuziweka wazi, sijuwi wanaogopa nini? Labda wana hofu ama ni wachoyo.Na kuna wale ambao walishazisikia fursa lakini bado wanasema nitaanza kesho na kuna wale wanaosingizia mitaji, umbali nk.

Mawasiliano : meshackmaganga@gmail.com 0713 48 66 36, na Whatsupp.fb ni meshackmaganga.