Tunaishi kwenye ulimwengu wa taarifa ambapo wenye taarifa sahihi ndio wanaotawala. Kwenye kila nyanja ya maisha au chochote unachofanya au kutegemea kufanya ni muhimu sana kuwa na taarifa sahihi. Na hata unapokuwa na taarifa sahihi ni muhimu kuendelea kupata taarifa sahihi kila siku ili usije kuachwa nyuma na dunia hii inayokwenda kwa kasi sana.

Watu wengi wamekuwa wakishindwa kufanya mambo makubwa au kushindwa kupambana na changamoto wanazokutana nazo kutokana na kukosa taarifa sahihi.

images

Leo tutajadili umuhimu na jinsi ya kupata taarifa sahihi kwenye jambo unalofanya au unalotegemea kufanya. Kabla hatujaangalia hilo, tupate maoni ya msomaji mwenzetu alieomba kutatuliwa changamoto hii.

Changamoto yangu ni kutokupata taarifa sahihi
juu ya kile ninachotamani kufanya
.

Kama alivyosema mwenzetu hapo juu, kuna watu wengi pia ambao wanapata changamoto hii ya kukosa taarifa sahihi kwa jambo wanalofanya au wanalotarajia kufanya.

Umuhimu wa kupata taarifa sahihi.

Ni muhimu sana kupata taarifa sahihi kwa jambo lolote unalofanya au kutarajia kufanya kwa sababu;

1. Dunia inabadilika kwa kasi sana. Mambo ambayo yalikuwa yanaonekana yana faida kubwa miaka mitano au kumi iliyopita sasa hivi hayapo kabisa. Hivyo kubaki na taarifa zilizokusaidia huko nyuma kunaweza kuwa kikwazo kwako kufikia mafanikio makubwa.

2. Teknolojia inakua kwa kasi kubwa sana. Matumizi ya teknolojia yanaongezeka kwa kasi sana, sasa hivi karibu kila kazi inayofanyika na binadamu inaweza kurahisishwa na teknolojia.

3. Kuondokana na umasikini. Kukosa taarifa sahihio kumekuwa ndio chanzo namba moja kwa watu wengi kushindwa kuondoka kwenye umasikini.

4. Kupata maarifa zaidi. Unapokuwa na taarifa sahihi unakuwa na maarifa ya ziada na machaguo mengi zaidi yatakayokuwezesha kufikia malengo yako kwa haraka na vizuri. Kukosa taarifa sahihi unakosa nafasi nzuri ya kuwa na machaguo mengi.

5. Kuepuka wakatisha tamaa. Kwenye kila jambo utakaloamua kufanya lazima kuna watu watakukatisha tamaa. Watakuambia hiki hakiwezekani, au unachofanya hakina soko au wateja, au watakuambia fulani alifanya kama wewe na akashindwa. Kama huna taarifa sahihi ni lazima utakubaliana nao na kukata tamaa. Ila unapokuwa na taarifa sahihi kelele hizi haziwezi kukubabaisha kwa sababu unajua ni kitu gani unafanya.

Unawezaje kupata taarifa sahihi?

Tunaishi kwenye ulimwengu ambao taarifa sahihi zinapatikana kwa urahisi kuliko kipindi chochote kuwahi kutokea kwenye maisha ya binadamu. Mendeleo ya teknolojia yamerahisisha sana utoaji na upokeaji wa taarifa.

Kuna njia nyingi sana za kupata taarifa sahihi, hapa nitazungumzia chache ambazo zinaweza kutumiawa na kila mtanzania na akapata taarifa zitakazomuwezesha kufikia mafanikio makubwa sana.

1. Kujisomea na kusikiliza vitabu.

Naweza kusema hii ni njia ambayo ni rahisi sana kupata taarifa sahihi ya kile unachotaka kufanya. Vitabu vilivyoandikwa au kusomwa vimejaa taarifa nyingi sana ambazo unaweza kuanza kuzitumia mara moja na ukapata mafanikio makubwa sana. Mimi ni mpenzi mkubwa sana wa kusoma vitabu na tabia hii imeniwezesha kufanya mambo mengi sana. Kwa mfano kwanzia mwaka 2012 mpaka sasa nimesoma na kusikiliza vitabu zaidi ya 200. Kujua ni jinsi gani nimeweza kusoma vitabu hivi na jinsi vilivyonisaidia soma makala hii; hivi ndivyo tabia ya kupenda kujisomea ilivyoboresha maisha yangu, inawezekana na kwako pia.

Weka malengo ya kujisomea kitabu kimoja kila wiki kinachohusiana na mambo unayofanya au unayotarajia kufanya.

Silikiza vitabu vilivyosomwa(AUDIO BOOKS) unapokuwa kwenye sehemu ambazo unaweza kuwa unapoteza muda. Kupata AUDIO BOOKS bonyeza maandishi haya.

Kwa tabia hii ya kujisomea unajikuta unapata mawazo mapya kila mara yanayohusiana na kile unachofanya au unachotaka kufanya.

2. Tembelea mitandao inayoandika kile unachofanya.

Kwenye mtandao kuna taarifa nyingi sana, kuchambua ni taarifa gani sahihi kwako ni muhimu kujua mitandao inayoandika mambo yanayohusiana na kile unachofanya au kutegemea kufanya.

3. Zungumza na wale ambao wamekutangulia.

Katika jambo lolote unalotaka kufanya kuna watu ambao tayari wanalifanya duniani. Ila kwa hapa Tanzania kuna baadhi ya mambo unaweza kukuta hakuna anayefanya. Ni vyema ukatafuta watu wanaofanya kile unachotaka kufanya au kinachofanana na hiko ili wakakupa uzoefu wao katika mambo hayo. Hii itakusaidia sana kuweza kufikia mafanikio makubwa.

4. Kuwa na washauri wazuri(MENTORS)

Mara nyingi sana unahitaji kuwa na mtu ambaye atakushauri na atakayekuangalia kwenye kile unachofanya. Ni muhimu sana kuwa na mshauri wako wa karibu ambaye sio atakuwa tu anakushauri, bali pia atakuwa nakufuatilia ili kujua maendeleo yako kama ni mazuri au la. Kupitia mshauri wako(MENTOR) utapata mambo mengi sana ya kuweza kukusaidia kufikia mafanikio makubwa.

5. Epuka wakatisha tamaa.

Hii haijakaa kwa mtiririko wa jinsi gani ya kupata taarifa sahihi lakini nimeiweka hapa kwa sababu ni muhimu sana kufanya hivi. Kama utaendelea kukaa na watu ambao hawajui ni kitu gani wanafanya kwenye maisha yao watakurudisha nyuma. Hivyo hata kama unapata taarifa sahihi halafu unakuja kutumia muda wako mwingi na wakatisha tamaa ni kazi bure kwa sababu utajikuta unashindwa kutumia taarifa sahihi ulizopata.

Huu ni ulimwengu wa taarifa na hivyo ni muhimu sana kwako kupata taarifa sahihi. Kwa yeyote ambaye bado anasumbuka kupata taarifa sahihi anaweza kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA na akajifunza mengi sana yatakayomuwezesha kufikia mafanikio makubwa sana. Na kwa ambaye anahitaji mentor anaweza kujiunga na MENTORSHIP PROGRAM ya AMKA MTANZANIA na akapata mengi sana(kupata maelezo ya mentorship tuma email kwenda amakirita@gmail.com)

Nakutakia kila la kheri kwenye safari ya kufikia mafanikio makubwa.

TUKO PAMOJA.