NA IMANI NGWANGWALU, TANGA TANZANIA

Siku zote huwa naamini maisha tunayoishi tumeyataka wenyewe.Kuna wakati nilikuwa nikisema kauli mbele ya watu nilikuwa nikipingwa sana “aaaah kwa sababu wewe unazo”.Lakini ukweli ni kwamba maisha tunayoishi tumeyataka wenyewe.Nguvu ya kuamini kauli hii inazidi kuwa kubwa ndani mwangu siku hadi siku.

Nadhani umeshaona watu katika maisha ambao kama vile wana mikosi.Katika maisha yao yote ni watu wasio na fedha siku zote,wanapata balaa moja baada ya nyingine,wanafukuzwa kazi,watoto wanafukuzwa shule kwa kukosa karo na balaa zingine chungu nzima zinawakumba.
Watu hawa wanapoulizwa chanzo cha matatizo yao wanakuwa ni watu wa kulalamika na kuzungumzia matatizo yao zaidi. Wakati mwingine wanalalamikia vitu vidogo ambavyo kwa mtu mwenye upeo angeachana navyo. Na kwa bahati mbaya hawajui kwa nini wanaandamwa na hizo balaa kila kukicha.
Sababu ya mambo kuwaendea kombo ni nini? Ni kwa sababu wanafanya kosa hili ambalo pengine hata wewe unalifanya, kosa la kuzungumzia sana matatizo yao na kulalamika. Ukiwa kila wakati ni mtu wa kuzungumzia matatizo utakuwa kweli na matatizo ambayo utashangaa kama hayaishi. Hili ndilo kosa linalowakumba watu hawa kutokana na kufikiri kwao, matendo yao, kuzungumza kwao, na hisia zao huwaumiza wao wenyewe na wanaowazunguka.
Watu hawa wanaona mabaya tu katika hii Dunia.Kwamba wao wameumbwa kwa mabaya tu hapa Duniani na mazuri hawayaoni. Wanajikuta kila wakati wanazungumzia mambo mabaya tu katika maisha yao huku wakidai kwamba wao ni watu wazuri. Wasichojua ni kwamba kila unapozungumzia tatizo kinachokupata ni tatizo. Hivyo kutokana na kuzungumzia sana matatizo na kuwaza mambo ambayo siyo mazuri wanajikuta wanavuta mambo mengi sana hasi katika maisha yao na ndio yanakuwa yao.
Sasa ufanye nini ili uondokane na hali hii ya kulalamika na kupata kile unachokihitaji? Kitu unachotakiwa kufanya ni wewe mwenyewe kubadilika na kuachukua jukumu la kufanya mambo yafuatayo:-
1. Acha kabisa kuzungumzia matatizo.
Ni jambo ambalo unahitaji kulifanyia mazoezi kila wakati. Weka mawazo kwenye mambo ambayo unapenda yakutokee kwenye maisha. Achana na biashara ya kuwazia matatizo haiwezi kukufikisha popote kule. Kuna kanuni bora inayosema “kila kitu kina Chimbuko Lake”. Sasa chimbuko la wewe kuwa na maisha mabaya ninini? Wengi wetu tunasingizia sana majibu ya nje lakini majibu ni sisi wenyewe. Hebu jifunze hili kwa makini, zungumza wakati wote juu ya ushindi tu. Usifanye kosa wanalofanya mamilioni ya watu Ulimwenguni kuzungumzia matatizo yao (Unaweza kusoma pia Kanuni ya kupata kile unachokihitaji katika maisha)
clip_image002
2. Jiangalie kwa makini jinsi unavyojiona.
Watu wengi tunajiangalia kihasihasi, tunajiona hatufai, tuna mawazo duni, hatuna mchango wowote na tunajiona ni watu wa kulogeka pia. Vile vile wakati mwingine tunajiona thamani zetu ni ndogo sana ukilinganisha na za wengine, hasa kutokana na tofauti zetu ziwe za maumbile au kujifunza.
Hii yote inatokana na kwamba wengi wetu tumekuwa tukifikiri kwamba sifa za nje, ambazo binadamu wamepeana zina maana sana.Kwa sababu hiyo watu wanakuwa wanasahau sifa za ndani ambazo zinamwongoza binadamu katika uthamani wake halisi.Kumbuka kwamba thamani ya mtu ipo ndani ya mtu mwenyewe na si nje ya hapo hivyo angalia usijidharau badili mtazamo wako hasa kutokana na unavyojitazama.
3. Badili imani zako.
Kama ulikuwa mtu wa majanga na unaamini utaendelea kuyapata utayapata kweli. Wapo watu ambao matatizo wanayaona na wanaendelea kuyaona kama sehemu ya maisha yao.Sasa badili imani zako kwa kujifunza kwamba hata wewe unaweza kuwa mtu wa mafanikio tena makubwa.Ingawa mazingira uliyonayo sasa hayaridhishi na hayakupi ushirikiano mzuri we amini tu wewe ni mtu wa mafanikio.
4. Weka mikakati ya kukabiliana na hali ya kuwa mtu mwenye mawazo kwa kufanya tahajudi (Sala), Kusikiliza muziki uliotulia na mazoezi ya viungo.
Muziki uliotulia, mazoezi ya viungo au sala vitakusaidia kuwa na hisia nzuri zilizotulia. Kama kuna baadhi ya watu walikukera au hali fulani zinakuudhi kaa mbali na hao watu na hizo hali.
Maana kuwa na hisia zilizotulia na za amani mara kwa mara ni jambo jema sana kuvuta unachokitaka katika maisha yako.
Kwa mambo hayo uliyojifunza naamini utabadili mwelekeo wako na kuwa tena mtu wa kuwaza chanya na si kulalamika. Ukichukua hatua ya kubadilika utaanza kuvuta mambo mengi mazuri na mafanikio utayaona.
Nakutakia kila la kheri tupo pamoja katika safari ya mafanikio.
UNAWEZA KUWASILIANA NA MWANDISHI WA MAKALA HII IMANI NGWANGWALU KWA 0767048035.
KAMA NA WEWE UNA MAKALA NZURI ULIYOANDIKA NA UNAFIKIRI INAWEZA KUWAAMSHA WATANZANIA TAFADHALI NITUMIE KWENYE amakirita@gmail.com
MAKALA ISIWE IMEWEKWA KWENYE BLOG AU CHOMBO KINGINE CHA HABARI, IWE IMETUMIA KISHWAHILI RAHISI NA KINACHOELEWEKA NA IWE NA MANENO KATI YA 500 NA 1000 KARIBU SANA.