Kwa wiki nzima kuanzia jumanne iliyopita nilikushauri unakili muda wa kila kitu unachokifanya unapoanza na unapomaliza. Kuna uwezekano umefanya au pia hukufanya. Kama ulifanya hivyo mpaka sasa utakuwa umeona muda wako mwingi unaupotezea wapi.

Leo tutaangalia ni jinsi gani unaweza kupata masaa mawili ya ziada kila siku. Ninaposema utapata masaa mawili ya ziada simaanishi utakuwa na siku yenye masaa 26, hapana, siku yako itaendelea kuwa na masaa 24 ila yatakuwa na maana zaidi kuliko ilivyokuwa wakati hujajua ni kiasi gani unapoteza muda.

Kwa sasa watanzania wengi tunapoteza muda kwenye mambo yafuatayo, ufuatiliaji wa habari, vipindi vya tv, mitandao na mitandao ya kijamii, kupiga soga na ubishi, ubishani wa kisiasa na michezo na mapumziko au starehe. Kwa namna moja au nyingine unatumia baadhi ya njia hizo kupoteza muda wako wa thamani.

1. Ufuatiliaji wa habari.

Kama siku yako unaianza kwa habari kwa kusikiliza redio au kuangalia tv asubuhi na mapema, unatoka hapo unakwenda kutafuta gazeti unalisoma, unaingia kwenye mitandao kutafuta tena habari na jioni tena unaangalia au kufuatilia habari maisha yako yatakuwa ni ya mhemko. Utajikuta unajazwa habari nyingi na hivyo siku nzima kuitumia kufikiria ni kwa nini mambo fulani yanatokea. Hii inakuzuia wewe kuwa na akili safi ambayo inafikiria jinsi ya kutumia fursa zinazopatikana ili kufikia mafanikio. Fikiria umeamka asubuhi unafungulia habari na kusikia taarifa kuna mtu kamuua mwenzake kinyama, kuna mabilioni ya hela yamepotezwa serikalini na kunaongezeko la bei ya vitu fulani. Siku yako nzima utakuwa ukifikiria mambo haya, ni kwa nini mtu amuue mwenzake kinyama hivyo, ni kwa nini watu waibe fedha serikalini kirahisi hivyo wakati wewe unazitafuta kwa shida na kadhalika, hali hii itakupa hasira na utajikuta hufanyi mambo makubwa kwa siku hiyo. Hiyo ni siku moja sasa fikiri kila siku kuna habari unalishwa na habari hizi zinakufanya ufikiri kwa mtizamo hasi. Na tatizo kubwa la hizi habari ni kwamba sio zote ni za kweli, nyingine zimetengenezwa au kuwekwa chumvi ili ziwasisimue wasikilizaji au wasomaji. Kwa wewe kusisimka wenzako wanafanya biashara.

Ufanye nini? Punguza habari unazozipata hasa muda wa asubuhi wakati unaanza siku yako. Anza siku ukiwa na akili safi uliyopangilia mambo ya kufanya na changamoto za kutatua, baada ya kufanya japo jambo kidogo ndio utafute habari, tena zile ambazo ni za msingi. Ningekushauri pia ufuatilie habari mwisho wa siku, yaani jioni na pia uangalie ni chombo gani unachopata habari zako. Kama kwa njia yoyote ile unasoma magazeti ya udaku nakushauri uache mara moja, hakuna jambo lolote la maana unaweza kujifunza kutoka kwenye vyombo vya habari za udaku. WATU WALIOFANIKIWA HAWAFUATILII HABARI, WANATENGENEZA HABARI. Jiulize kama unataka kuendelea kufuatilia habari au kutengeneza habari, baada ya hapo chukua hatua.

