USHAURI; Unawezaje Kuacha Kazi Yenye Maslahi Kidogo Na Kujiajiri?

Mpendwa msomaji wa AMKA MTANZANIA karibu tena kwenye sehemu yetu hii ya ushauri ambapo tunajaribu kushirikishana mawazo ili kuweza kuwasaidia wenzetu kuvuka changamoto kubwa zinazowazuia kufikia malengo yao.

Moja ya changamoto kubwa ambayo watu wamekuwa wakituma ni kuhusu kuacha kazi na kujiajiri. Wengi wanalalamika ajira wanazofanya hazina maslahi na hivyo maisha kuendelea kuwa magumu kwao, ila pia hawana udhubutu wa kuacha kazi hizo na kwenda kujiajiri. Hivyo leo tutaangalia unawezaje kuacha kazi isiyo na maslahi na kwenda kujiajiri?

Naomba nianze na moja ya ujumbe nilioandikiwa na msomaji;

“Nimeajiriwa kwa Muhindi miaka 7 imepita sina chochote cha maana. Nataka kujiajiri lakini nakuwa mwoga kuacha kazi nahisi biashara haitaenda vizuri. Nishauri nifanyeje?”

Kuna jumbe nyingi sana nimepokea kutoka kwa wasomaji zote zikiwa na swali hilo la msingi la jinsi ya kuacha kazi na kwenda kujiajiri.

broke

Tukianza na tatizo la msingi kabisa, kazi yoyote ni utumwa. Ni utumwa sio tu kwa sababu kuna mtu anayekupangia na kukusimamia ufanye kazi bali pia kwa sababu jinsi unavyozidi kuendelea kukaa kwenye kazi ndivyo unavyozidi kuwa mwoga kuondoka kwenye kazi hiyo.

Utumwa huu ndio unawafanya watu kuendelea kung’ang’ania kufanya kazi ambazo hazina maslahi kwao na zinawatesa. Ili kuweza kuacha kazi na kwenda kujiajiri inabidi kwanza kuondoka kwenye utumwa huu, inabidi uweze kuvunja gereza hili na kupata uhuru wako.

Unawezaje kuvunja gereza hili na kupata uhuru wako? Kwanza jua kabisa kwamba ukiacha au kufukuzwa kazi leo sio mwisho wa dunia. Ndio utateseka, lakini hata sasa unateseka. Umejazwa hofu kwamba kama kazi ikisimama leo basi ndio huna tena maisha, huu ni uongo ambao hauwezi kudhibitishwa mahali popote pale.

Hebu fikiria kwa mtu aliyefanya kazi miaka 7 na kuna wengine wamefanya zaidi ya miaka 10 lakini hawana chochote wanachoweza kuonesha kwamba wamekipata kutokana na kazi, kuna kipi kikubwa anachoweza kupoteza kama akiacha kazi?

Kabla hujamuandikia mwajiri wako barua ya kuacha kazi kuna mambo muhimu unatakiwa kuyafanya.

1. Weka mipango ni kitu gani utafanya baada ya kuacha kazi hiyo. Kama ni biashara unatafanya jua ni biashara gani na utafanyia wapi na utaanza na mtaji wa shilingi ngapi. Tengeneza mtaji huo na fedha za ziada za kuishi kabla hujaacha kazi. Hii itakusaidia kuanza biashara yako huku ukiwa angalau una uwezo wa kuendela kuishi.

Kuna mtu anasema kupata huo mtaji na fedha za kuendelea na maisha ndio tatizo. Leo nakuambia sio tatizo ila ni kisingizio ambacho umekuwa ukikitumia ili kuendelea kuwa mtumwa. Tuchukue mfano wa huyu ndugu yetu ambaye amefanya kazi kwa miaka 7, tuseme labda mshahara wake ni tsh laki moja kwa mwezi. Kama ndugu yetu huyu angeanza kwa kuweka pembeni asilimia kumi ya mshahara wake ambayo ni sawa na tsh elfu kumi kwa mwezi, kwa mwaka angeweka pembeni tsh laki moja na elfu ishirini. Kwa miaka saba angekuwa na tsh laki nane na elfu arobaini. Sasa hebu jiulize ni biashara ngapi za wastani anaweza kuanzisha kwa shilingi laki nane? Zipo nyingi sana.

