Mpaka sasa unajua kuna umuhimu mkubwa wa wewe kujijengea tabia ya kujisomea. Na pia unajua kwa kujijengea tabia hii utaweza kuboresha maisha yako kwa kiwango kikubwa sana. Kama bado hujajua haya bonyeza hapa ili kujua umuhimu wa kujijengea tabia hii.

Kwa kifupi ni muhimu sana kujijengea tabia ya kujisomea kwani kupitia tabia hii unaweza kuongeza ujuzi na utaalamu wako haraka zaidi. Kwa sasa tunaishi kwenye ulimwengu ambao mambo yanabadilika kwa kasi sana, kama na wewe huna kasi ya kubadilika ni lazima utaachwa nyuma. Kuna vitu vingi vilikuwa vinaonekana ni vya thamani sana miaka mitano iliyopita ila kwa sasa havina thamani kabisa. Kila kukicha wanasayansi wanakuja na ugunduzi mpya ambao unapunguza idadi ya watu wanaohitajika kufanya kazi. Hivyo kama unaamini baada ya kupata elimu ya shuleni na chuoni unaweza tu kufanya kazi bila ya kuendelea kujifunza, miaka michache ijayo utaamka ujikute huna kazi ya kufanya.

Kwa nini watu wengi hawana tabia hii ya kujisomea?

Hili ndio swali muhimu sana la kujiuliza siku ya leo, ukishindwa kujiuliza na kujijibu swali hili hata ungekusanya vitabu vingapi bado utashindwa kuvisoma. Kwanini huna tabia ya kujisomea na kujifunza binafsi?

Kuna watu wanapenda sana kujisomea, kila wanapopita na kukutana na kitabu kizuri wanakinunua. Ila inapofika wakati wa kusoma anashindwa kukaa chini na kusoma, anajikuta anaahirisha na kufanya mambo mengine mpaka anasahau kusoma kitabu alichopanga kusoma. Kuna watu wana library nyumbani kwao ila hawajaweza kumaliza hata kitabu kimoja wanachomiliki.

Hii yote inatokana na kitu kimoja kikubwa, MTAZAMO WAKO JUU YA KUSOMA. Unaweza kufikiri ni uzembe au uvivu wako kushindwa kukaa chini na kusoma kitabu, lakini kwa sehemu kubwa umejengewa mtizamo hasi na mbovu sana juu ya kusoma.

Hebu tuangalie maisha yetu tangu utoto ni jinsi gani tunajengewa mtazamo mbaya juu ya kusoma.

Ulipokuwa mtoto na ukapelekwa shule, kwanza ulitoka nyumbani ambapo muda mwingi ulikuwa unacheza na kufanya vitu ambavyo unapenda mwenyewe kufanya. Baada ya kuanza shule, ghafla unahamishwa kutoka kufanya vitu unavyopenda kufanya na kufundishwa kusoma. Kufundishwa huku sio hata kwa kushawishiwa au kubembelezwa, ni kwa viboko na adhabu pale unaposhindwa kufanya kile ulichoambiwa ufanye.

Kwa njia hii ya adhabu pale unapofeli masomo yako unajijengea msimamo kwamba KUSOMA=ADHABU na sababu pekee inayokufanya uendelee na adhabu hiyo ni kwa sababu unaambiwa usiposoma na kufaulu maisha yako yatakuwa magumu.

Kauli hii inakujaza woga kwamba ili maisha yako yawe mazuri ni lazima usome na kufaulu(kitu kizuri), ila kwa kuwa kusoma kwenyewe ni kwa adhabu unajijengea nadhiri kwamba pale tu utakapohitimu masomo yako kusoma ndio basi tena.

Hii ndio sababu kubwa inayowafanya watu washerekee sana pale wanapomaliza masomo yao. Hii ndio sababu kubwa inayowafanya watu wauze vitabu vyao baada ya kumaliza masomo. Hii ndio sababu kubwa inayosababisha wanafunzi kusoma pale tu wanapokuwa na mitihani. Nafikiri umeweza kupata picha ni jinsi gani mtizamo huu mbovu ulivyokuondolea wewe tabia nzuri ya kuweza kujisomea.