2. Kuangalia vipindi vya tv.

Kwa hili naomba nisizunguke sana, kama unaangalia zaidi ya saa moja ya vipindi vya tv kwa siku, huwezi kufanikiwa. Ndio namaanisha saa moja, najua kwa wastani watanzania ambao wana tv majumbani kwao wanaangalia masaa matatu kwa siku, wanaangalia habari masaa kama mawili, wanaangalia tamthilia kama saa moja na wanaangalia tena vipindi fulani wanavyofuatilia. Kama unataka kufanikiwa punguza huu muda ambao unapoteza kwenye kuangalia tv, weka muda usiozidi saa moja kwa siku kuangalia tv na chagua vipindi vichache kwa wiki ambavyo utakuwa unafuatilia, na tamthilia acha kabisa kufuatilia maana hizi zinakupoteza zaidi. Asilimia 90 ya vipindi unavyofuatilia kwenye tv havina msaada wowote kwako. Kuna siku nilifika nyumbani nikakuta watu wanaangalia kipindi fulani cha Wema Sepetu kupitia EATV, alikuwa akionesha mbwa wake aliezaa, nikajiuliza kwa mshangao sana ina maana watanzania ndio wanachotaka hiki? Kuona mbwa aliyezaa? Nilisikitishwa sana. Wakati mwingine unapoangalia tamthilia kwenye tv jua jambo hili moja, kuna pande mbili za kioo cha tv kuna upande wa nyuma ambapo waigizaji wanaishi maisha yao na wanalipwa na kuna upande wako ambapo unafuatilia maisha ya kuiga na unalipa na kupoteza muda. Je unataka kuendelea kuwa mtu wa kufuatilia maisha ya kuigiza? Hapana, hiki sio kiwango chako wewe ambaye unataka kufikia mafanikio makubwa. Kama unakaa nyumbani sijakushauri ukataze kila mtu kuangalia tv, unaweza kuwashauri waache, kama ni watu wazima ila kama wanaendelea nakupa ushauri mmoja mzuri, wakati wowote mtu anapowasha tv kuangalia nenda sehemu iliyotulia na usome kitabu halafu mwisho wa siku utaona ni nani atakuwa amefaidika zaidi.

3. Mitandao na mitandao ya kijamii.

Hili ndio kaburi la kuchimbia muda kwa sasa, na ni tatizo la dunia nzima. Mitandao ya kijamii imekuwa na utegemezi mkubwa sana kiasi kwamba watu hawafikirii tena mambo ya msingi. Watu hawakai chini wakala chakula wakakifurahia ila wanakimbilia kukipiga picha na kuweka facebook, watu hawafikirii jinsi ya kutatua matatizo yao wanayaanika facebook. Facebook na mitandao mingine ya kijamii imekuwa kelele sana kwa watu wa zama hizi. Na urahisi wa kupata smartphone ambazo unaweza kuingia kwenye mtandao kwa urahisi zaidi ndio unamaliza watu kabisa. Kama hutengenezi fedha, yaani hutumii facebook kama njia ya biashara nakushauri usitumie zaidi ya nusu saa kwa siku kwenye facebook. Kwa vyovyote vile usianze siku yako na facebook, labda uwe umeamua kuizika siku hiyo. Ubaya wa mitandao ya kijamii ni kwamba ukishaingia tu kuchomoka inakuwa ngumu kwa sababu unakuwa unaona kama kuna vitu fulani vinakupita. Sasa hebu fikiria ni vitu gani vinakupita? Picha ya rafiki yako ambae hata hujawahi kuonana naye aliyopiga akinywa chai? Malalamiko ya marafiki zako kwenye mtandao kwamba maisha ni magumu? Kama una malengo ya kufikia mafanikio makubwa haya ni matumizi mabovu sana ya muda wako. Unaweza kuingia na kuchungulia facebook kidogo kwa siku kwenye muda wako wa mapumziko, ila hakikisha hazizidi dakika kumi, la sivyo utajikuta unashituka baada ya saa moja.

Mitandao kwa ujumla imejaa habari nzuri sana za kujifunza, ila pia imejaa kelele nyingi sana za kukupoteza. Hujawahi kujikuta umeenda google kutafuta kitu fulani na kuishia kusoma habari ambazo hukupanga kuzisoma? Hii inatokea kila mara kwa sababu ya kelele iliyojaa kwenye mitandao. Chagua mitandao sahihi unayoweza kuifuatilia kila siku na kujifunza, mtandao kama AMKA MTANZANIA na hapa kwenye KISIMA unaweza kujifunza mengi sana unapotembelea. Jua ni mitandao ipi ukitembelea unajifunza na ndio uitembelee.

