Kuna neno moja ambalo linaweza kuleta maajabu makubwa sana kwenye maisha yako.

Neno hili la maajabu ni siri ya kuwafanya wengine wafanye kile unachotaka.

Neno hili la maajabu ni siri ya kupata chochote unachotaka.

Neno hili la maajabu linafundishwa katika dini zote na linatumika katika kada zote za elimu, matibabu, biashara na hata uongozi.

Neno hili la maajabu sio la ajabu, lakini linazalisha majibu makubwa yanayoonekana kama maajabu.

Neno hili ni KUOMBA.

Unakumbuka mstari huu; OMBENI NANYI MTAPEWA. Ni mstari maarufu sana kwenye mafundisho ya dini.

Utapata chochote unachotaka kutoka kwa watu wengine na utapata msaada wowote unaotaka kama tu utaomba.

Ni kupitia kuomba ndio unaweza kupata kazi unayotaka. Ni kupitia kuomba ndio unaweza kupata mtaji wa biashara. Ni kupitia kuomba ndio unaweza kupata punguzo la bei kwenye manunuzi unayofanya. Ni kupitia kuomba ndio unaweza kupata ongezeko la mshahara au ongezeko la faida. Na pia ni kupitia kuomba ndio unaweza kupata mwanamke au mwanaume wa kuoa au kuolewa naye.

Kuomba kumekupatia mambo mengi sana mpaka sasa, na kutakupatia mambo mengi zaidi kama utaweza kutumia vizuri kuomba.

Usilazimishe.

Jinsi gani unavyoomba ni muhimu sana kwa sababu inaweza kupelekea kupata au kukosa unachoomba.  Ni muhimu sana kujifunza jinsi ya kuomba ili uweze kupata chochote unachotaka. Usitake kitu kwa kulazimisha, mtu akijua unamlazimisha kufanya au kukupa kitu hatakubali kamwe kufanya hivyo.

Unapoomba vizuri na kuonesha kwamba unathamini kile ambacho mtu anacho unakuwa kwenye nafasi nzuri sana ya kupata kile unachotaka. Nikupe mfano mmoja, nenda kwenye eneo lolote ambalo hujui uelekeo halafu mfuate mtu anaeonekana kuwepo eneo lile labda muuza magazeti au hata mfanya biashara mwingine na umuombe akuelekeze unakotaka kwenda, nini kitatokea? Atakuelekeza vizuri na wakati mwingine atarudia mara mbili mbili ili kuhakikisha umeelewa, atakuambia nenda hivi ukifika pale kata kona mkono wako wa kushoto utaona kitu fulani…… Lakini fanya hivyo na mwambie mtu nataka unielekeze sehemu fulani, wala hatahangaika na wewe. Kinachomfanya mtu asumbuke kukupa maelekezo ya unapotaka kwenda ni kwa kuwa umemuomba vizuri na katika kumuomba kule umethamini kwamba yeye anajua zaidi eneo lile kuliko wewe.

Ukiweza kutumia siri hii kwenye maisha yako ya kawaida utapata vitu vingi sana unavyohitaji.

Kwa nini unaogopa? Hakuna chochote utakachopoteza.

Unaogopa kuuliza au kuomba kile unachotaka?

Unaogopa utaambiwa HAPANA?

Watu wengi wanaogopa kuomba kile wanachotaka kwa kuogopa kuambiwa HAPANA. Unapoogopa kuuliza kwa sababu utajibiwa hapana unakuwa tayari umejinyima mwenyewe. Kuna kauli moja inasema JIBU NI HAPANA MPAKA UTAKAPOULIZA. Hivyo kama usipouliza jibu ni HAPANA. Na utakapouliza unaweza kujibiwa NDIO au HAPANA. Ukijibiwa ndio utakuwa umetimiza lengo lako. Ukijibiwa hapana pia utakuwa umejifunza kitu. Kujibiwa hapana hakukupotezei chochote, kwa sababu hicho unachoomba haukuwa nacho mwanzoni.

Na hata pale unapoomba na kujibiwa HAPANA bado sio mwisho, unaweza kuomba tena na tena na baadae jibu likawa ndio.

Watu wanaposema HAPANA wanamaanisha nini?

Sio kila hapana unayoambiwa ni hapana ya kweli. Ni muhimu sana kulijua hili ili ujue kama utaendelea kuomba au uangalie utaratibu mwingine. Unapoambiwa HAPANA mtu anaweza moja au mchanganyiko wa yafuatayo;

1. LABDA. Watu wengi wanaosema HAPANA kwa ndani kabisa wanamaanisha labda. Wanasema HAPANA kwa sababu hawana uhakika kama kile unachoomba kitakuwa na faida kwao au hakitakuwa na madhara kwao. Kama ukiwahakikishia watu hawa kwamba unachoomba kina manufaa kwao au hakitakuwa na gharama kwao watakuwa tayari kukuambia NDIO.

2. NAFIKIRIA ZAIDI. Baadhi ya watu watakuambia hapana ili wapate muda wa kufikiri zaidi kile ulichoomba. Watu wa aina hii hawapendi kukimbilia kufanya maamuzi kwa sababu hawataki kuja kujutia baadae kwa maamuzi mabovu waliyofanya. Watu wa aina hii unahitaji kwenda nao taratibu na kuwahakikishia kwamba maamuzi wanayokwenda kufanya hawatayajutia. Mfano mzuri wa hili ni kwenye kuomba kuoa au kuolewa, watu wengi huhitaji muda zaidi. Vivyo hivyo unaweza kutumia kwenye biashara na mafanikio.

3. HAPANA. Kuna watu watakuambia HAPANA na kweli wanamaanisha hapana. Watu hawa wanakuwa na sababu zao ambazo wanaamini ni sahihi na hakuna unachoweza kufanya kuwashawishi vinginevyo. Watu hawa ni vyema kuachana nao ili upate muda wa kuomba wale ambao wanaweza kukusaidia.

Neno jingine linaloendana na KUOMBA.

Kuna neno jingine linakwenda bega kwa bega na KUOMBA, neno hilo ni KUULIZA. Wakati mwingine kuomba ni sawa na kuuliza na wakati mwingine ni tofauti.

Tumia neno KUULIZA ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Kuanzia leo jiulize maswali haya mawili na ujipe majibu yatakayokusaidia;

1. Nawezaje kufanya kwa ubora? Hapa unajiuliza jinsi ya kuongeza thamani ya kile unachofanya. Kama ni kazi jiulize unawezaje kuongeza thamani kwenye kile unachofanya. Kama ni biashara jiulize unawezaje kuongeza thamani kutokana na biashara unayofanya.

2. Nawezaje kufanya zaidi? Hapa unajiuliza jinsi ya kuongeza uzalishaji. Jiulize kulingana na kazi au biashara unayofanya unawezaje kuzalisha zaidi ya unavyozalisha sasa?

Jiulize maswali haya mawili kila siku na kama huna majibu mtafute mtu anayeweza kukujibu na OMBA msaada wake. Ukiweza kupata majibu ya maswali haya na ukayatekeleza una uhakika wa kufikia mafanikio makubwa sana. Kumbuka unaweza kufanya zaidia ya unavyofanya sasa bila ya kujali unafanya kwa kiwango cha juu kiasi gani.

Hayo ndio maneno ya maajabu ambayo yanaweza kukupatia mambo makubwa sana kwenye maisha yako na kukuwezesha kufikia mafanikio makubwa. KUOMBA NA KUULIZA.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)

TUKO PAMOJA.