Katika kipato chochote unachopata hakikisha unaweka pembeni asilimia kumi, hii usiitumie kwa njia nyingine yoyote ile. Kama unasema kipato chako ni kidogo na huwezi kuweka pembeni asilimia kumi cha kufanya ni kuongeza kipato, ila asilimia kumi iwe pale pale na usiitumie kwenye matumizi yoyote yale. Kujifunza zaidi kuhusu hii asilimia kumi soma makala; unawalipa watu wote kasoro huyu mmoja wa muhimu.

2. Angalia ni jinsi gani unaweza kuongeza kipato chako kwa sasa wakati unaendelea na kazi. Kwa kuwa changamoto kubwa uliyonayo sasa ni kazi ambayo haitoshelezi hata mahitaji yako ni vyema ukaangalia njia nyingine za kuongeza kipato ukiwa bado kwenye kazi hiyo. Kwa kufanya hivi itakupunguzia muda utakaoendelea kuwa mtumwa. Njia za kuongeza kipato zipo nyingi sana kulingana na kazi unayofanya na mazingira unayoishi. Fungua macho yako na kutafuta utaona.

3. Jua ya kwamba maisha yako yataendela hata kama hiyo kazi haitakuwepo. Hii nimeizungumzia hapo juu kuhusiana na utumwa unaotengenezewa kwenye ajira yako.

4. Tumia muda huu kujifunza kile unachokwenda kufanya. Tatizo letu kubwa watanzania ni kuwa hatupendi kuongeza maarifa. Tukishapata ajira basi tunapumzika na kuona ndio mwisho wa maisha. Hili ni kosa kubwa sana. Dunia inabadilika kwa kasi ya ajabu sana, jifunze mambo mapya kila siku, kama umepanga kuja kufanya biashara anza kujifunza kuhusu biashara. Jifunze njia mbalimbali za kuanzisha biashara, jifunze mbinu za masoko na pia jua ni jinsi gani unaweza kutumia ubunifu kwenye biashara unayotaka kufanya ili kuwa tofauti na wengine wanaofanya biashara hiyo. Kwa kufanya hivi wakati bado uko kwenye ajira itakusaidia kupata ujasiri kwamba inawezekana na unaweza kuacha kazi na kuingia kwenye biashara. Unaweza kujifunza yote haya kwa bure kabisa au kwa gharama kidogo sana. Kwa kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku utajifunza mambo haya mazuri. Kwa kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA utapata maarifa mengi kuhusu biashara na kufikia mafanikio.

Kwa vyovyote vile jenga ujasiri na jua kwamba wewe ndi kiongozi mkuu wa maisha yako. Weka mipango ni lini utaacha kazi, unahitaji nini ili uweze kuacha kazi hiyo na anza kufanyia kazi mipango yako.

Kwenye KISIMA CHA MAARIFA niliandika makala ya mambo kumi muhimu unayotakiwa kujua kabla hujaacha kazi, kapa nitaweka kipande cha makala hiyo na kama utahitaji kuisoma yoyote jiunge na kisima cha maarifa ili upate mengi zaidi. Kujiunga na kisima cha maarifa unatuma tsh elfu kumi pamoja na email yako kwenye namba 0717396253 au 0755953887. Kujiunga ni siku tatu za mwisho wa mwezi, ila leo natoa nafasi kwa ajili ya makala hii, hivyo fanya hima kutumia nafasi hii.

Mambo Kumi Muhimu Unayotakiwa Kujua Kabla Hujaacha Kazi Na Kwenda Kujiajiri.

Kutokana na ugumu wa ajira kwenye zama hizi watu wengi wanaona kujiajiri au kuwa mjasiriamali ndio njia mbadala ya kuyakomboa maisha yao. Hivyo kumekuwa na wimbi kubwa la watu kuondoka kwenye kazi na kwenda kujiajiri au kuanzisha biashara zao. Ni kitu kizuri sana kwa sababu angalau watu wanaweza kuwa na mamlaka na maisha yao na wanaeza wakaajiri na wengine pia. Ila kwa upande wa pili sio wote wanaokwenda njia hiyo wanafanikiwa kufikia malengo waliyojiwekea. Wengi sana wanashindwa na kujikuta wako kwenye mazingira magumu kuliko hata yale waliyokuwa nayo kwenye ajira.