4. Kupiga soga na ubishi, ubishani wa kisiasa na michezo.

Kupiga soga inaweza kuwa kitu kizuri sana kwa sababu kuna taarifa unapata na pia unajumuika, ila kama kupiga huku soga kunakuzuia kufanya mambo yako ya msingi unapoteza muda wako. Kama ukifika tu kazini zinaanza hadithi mara hiki mara kile, hamjakaa sawa mnaanza kupiga hadithi za kufuatilia maisha ya watu, na wakati mwingine umbea, haya ni matumizi mabovu sana ya muda wako. Usitumie hata sekunde yako moja kujadili maisha ya mtu, hujui hata nusu ya maisha yake, unachoona kwa nje ni picha tu na sio uhalisia, kila mtu ana matatizo yake na anajaribu kuyatatua sasa kama wewe umeacha matatizo yako na kuanza kufuatilia ya watu sijui ni nani atakusaidia kutatua matatizo yako.

Ubishani wa siasa na michezo ni kitu ambacho kinapoteza muda wa watu wengi sana. Sikushauri uache kufuatilia siasa, ni muhimu sana kwenye maisha yako, ila kukaa na kuanza kubishana sijui CCM kafanya hiki mara CHADEMA kafanya kile halafu hakuna hatua yoyote unayoweza kuchukua ni kupoteza muda wako. Naona vijana wengi sana wakitumia muda wao kubishana mpaka kufikia hatua ya kuchukiana kwa sababu ya siasa, mwisho wa mabishano kila mtu anarudi kwenye matatizo yake na kuendelea kuteseka. Usipoteze muda wao kubishana siasa, hakuna faida yoyote unayoweza kuipata hapo.

Mabishano ya michezo nayo yanachukua muda wa watu wengi sana. Timu za ulaya, wachezaji wa ulaya na mpira umechezwa ulaya ila kuna watu wanabishana mpaka kufikia hatua ya kutafutana kama vile ni kesi. Fuatilia mchezo unaoupenda ila usiingie kwenye ubishani ambao utakupotezea nguvu zako na kukufanya upate hasira na kushindwa kufuatilia mambo muhimu kwenye maisha yako.

5. Mapumziko au starehe.

Kupumzika ni muhimu sana, hasa baada ya kufanya kazi yenye maana. Swali ni je unapumzikaje? Kuna wengine wanafikiri kupumzika baada ya kazi ngumu ya siku ni kukaa baa na kunywa bia mbili tatu. Inaweza kuwa njia nzuri ya kupumzika kwako ila inaweza kuwa ni njia ya kukuondoa kwenye mstari wa kufikia mafanikio makubwa. Kwa vyovyote vile jitahidi sana usinywe pombe kati kati ya wiki kwa sababu unapolala ukiwa umekunywa pombe, unaamka ukiwa umechoka na unapoamka ukiwa umechoka ni vigumu sana kuianza siku yako ukiwa na shauku kubwa. Makala ijayo tutajifunza mambo ya kufanya asubuhi na mapema ili kuwa na siku bora, itakuwa vigumu sana kuweza kuyafanya kama umelala na pombe. Uzuri ni kwamba pombe haina uteja mkubwa unaweza kuacha au kupunguza wakati wowote unaotaka, ni wewe kuwa na nidhamu na kuwa na kitu kingine cha kufanya badala ya kunywa pombe. Epuka pombe katikati ya wiki na punguza kiwango unachokunywa mwishoni mwa wiki. Hii itakusaidia sana sio tu kwenye kuokoa muda, bali hata kwenye kujenga afya bora na kwenye matumizi mazuri ya fedha zako.

Kama umeshakuwa mnywaji mzoefu anza kwa kupunguza kiwango unachokunywa mpaka ufikie chini kabisa au kuacha.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo unayafanya na yanakupotezea muda wako mwingi na wa thamani, kuna mengi zaidi ya haya ambayo unayajua wewe mwenyewe, angalia ni jinsi gani unaweza kuyatatua ili kuokoa muda wako unaopoteza.

ZOEZI LA WIKI HII.

Wiki hii fanya zoezi moja la kupunguza nusu ya muda unaotumia kwenye mambo yote ambayo hayakusaidii kufikia lengo lako kwenye maisha. Punguza nusu ya muda unaotumia kwenye mitandao ya kijamii, kufuatilia habari na hata kustarehe. Utumie muda huo kujisomea kitabu kizuri ambacho nakupatia hapa kisha tutakijadili kwenye MAJADILIANO ndani ya KISIMA.

Kupata kitabu hiko bonyeza maandishi haya.

Karibu sana, TUKO PAMOJA.