Zamani kidogo mafanikio kupitia ajira yalikuwa makubwa sana hasa kwa wale waliokuwa wamesoma. Uchumu ulikuwa mzuri, usalama wa kazi ulikuwa wa uhakika na maisha hayakuwa magumu sana. Mtu alikuwa na uhakika wa kukaa kwenye kazi, kupanda ngazi ya uongozi kazini kwa kupandishwa cheo na baadae kuwa afisa mkubwa sana kwenye sehemu yake ya kazi.

Siku za hivi karibunu mambo yamegeuka kwa kiasi kikubwa sana, yaani sasa hivi mambo yanayohusiana na ajira ni kinyume kabisa na miaka ya zamani. Kwanza uchumi umekuwa legelege sana dunia nzima, usalama wa ajira umepotea na maisha yamekuwa magumu sana. Watu wenye sifa za kuajiriwa wamekuwa wengi ila nafasi za kuajiriwa ni chache, hata wale walioajiriwa bado mambo yao sio mazuri sana kwani wakati wowote kuna uwezekano wa kupunguzwa kazi kutokana na kuyumba kwa uchumi wa nchi nyingi duniani. Kwa upande mwingine maisha yamekuwa magumu sana hivyo hata mshahara mfanyakazi anaolipwa haumtoshelezi kukidhi mahitaji yake.

Kutokana na yote haya ni dhahiri kwamba kwa kipindi hiki ni vigumu sana kutajirika au kuwa na uhuru wa kifedha kupitia ajira. Japo kuwa kuna wachache walioweza kupata uhuru wa kifedha kupitia ajira zao kwa sasa ni vigumu sana na kati ya watu mia moja walioajiriwa ni mmoja tu ambaye maisha yake yanaweza kuwa safi na hata yeye akiacha kazi mambo yake yatakuwa sio mazuri.

Kama bado huamini ni vigumu kupata uhuru wa kifedha kupitia ajira soma sababu tano hapo chini kisha utafakari na kuchukua hatua.

1. Muda ni zaidi ya pesa.

Poteza milioni kumi unaweza kuipata nyingine, poteza sekunde moja huwezi kuipata tena daima. Tunachukulia kirahisi sana muda ila huwezi kulinganisha muda na fedha, muda unathamani kubwa sana kushinda fedha.

Tatizo kubwa kwenye ajira ni kwamba unabadilishana muda wako kwa fedha, kwa kifupi unauza muda wako. Kibaya zaidi fedha unayopewa kwa kuuza muda wako ni kidogo sana ukilinganisha na thamani ya muda wako.

Kazi nyingi za kuajiriwa zinachukua muda wako mwingi sana kiasi cha wewe kushindwa kupata muda wa kufanya mambo yako ya pembeni. Wakati mwingine hata kama umemaliza majukumu yako kazini inakubidi usubiri mpaka muda wa kuondoka kazini ufike. Kwa njia hii unakuwa huna mamlaka na muda wako na unapangiwa ufanye nini na kwa wakati gani.

Kama huna mamlaka na muda wako ni vigumu sana kufanikiwa.

2. Kuweka akiba ni kupoteza hela.

Zamani kidogo wakati uchumi ulipokuwa imara mtu aliweza kuwa tajiri kwa kuweka akiba na akiba ile ikakua na baada ya muda akawa na kiasi kikubwa sana cha fedha ambacho kinamwezesha kuishi maisha mazuri. Dhana hii ndio ilileta mifuko ya kujikimu au pensheni ili kuwasaidia waajiriwa kuweka akiba zao kwa ajili ya kutumia uzeeni ambapo watakuwa hawawezi kufanya tena kazi.

Mpango huu ni mzuri sana ila kwa mazingira ya sasa ni hasara kubwa kutunza hela ya akiba kwa muda mrefu. Uchumi umekuwa dhaifu sana na kuna kitu kinaitwa mfumuko wa bei. Mfumuko huu wa bei unakula akiba yako mwaka hadi mwaka, kama uliweka shilingi laki moja mwaka 1999 leo hii thamani ya hela hiyo ni ndogo sana ukilinganisha na kipindi kile.  Hebu niambie kama umeanza kufanya kazi na miaka 25 na ukastaafu na miaka 60 akiba uliyoweka au kuwekewa kwa miaka 35 itakuwa na thamani kiasi gani? Kwa haraka haraka unaweza kuona ni fedha nyingi ila ukiweka mfumuko wa bei na vitu ningine unaweza kukuta nusu ya fedha yako imeliwa.