Leo tutazungumzia mambo kumi unayotakiwa kuyajua au kuyafanya kabla hujaacha kazi na kuingia kwenye ujasiriamali au biashara. Sisemi mambo haya ili kukukatisha tamaa na uendelee kuwa mtumwa, ila nayasema ili kukupatia mwanga wa kule unakokwenda ili usije kushangazwa na mambo haya baadae. Mambo hayo kumi ni kama ifuatavyo;

1. Kujiajiri au ujasiriamali ni kugumu.

Kama unafikiri kujiajiri au kuingia kwenye ujasiriamali ndio nJia rahisi kwako kufanikiwa ni vyema ukabadili mawazo yako mara moja kabla hujaingia na ukashindwa vibaya. Zaidi ya nusu ya biashara zinazoanzishwa zinakufa ndani ya mwaka mmoja baada ya kuanzisha. Na hata zile zinazoendelea kudumu zinakuwa na hali ngumu sana na hazitengenezi faida kubwa. Hizi ni takwimu ambazo zinasikitisha sana ila ndio ukweli wenyewe.

Kujiajiri ni kugumu, ujasiriamali ni mgumu na biashara ni ngumu. Jua kabisa unaingia kwenye njia ambayo uwezekano wa kushundwa ni mkubwa hivyo mipango na kufanya kazi kwa bidii na maarifa ni muhimu sana.

2. Utafanya kazi kuliko ulivyokuwa umeajiriwa.

Unafikiri ukishajiajiri wewe ndio bosi mwenyewe unakaa nyuma ya meza kubwa yenye kiti cha kuzunguka huku ukiongea na simu au wageni na wateja waliokutembelea ofisini. Ndoto za mchana hizo. Unaweza kukaa kwenye kiti cha kuzunguka na meza kubwa ila utafanya kazi zaidi ya unavyofanya kwenye ajira. Unaweza kujikuta unafanya kazi masaa kumi na mbili ofisini na ukirudi nyumbani unaendelea tena na kazi kwa zaidi ya masaa mawili. Mwanzo wa biashara au ujasiriamali kuna misingi mingi unayotakiwa kuijenga na ni wewe pekee utakaefanya hivyo.

3. Utavaa kofia nyingi kwa wakati mmoja.

Kwenye ajira yako una jukumu moja tu au machache yaliyoelezwa. Labda unafanya kazi kwenye idara ya masoko, au idara ya uzalishaji au idara ya huduma kwa wateja na kadhalika. Unapojiajiri utajikuta unafanya kazi za kila idara katika biashara yako. Kuna wakati utavaa kofia ya kiongozi, wakati mwingine masoko, wakati mwingine huduma kwa wateja na kadhalika. Kuwa tayari kubadilika kutokana na hitaji la biashara yako kwa wakati husika.

4. Usichome madaraja.

Kuna dhana moja iliyokuwa ikitumika sana kipindi cha nyuma ambapo mtu alikuwa akiondoa uwezekano wowote wa kurudi nyuma. Kwa mfano kama wewe unataka kuacha kazi na kwenda kujiajiri basi unagombana na waajiri wako kiasi kwamba huwezi kurudi tena kwenye ulimwengu wa ajira, hii inakusababisha uhakikishe unafanya kila mbinu kufanikiwa kwani huna kimbilio jingine. Dhana hii ilifanya kazi sana zamani ila kwa sasa usijaribu kuitumia. Ondoka kwa amani na kama ikiwezekana mwambie muajiri wako unakwenda kufanya nini, mwajiri wako tayari ana mtandao mkubwa hivyo anaweza kukusaidia kupata wateja wa biadhaa au huduma uayokwenda kutoa. Nguvu ya mtandao ni kubwa sana kwenye ulimwengu wa sasa wa biashara na ujasiriamali.

Kujua mambo mengine sita muhimu unayotakiwa kuyajua kabla hujaacha kazi jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa maelekezo yaliyotolewa hapo juu.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kuyaza fomu.

Karibu sana, tuko pamoja.

2 thoughts on “USHAURI; Unawezaje Kuacha Kazi Yenye Maslahi Kidogo Na Kujiajiri?

Add yours

  1. NAkushukuru sana ndugu mwandishi hakika makala zinafundisha na kutoa mwanga wenye mwelekeo sahihi ktk naisha yetu ya kila siku..mungu wangu akubariki pamoja na wote unaoshirikiananao.endelea kutoa elimu hii kwa watanzania na ipo siku km sio leo basi kesho umaskin utabakia historia haswa kwa vijana wa kipato cha chini ktk taifa letu.

    Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: