Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu RICH DAD, POOR DAD ambapo kwenye makala iliyopita tulichambua utangulizi wa kitabu hiki.
Robert akiwa na miaka tisa(mwaka 1956), siku moja alimuuliza baba yake baba nawezaje kuwa tajiri? Baba yake aliacha gazeti alilokuwa anasoma na kumuuliza kwa nini unataka kuwa tajiri? Robert alimjibu kwamba siku hiyo mwanafunzi mwenzake anayeitwa Jimmy alichukuliwa na gari la mama yake pamoja na marafiki zake na wakaelekea ufukweni. Lakini yeye Robert pamoja na rafiki yake Mike hawakualikwa kwa sababu wao ni masikini.
Baba yake alionesha kusikitishwa sana na hali hiyo ya Robert kuachwa kwa sababu yeye ni masikini, aliendelea kusoma gazeti bila ya kumjibu chochote. Robert aliendelea kusimama pale akisubiri jibu, baadae baba yake alimjibu; mwanangu kama unataka kuwa tajiri ni lazima ujifunze jinsi ya kupata fedha. Robert alimuuliza nawezaje kujifunza jinsi ya kupata fedha, baba akamjibu tumia kichwa chako. Robert hakupata jibu jingine kutoka kwa baba yake.
Kesho yake Robert alimfata rafiki yake Mike na kumwambia kile alichoambiwa na baba yake. Robert na Mike ndio watoto wanaotoka familia masikini ambao walikuwa wanasoma kwenye shule hiyo. Na hiyo ilitokana na wao kuishi karibu na eneo wanaloishi watu matajiri. Robert na mike walikubaliana kuwa washirika kwenye biashara ili waweze kupata fedha. Walitumia siku nzima kufikiria wazo la kufanya ili wapate fedha na iliofika jioni walipata wazo moja walilojifunza kwenye sayansi darasani.
Kutengeneza fedha.
Robert na Mike walikubaliana kukusanya makasha ya dawa za meno yaliyotumika na kuyayeyusha ili kupata madini ya nickel. Kesho yake waliamka na kuanza kupita nyumba kwa nyumba wakiomba kupewa makasha ya dawa za meno yaliyokwisha kutumika. Kila mtu aliwapa na walipoulizwa wanapeleka wapi walisema hawawezi kusema kwa sababu ni siri ya kibiashara.
Baada ya kukusanya makasha ya kutosha walianza kuyayeyusha ili kuweza kupata madini waliyotaka. Walifanya kazi kwa juhudi sana na jioni baba yake Robert aliwakuta wamechafuka vumbi kwa kazi ile. Aliwauliza mnafanya nini? Robert akamjibu tunatafuta fedha ili tuwe matajiri kama ulivyosema. Akawaambia wanachofanya ni kinyume na sheria.
Walikata tamaa sana baada ya kuambiwa wazo lao haliwezekani. Robert alisema Jimmy na rafiki zake walikuwa sahihi, sisi ni masikini na hatuwezi kuwa matajiri. Baba yake alimsikia na kumwambia usitumie tena kauli hiyo, aliwaambia utakuwa masikini pale unapokata tamaa. Na pia aliwatia moyo waendelee kufikiria ili kuja na wazo zuri zaidi. Aliwapongeza kwa kuchukua hatua kwani watu wengi hupanga kuwa matajiri ila hawachukui hatua.
Robert alimuuliza baba yake kwa nini wewe sio tajiri? Baba yake akamjibu yeye sio tajiri kwa sababu amechagua kuwa mwalimu na walimu hawana mpango wa kuwa matajiri, wanapenda tu kufundisha. Akawaambia kama wanataka kujifunza kuwa matajiri amuulize baba yake Mike. Alisema baba yake Mike anaonekana kuwa na mipango mizuri ya fedha na siku chache zijazo atakuwa tajiri mkubwa.
Robert na mike walikubaliana kumwomba baba yake mike awafundishe jinsi ya kuwa matajiri. Kwa kuwa baba yake Mike alifanya kazi muda mrefu ilibidi mike amsubiri mpaka usiku ili kufikisha ombi lao. Siku hiyo alifikisha ombi lao na baba yake Mike alikubali kuwafundisha watoto hawa wawili jinsi ya kuwa matajiri.
Kwenye makala ijayo tutaona kilichoendelea katika kujifunza kuwa matajiri.
TUNAJIFUNZA NINI KATIKA SEHEMU HII?
Kuna mambo mengi ya kujifunza hapa, baadhi ni;
1. Ni muhimu kujifunza jinsi ya kupata/kutengeneza fedha kama mu anataka kuwa tajiri.
2. Ni muhimu sana kufikiri vizuri ili kupata wazo zuri la kibiashara.
3. Matendo ni muhimu sana kuliko mipango.
4. Wafanyakazi wengi hawajifunzi jinsi ya kuwa matajiri, wanapenda tu kufanya kazi zao.
5. Umasikini sio mzuri kwa sababu unakufanya utengwe au upate hisia za kutengwa.
Naamini unaendelea kujifunza vizuri kupitia uchambuzi huu wa vitabu. Kwa mijadala zaidi juu ya uchambuzi huu tafadhali karibu kwenye FORUMS ZA MAJADILIANO ili tuendelee kujifunza zaidi.
TUKO PAMOJA.
kiongozi asante kwa kunitoa kwenye tatzo la akil litwalo UTINDIO Wa UBONGO,kwani mafundisho haya yanatbu sana tatzo hilo.anayekufa maskin utindio huwa umemtawala kwa 90%.asante kwa TBA nzur
LikeLike
Asante sana Godlove,
TUKO PAMOJA.
LikeLike