Kitu pekee kinachoweza kuongeza thamani ya fedha yako kwa sasa ni uwekezaji ila uwekezaji ni mgumu sana kwa mwajiriwa hasa ukizingatia tulichozungumza hapo juu, MUDA.

3. Kukua kuna kikomo.

Unapokuwa umeajiriwa una kikomo cha wewe kukua au kipato chako kukua. Kwa mfano unapoajiriwa mnakubaliana mshahara na unapangiwa majukumu ya kazi ambayo utatakiwa kutekeleza. Ikitokea ukaweza kufanya kazi kwa bidii zaidi ya majukumu uliyopangiwa bado kipato chako ni kile kile, sana sana utakachoweza kufaidika ni zawadi za hapa na pale utakazopewa kama mfanyakazi bora au kupandishwa cheo. Hata ufanye kazi kwa bidii kiasi gani ongezeko lako la kipato linakuwa dogo sana ukilinganisha na nguvu na maarifa uliyowekeza kwenye kazi yako.

Kwenye kujiajiri au biashara mara nyingi hakuna kikomo, ukiongeza nguvu na maarifa kwenye kazi yako unaona majibu moja kwa moja kwa biashara yako kukua na mapato kuwa mengi. Ni ongezeko la kipato ndio litaweza kukupatia uhuru wa kifedha kwenye nyakati hizi ngumu kiuchumi.

4. Nafasi kubwa ni chache.

Moja ya vitu vinavyowapa watu matumaini kwenye ajira ni pale wanapomuangalia bosi wao au mfanyakazi mwingine ambaye alianzia chini na baadae akapanda vyeo mpaka kuwa bosi mkubwa na mwenye maisha mazuri. Hivyo wafanyakazi wengine wanajipa moyo kwamba wakifanya kazi na maarifa wanaweza kufikia mafanikio makubwa kama mmoja wa mabosi wao. Dhana hii ni kweli kabisa kwamba kama ukifanya kazi kwa bidii na maarifa unaweza kufikia hafasi hiyo kubwa kwenye kazi yako. Tatizo ni moja tu. NAFASI HIYO UNAYOIANGALIA kila mtu naye anaiangalia, ni nafasi moja na mpo zaidi ya watu mia moja na hamuwezi kuwa wote kwenye nafasi hiyo kwa wakati mmoja. Unaweza kujitoa sana lakini ukakosa nafasi hii kwa hesabu rahisi tu za probability.

Hii ni tofauti kabisa na kwenye kujiajiri au biashara kwani huku kila mtu anaweza kufikia kiwango kikubwa na cha juu kabisa cha mafanikio bila ya kutegemea au kuzuiwa na mtu mwingine. Nafasi zipo wazi kwa yeyote anayetaka kupata mafanikio, kama ukifanya kazi kwa bidii na maarifa utapata mafanikio makubwa.

5. Huwezi kuuza ajira yako.

Kama maisha yako yote umewekeza kwenye ajira una hasara kubwa kwa sababu huwezi kuuza ajira yako unapofikia ukingoni mwa ajira. Ukifikia muda wako wa kustaafu kufanya kazi unaachia ngazi na wenzako wanaingia. Angalau kungekuwa na uwezekano wa kuuza hadhi ya kazi yako ungeweza kutengeneza faida kubwa ya kukuwezesha kuwa na uhuru wa kifedha.

Kama umejiajiri, kwa mfano umefungua kampuni yako na baadae ukaona huwezi tena kuisimamia kutokana na kuchoka unaweza kuiuza na kupata kiwango kikubwa cha fedha kitakachokufanya uishi kwenye uhuru wa kifedha.

Kuweka asilimia 100 ya muda wako na maisha yako kwenye ajira ni kupoteza muda hasa kama unapendelea kuwa na uhuru wa kifedha(hivi kuna mtu ambaye hapendelei?). Cha muhimu sana ni kujipanga na kuona ni jinsi gani unaweza kuepuka changamoto hizi za ajira na kuwa na maisha mazuri.

Moja ya njia ninazowashauri wengi ni kuweka malengo ni kwa muda gani mtu utafanya kazi yako hiyo na baadae uondoke kwenye kazi hiyo ukafanye kazi zako binafsi au biashara. Ukishindwa kuwa na mpango huu subiri kufa na miaka 35 na kuzikwa na miaka 65.

Nakutakia kila la kheri katika harakati zako za kuboresha maisha yako.

Kumbuka TUKO PAMOJA.