Wiki hii tuko kwenye zoezi la kujua matumizi ya muda wetu yakoje. Kama tulivyokubaliana ni kwamba tutaandika kwenye karatasi au kijitabu kidogo kila muda tunaotumia kufanya jambo lolote. Yaani utaandika muda ulioanza kufanya na muda ulipomaliza kufanya.

Katika wiki hii fanya hivi bila ya kujilazimisha kurekebisha chochote, endelea kuishi maisha yale uliyokuwa unaishi kila siku. Ukikimbilia kurekebisha wakati huu wa kufuatilia hutojua chanzo halisi na utaishia kurudia makosa yaleyale.

Kama bado unaendelea na zoezi hili nikupongeze kwa sababu unajenga tabia ya kuelekea kwenye mafanikio.

Kama umeamua kuachana nalo kwa sababu moja au nyingine nikusikitikie kwa sababu maisha yako yataendelea kuwa magumu na utamlaumu kila mtu ila hakuna kinachobadilika.

Tunataka tutengeneze mfumo mpya kwenye maisha yako, ila wewe mwenyewe ndio wa kuamua kama unataka kufanikiwa au la. Kama unataka hakuna anayeweza kukuzuia, naweza kukuhakikishia hilo. Na kama hutaki hakuna anayeweza kukulazimisha, hilo liko wazi.

Kama kwa bahati mbaya ulisahau kuendelea na zoezi hili naomba urudi na kukamilisha zoezi hili. Mwisho wa kulifanya ni jumatatu jioni na jumanne tutakuwa na makala nyingine ya kujua muda wetu mwingi unapotelea wapi na ni jinsi gani tunaweza kurekebisha hili.

Nakusihi sana uendelee na zoezi hili kwa sababu najua litakusaidia sana, limenisaidia mimi, limewasaidia wengi na hata wewe litakusaidia sana kuweza kufikia malengo yako na kupata mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kuboresha maisha yako.

Kumbuka TUKO PAMOJA.