ANGALIZO; Ninapozungumzia kujisomea hapa simaanishi kusoma tu chochote mabacho kimeandikwa. Namaanisha kusoma kitabu au maandiko yoyote ambayo yanaongeza ujuzi au utaalamu wako ili kuweza kuboresha maisha yako. Kwa maana hii basi usomaji wa magazeti au aina nyingine za habari hauhusiki kabisa hapa. Kwa sababu habari unazopata kwenye vyombo vya habari kama magazeti kwa asilimia 90 haziwezi kuboresha maisha yako. Ni habari ambazo zinazidi kukujengea mtizamo hasi juu ya maisha kama haupo makini.

Ufanye nini ili kubadili hali hii?
Kama unataka kujifunza na kujijengea tabia hii ya kujisomea cha kwanza kabisa unachotakiwa kufanya ni kwenda kung’oa mtizamo huu mbaya kuhusu kujisomea ambao umepandikizwa kwenye akili yako miaka mingi iliyopita.

Anza kujijengea mtizamo kwamba kujisomea ni tabia nzuri na muhimu sana kwako kama unataka kufanikiwa kwenye maisha haya. Jiwekee nadhiri kwamba siku yako itakuwa haijakamilika kama hutapata muda kidogo wa kujisomea kitu ambacho kitaongeza ubora kwenye maisha yako.

Tenga muda maalumu kila siku ambao utakuwa unajisomea, muda huu hakikisha upo sehemu ambayo sio rahisi kusumbuliwa na ikiwezekana usiwe karibu na simu. Unaweza kuanza na kutenga nusu saa kwa ajili ya kujisomea na kama ukiitumia vizuri ni muda wa kutosha sana kujisomea kila siku. Hata kama upo bize kiasi gani huwezi kukosa nusu saa ya kujisomea kila siku. Kinachokufanya uone uko bize ni mtizamo mbovu uliojijengea kuhusu kujisomea.

Usome vitabu kwa njia gani?

Kama nilivyoeleza kwenye makala iliyopita jinsi utaratibu wa kujisomea ulivyoweza kuwa na faida kwangu, kwa miaka miwili iliyopita mpaka leo nimeshaweza kusoma vitabu zaidi ya 200. Unaweza kujiuliza labda nashinda siku nzima nikisoma kitabu mpaka kiishe, la hasha, ni upangiliaji mzuri wa jinsi ya kusoma ambao nakushauri na wewe uwe nao. Kuna aina tatu za vitabu ambazo unaweza kuanza tabia ya kujisomea kupitia aina hizi;

1. Vitabu vilivyochapwa. Hivi ni vitabu vya kawaida ambavyo unanunua na kuweza kusoma. Kwa vitabu vya aina hii ni muhimu sana kutembea na kitabu popote unapokwenda ili hata unapopata dakika kumi unafungua na kusoma kurasa chache. Kwa mfano mimi ninapokuwa na ahadi ya mkutano na mtu huwa napenda kuwahi eneo la mkutano, nikifika pale wakati namsubiri arudi nafungua kitabu changu na mpaka anapofika najikuta nimeshasoma sio chini ya kurasa kumi.

2. Kuna vitabu vya kusomea kwenye kompyuta au simu. Hivi ni vitabu ambavyo vipo kwenye mfumo wa kieletroniki. Vitabu hivi ni rahisi zaidi kuvipata na unaweza kuwa navyo vingi kwa wakati mmoja. Kwa mfano mimi sijui idadi ya vitabu nilivyonavyo kwenye kompyuta tangu ila ni vingi mno na sijasoma hata robo yake. Vinaweza kuzidi vitabu elfu moja. Changamoto ya kusoma vitabu hivi ni kwamba kama unasomea kwenye kompyuta au simu ni rahisi sana kujikuta umeshaacha na kufanya vitu vingine ambavyo havina msaada kwako. Hivyo unaposoma vitabu kwa njia hii ni muhimu uwe umejijengea nidhamu kubwa.

