Kwenye makala tatu zilizopita tumejifunza mambo mengi sana kuhusu muda, tunavyoupoteza na jinsi ya kupata muda wa ziada. Mpaka sasa unaelewa kwamba muda ni muhimu na adimu sana zaidi hata ya fedha, kwa sababu ukipoteza fedha unaweza kupata nyingine ila ukishapoteza muda ndio umepotea huwezi kuupata tena. Pamoja na umuhimu na uadimu huu wa muda bado watu wengi hatuchukulii muda kwa umuhimu wake.
Leo tunakamilisha wiki ya mwishi ya mwezi huu wa tano ambapo tulikuwa tunazungumzia tabia ya matumizi mazuri ya muda ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Katika kumalizia huku leo tutajadili mambo muhimu unayotakiwa kufanya au kukumbuka ili kuweza kuwa na matumizi mazuri ya muda wako.
Mambo hayo ni;
1. Pangilia siku yako kabla hujaianza.
Kabla hujaanza siku yako ipangilie vizuri utafanya nini na kwa muda gani. Unaweza kupangilia siku yako kabla ya kulala usiku au ukafanya hivyo asubuhi na mapema. Vyovyote utakavyopanga hakikisha huanzi siku kama hujaipangilia. Kwa sababu unapoanza siku bila kuipangilia utajikuta unafanya mambo ambayo hayana umuhimu kwenye maisha yako hivyo kupoteza muda. Watu wengi sana wanazianza siku zao bila ya kupamgilia, hiki kimekuwa chanzo kikubwa cha kupoteza muda.
2. Jua muda ambao ni wa uzalishaji mkubwa kwako.
Binadamu tunatofautiana na hata mtu mmoja anatofauti ndani ya siku moja. Kuna wakati fulani kwenye siku unakuwa na uzalishaji mkubwa sana, unaweza kufikiri vizuri na kufanya kazi kwa kiwango kikubwa sana. Ndani ya siku hiyo hiyo moja kuna wakati uzalishaji wako unakuwa kidogo sana, hutaki kabisa kufikiri na huwezi kufanya kazi yenye maana. Ni vyema ukajua ni muda gani kwenye siku ambapo una uzalishaji mkubwa. Karibu binadamu wote tunakuwa na nguvu na uzalishaji mkubwa asubuhi tunapoamka. Hii inatokana na kwamba tunakuwa tumetoka kupumzika na hivyo tunakuwa na akili safi ambayo haijaingia sumu. Huu ndio wakati mzuri wa kufanya kazi zako zinazohusisha kufikiri.
3. Fanya majukumu makubwa kitu cha kwanza asubuhi.
Kwa kuwa tumeona muda wa uzalishaji mkubwa ni asubuhi unapoamka, panga kufanya majukumu yako magumu na yanayohusisha kufikiri muda huu wa asubuhi. Kwa kufanya hivi utaona unaweza kukamilisha mambo mengi sana ndani ya siku moja. Amka mapema kama tulivyojadili kwenye makala zilizopita, ukishaamka usiingie kwenye email wala mitandao ya kijamii, bali panga siku yako, jisomee na ufanye meditation. Kisha baada ya hapo fanya lile jukumu kubwa linalohitaji utulivu na kufikiri.
4. Fanya jambo moja ndani ya dakika 90.
Kutokana na majukumu mengi tuliyonayo ndani ya siku moja kuna wakati tunafikiri kukaa na kufanya kazi kwa muda mrefu ndio tunaweza kuimaliza vizuri. Tafiti za kisayansi zinaonesha kwamba uwezo wa binadamu wa kuweza kufuatilia jambo moja kwa makini unaanza kupungua kwa kasi sana baada ya dakika 90. Hivyo kama unafikiri kufanya jukumu moja kwa masaa manne ndio kulimaliza kabisa, zaidi ya masaa mawili utakuwa umeyapoteza. Ili kuepuka kuchoka haraka na kutokamilisha majukumu yako kwa kiwango ulichotarajia tenga muda wako kwa dakika 90. Fanya jambo moja kwa dakika 90 baada ya hapo pumzika kidogo kama dakika 5 na ubadili kufanya jambo jingine. Kwa njia hii utajikuta una uzalishaji mkubwa na kuweza kukamilisha mambo mengi ndani ya siku moja. Ukichukua masaa 24 na kugawa kwa dakika 90 unapata dakika 90 kumi na sita. Ukivipangilia vizuri vipande hivi kumi na sita vya muda utaona ukikamilisha mambo mengi sana.
Kwa mfano kama umeajiriwa unaweza kugawa vipande hivi 16 kama ifuatavyo; Vipande 6 kazini, vipande 5 kulala, kipande 1 kupumzika mchana na vipande 4 vilivyobakia kufanya mambo yako binafsi.