3. Kuna vitabu ambavyo vimerekodiwa kwa mfumo wa kuangalia au kusikiliza. Katika aina hii ya vitabu unakuwa na vitabu vilivyosomwa na wewe unachofanya ni kusikiliza. Huu ni mfumo ambao naupendelea sana kwa sababu unawqeza kuwa unasoma kitabu hata kama unatembea. Siku hizi kila mtu anaweza kumiliki simu inayoweza kuweka memory kadi. Kwa kuweka vitabu vyako ndani ya memory kadi na kuweka kwenye simu yako unaweza kuvisikiliza popote unapokuwa. Napenda sana kusikiliza vitabu hivi nikiwa natembea, nasafiri au hata nikiwa nimepumzika. Kuna muda mwingi sana unaweza kuwa unaupoteza kwenye foleni au wakati unasubiri kitu au huduma fulani. Ukitumia muda huu kusikiliza vitabu vilivyosomwa utajikuta unajifunza mambo mengi sana.

Leo tuishie hapa ili tuweze kupata zoezi la wiki.

Wiki ijayo tutaona jinsi gani unawezakutenga muda mzuri wa kusoma na ni sehemu gani unaweza kupata vitabu vya kujisomea.

ZOEZI LA WIKI.

Kwa kuwa tumeona tatizo kubwa la kutokuwa na tabia ya kujisomea ni mtazamo hasi juu ya kujisomea, wiki hii tutafanya zoezi la kubadili mtazamo huo. Una mtazamo mbaya juu ya mambo mengi sana kwenye maisha yako, kuanzia mafanikio, hela, furaha na vingine vingi jamii imekujengea mtazamo hasi unaokusababisha uashindwe kupata vitu hivyo.

Kutokana na hilo leo natoa kitabu ambacho kama ukikisoma utaweza kubadili mtazamo wako kwenye kila kitu unachofanya kwenye maisha yako. Kitabu hiki kinaitwa WHY YOU’RE DUMB, SICK AND BROKE (kwa tafsiri isiyo rasmi; KWA NINI WEWE NI BUBU, MGONJWA NA MASIKINI) kimeandikwa na RANDY GAGE. Kupata kitabu hiki BONYEZA MAANDISHI HAYA. Ukikisoma kitabu hiki mwanzo mpaka mwisho utaona ni jinsi gani wewe mwenyewe, wazazi wako, marafiki zako, dini yako, jamii yako na hata serikali inavyokuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa. Sio kwamba wanafanya makusudi, na wao pia hawajui kama wanakuzuia wewe na wao wenyewe kufikia mafanikio makubwa.

Ni kitabu ambacho kitabadili mtizamo wako kwenye maisha.

Kitabu hiki kina kurasa 209 ila zenye maandishi 190 na kina sura 11. Hivyo kama tunataka kukisoma kwa siku saba kuanzia leo jumanne mpaka jumatatu ijayo inabidi kila siku kusoma kurasa 30 tu za kitabu hiki au sura moja na nusu kila siku. Nusu saa kwa siku inakutosha kusoma kwa mpangilio huo. Baada ya kusoma kwa mpangilio huo kila siku tutakuwa tunajadiliana kwenye forum yetu ndogo juu ya yale ambayo tumejifunza kwenye kitabu hiki. Tafadhali tembelea forum yetu kila siku ili tuendelee kushirikishana tumejifunza nini. Kuenda kwenye forum bonyeza FORUM-MAJADILIANO na uweze kuweka mchango wako juu ya yale uliyojifunza.

Nakutakia kila la kheri katika kujenga tabia hii muhimu sana kwako kwa ajili ya kufanikiwa.

TUKO PAMOJA.

Kumbuka kupata kitabu WHY YOU’RE DUMB, SICK AND BROKE bonyeza maandishi haya na kitaanza kudownload.