5. Tenga muda wa dharura na muda wa kusumbuliwa kila siku.
Pamoja na mipango mizuri tunayoweza kuweka kwenye matumizi ya muda wetu bado tunaishi kwenye dunia ambayo imejaa usumbufu mkubwa. Unaweza kupanga ratiba zako vizuri ila watu wengine wakazivuruga. Ili kuepuka kuvurugwa na upotevu wa muda nakushauri utenge muda wa dharura au wakusumbuliwa kila siku. Kwa mfano unaweza kutenga saa moja kwa siku au dakika 90 kama unatumia mfumo huu kama muda wa dharura na kusumbuliwa. Baada ya kutenga muda huu unaweza kuweka kitu cha kufanya katika muda huu ili kutoruhusu upotee kabisa, kwa mfano unaweza kujisomea au kusikiliza kitabu kwenye muda huu. Muda huu unauweka kwa sababu kuna watu wengine muhimu ambao wanaweza kukushababisha upoteze muda wako muhimu. Kwa mfano mnaweza kupanga kukutana na mtu ila akachelewa kufika, unaweza kwenda kazini ukijua utafanya majukumu yako mara kukawa na mkutano uliochukua muda mrefu na mengine mengi.
6. Fanya jambo moja kwa wakati mmoja.
Kuna kitu kimoja watu wengi huwa tunajidanganya sana, tunafikiri tunaweza kufanya mambo mengi ndani ya muda mmoja. Kwa mfano unataka ufanye kazi, huku unasikiliza mziki, huku unafuatilia kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii. Hapo unakuwa unapoteza muda wako kwa sababu hakuna hata kimoja utakachokikamilisha kwa kiwango cha juu. Akili ya binadamu haiwezi kufanya majukumu mengi kwa wakati mmoja. Hivyo kama unataka kuwa na matumizi mazuri ya muda wako fanya jambo moja ndani ya muda mmoja, muda ukiisha hamia kwenye jambo jingine. Mawazo yako yote yawe kwenye jambo unalofanya kama unataka kuwa na uzalishaji mkubwa na wa kiwango cha juu.
7. Tenga muda maalumu wa kuingia kwenye mitandao ya kijamii na kupata habari.
Mitandao ya kijamii na ufuatiliaji wa habari ni vitu vizuri sana, ila sio vitu vya kuanza navyo siku yako, labda uwe umepanga kuipoteza siku hiyo. Jitengee muda maalumu kila siku ambapo utaingia kwenye mitandao ya kijamii, utasoma na kujibu email na utafuatilia habari zinazoendelea. Ingekuwa vizuri sana kwako kama mambo haya ungeyafanya baada ya kukamilisha majukumu makubwa uliyojipangia kufanya ndani ya siku hiyo.
8. Jifunze kusema hapana.
Hijalishi unafanya kazi gani au unapendelea kufanya nini kama huwezi kusema hapana hutaweza kuwa na matumizi mazuri ya muda wako. Kwa mfano unapokuwa unafanya jambo ambalo ni gumu la linakuhitaji ufikiri sana akili yako inaanza kutafuta njia za kutoroka, unajikuta unaanza kufikiria labda uingie kwenye mtandao kidogo na kuangalia ni kitu gani kinaendelea. Sema hapana na endelea na jukumu lako, ukishindwa kusema hapana na kufuata mawazo yako utajikuta kila mara unakwepa kufanya majukumu makubwa. Pia weza kusema hapana kwa watu wako wa karibu pale wanapokutaka ufanye jambo ambalo halina msaada mkubwa kwako au kwao na pia linaingilia ratiba zako ulizojipangia kwa siku.
Haya ni baadhi ya mambo unayotakiwa kufanya au kukumbuka ili kuweza kuwa na matumizi mazuri ya muda wako. Endelea kuwa na matumizi mazuri ya muda kwani hii ndio tabia muhimu sana ya kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Zoezi la leo.
Kwa kuwa ndio tunamaliza kuhusiana na tabia ya matumizi mazuri ya muda, leo naomba ukamilishe kwa zoezi hili moja.
Weka ratiba yako ya kudumu ya matumizi yako ya muda kila siku. Fuata ratiba hii na kuiboresha kila siku ili uweze kuwa na matumizi mazuri sana ya muda. Unaweza kupangilia ratina zako za siku, wiki, mwezi na mwaka kwa kutumia GOOGLE CALENDER kama una account ya google. Google calender imeunganishwa na calender ya simu kama unatumia smartphones. Hivyo unaweza kupanga ratiba zako kwenye kalenda ya simu yako au ukapanga kwenye google kalender. Kufika google calender tumia link hii https://www.google.com/calendar
Naamini umejifunza mengi kwenye mwezi huu wa kujenga tabia ya matumizi mazuri ya muda. Kujifunza tu hakutoshi ila unapochukua hatua ndio unakamilisha kujifunza. Nakusihi sana uchukue hatua kwa yale uliyojifunza na utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.
Mwezi wa sita tutajadili tabia ya kujisomea.
Nakutakia kila la kheri kwenye harakati za kuboresha maisha yako, kumbuka TUKO PAMOJA.